Ndugu Rais, Tumekusikia sasa na wewe tusikilize

Ndugu Rais, kuna watu hapa nchini kazi yao ni kukosoa tu! Hata pale jambo jema linapofanyika badala angalau wakae kimya wao watatafuta namna tu mpaka wakosoe.

Hata hivyo, wabaya wa mtu siyo wanaomkosoa kwa sababu hawambomoi, bali wanamjenga zaidi kuliko wanaomsifikia kwa unafiki wao. Wakosoaji ndiyo wanaomfanya mwenye busara kufanya mambo ya maendeleo zaidi. Wabaya wako ni hao ambao mchana wanasimama kwenye majukwaa wakikusifikia, lakini ikifika wakati wakukabidhi kijiti mpaka kwa mbinde! Ogopa sana watu hao! Ukifikishwa hapo ikumbuke ile busara isemayo: “Kama kwenda kunakuwa kugumu, basi, acha kugumu kwende!” Kama uenyekiti unakuwa mgumu kupatikana, basi tumbua jipu la Lugumi na uenyekiti utakuja wenyewe! 

Ni kweli wakati mwingine unatoa fursa kirahisi ya kukosolewa. Ukisema mafisadi, wahujumu uchumi wa sukari hawazidi 10 wakosoaji wako watakuuliza, unashindwa nini kutengeneza polisi wako makini 10, wapelelezi makini 10, waendesha mashtaka makini 10, mawakili wenye weledi mkubwa 10 na majaji waadilifu 10 uwakabidhi hao wahujumu uchumi na mafisadi wa sukari 10, walimalize hili jambo ili wananchi na wewe mwenyewe pia mfanye kazi nyingine?

Hadithi ya sukari imechosha. Inachefua! Haifanani kabisa na falsafa ya Hapa Kazi Tu! Baba, kwenye hili la sukari unalalamika, acha! Ndugu Rais umeagiza sukari iliyofichwa itaifishwe, igawiwe bure kwa wananchi na wenyewe wafutiwe leseni wasifanye tena biashara katika nchi hii! Agizo madhubuti kutoka kwa kamanda mkuu wa majeshi yote yaliyopo katika nchi. 

Vijana shupavu, polisi wadogo, watiifu kwa Rais wao na nchi yao wamekamata kilo milioni tano Mbagala peke yake. Tani zingine nyingi sehemu mbalimbali. Kwanza, polisi wakubwa wakasema wanawahoji. Ushahidi uko wazi wanahojiana nini? Sasa sukari nyingine imeachiwa! Eti hata iliyozalishwa Mtibwa, Morogoro nayo iliingizwa nchini kihalali! Mungu huyu! 

Agizo la Rais lilikuwa ni sukari iliyofichwa au sukari iliyoingizwa kwa magendo? Katika hali kama hii wananchi wataona unachokifanya kweli? Kuepusha kufifisha nguvu hii adhimu ya Rais wangu, Baba nitume mimi Ee, Bwana!

Ndugu Rais, tengeneza polisi wako. Amani ya nchi haiwezi kuchezewa kwa kiwango hiki. Lazima Rais ailinde amani ya nchi kwa nguvu zote. Iwe ni kwa mujibu wa sheria au kwa namna nyingine yoyote! Akiwahutubia waandishi wa habari kutoka katika Hoteli ya Kilimanjaro, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema: “Nawaambia hapa kuhusu utawala wa sheria, lakini Mgiriki yule nilimweka ndani. Hana adabu…..!” Baba wanakwambia akili ni nywele, kila mtu ana zake! Ni msahafu tu ndiyo hautenguliwi!

Kuna tuhuma kuwa kuna mtuhumiwa alishirikiana na polisi mkubwa kuiibia Serikali. Sasa unataka polisi wa chini wakamkamate huyo mtuhumiwa aliyeshirikiana na afande wao! Jamani! Utasubiri sana! Wamkamate Lugumi, wampeleleze, na hao hao wamshitaki Lugumi! Ah! Baba! Mbona hii ni ngumu zaidi kuliko ngamia kupenya katika tundu la sindano?

Ndugu Rais, nililiona andiko la mwanamwema Ananilea akimlilia mwanaye waziri juu ya uamuzi wa hovyo, kuwazuia wananchi wasione yanayoendelea katika chombo chao cha uwakilishi, Bunge. Matarajio yake ujumbe ungekufikia! Wengi wengine wamekusihi kusitisha zuio hili ovu ambalo huja lilitolewa kwako kama ushauri ili uongozi wako uonekane ni wa kiimla. 

Hujatamka neno juu ya hilo! Wakati ule ndugu Edward Lowassa, aliniambia: “Kama Rais wako hasomi haya unayoyaandika, huku watu wake wanayasoma, basi ni kwa hasara yake mwenyewe!” Leo tunayaona yanayojiri. 

Watu wamehemewa! Wameshindwa wakiwa na mamlaka makubwa kwa miaka 10sasa wanang’ang’ania kijiti japo kwa mwaka mmoja. 

Hili litaleta mgawanyiko mkubwa katika chama! Hapa ni mawili tu uliyobaki nayo. Ama ufuate nyayo za aliyekuwa Rais wa Malawi Bingu Mutharika au ufanikishe kazi ya mgombea binafsi! Bila hivyo kesho yako siioni kama vile ambavyo kesho ya masikini na wanyonge wa nchi hii siioni!

Wiki iliyopita niliangalia mahojiano yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja kutoka katika kituo kimoja cha televisheni. Mchambuzi kwa umahiri mkubwa akasema: “Kazi anayoifanya Rais wetu ni nzuri sana, lakini kama hatarudisha Azimio la Arusha atashindwa!” 

Hawa wanaosema na kukuandikia watakapojua kuwa husomi au huwasikilizi watavunjika moyo, nao watakuacha! Utakuwa peke yako maana huko uliko huna hata mjomba!

Ndugu Rais kutegemea maombi katika mapambano kunaondoa ujasiri na kuonesha woga. Kuogopa ni kushindwa nusu ya vita kabla ya mapambano.

‘Mtuombee,’ hiyo lugha waachie wenyewe. Mashekhe misikitini, Mapadri, Wachungaji, Maaskofu na Mzee wa Upako makanisani kwao. Mhubiri dini. mpaka wapatikane watu wema ndiyo asikilizwe. Vimburu wanabaki vilevile. 

Huwezi kumwambia kiongozi mwana siasa wa kiswahili ambaye pia ni mfanyabiashara asiajiri kampuni zake kwenye kazi za Serikali akakuelewa. Tenganisha siasa na biashara, ‘full stop.’

Kwa uwezo mkubwa wa kufikiri na upeo wa kuona mbali, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jambo hili alilitungia kanuni, sheria na taratibu akaliita Azimio la Arusha. 

Manyang’au walipopata mwanya wakaliua! Wanaosema sasa, kuwa bila kurudisha Azimio la Arusha tunatwanga maji katika kinu, wataunganishwa na wale wanaosema nchi inapita katika mhemko wa muda. Na baada ya muda si mrefu hawa ndiyo wataonekana ni watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kuona mbali!

Tumekusikia sana baba sasa na wewe tusikilize! Nitume mimi Ee, Bwana!