Ndugu Rais, ukifanya vema lazima tukuambie umefanya vema. Ukiwaapisha makamishna wa Polisi, Ikulu jijini Dar es Salaam, baba ulisikika ukisema, “…Lakini kuna mambo mengine tu ambayo ni ya kawaida ambayo Jeshi letu la Polisi mnatakiwa myaelewe kwamba Watanzania siyo wajinga sana.

Wanafahamu na wanajua ‘kuanalaizi’ mambo.’’ Kwa kulitambua hili baba, Mwenyezi Mungu akutangulie katika kutuongoza.

Ukaendelea, “Niwatolee mfano tu alipotekwa huyo Mohamed tulipata stori nyingi sana za maelezo  kuwa ametekwa na aina fulani ya Wazungu na maelezo mengi sana…Lakini lilipokuja kumalizika hili suala likazua maswali mengi zaidi yasiyokuwa na majibu.’’

Baba kumbuka, alipotangaza tu kuwa Mohamed Dewji ametekwa, hakungojea kumeza mate; pale pale na kwa haraka ile ile akatangaza kuwa waliomteka Mohamed Dewji, siyo raia wa nchi hii. Nikaikumbuka busara ya marehemu mama yangu. Aliniambia, “Mwanangu Ngowe, mwizi hujishika mwenyewe!’’ Wako wanaodhani Watanzania ni wajinga sana. Unautambuaje uraia wa mtu kwa kuitazama tu sura yake kwenye picha? Watakaofikiri kuwa aliyetangaza utekaji na watekaji walikuwa kitu kimoja watakuwa wamekosea wapi?

Kulifufua tukio la kutekwa kwa Mohamed Dewji kumefufua maswali mengi zaidi. Hili jambo limenyamaziwa kwa muda mrefu sana kiasi kwamba labda ingekuwa bora kama lingeachwa liendelee kunyamaziwa. Kwa Watanzania walio wengi hasa wa kule mashambani waliishalisahau jambo lenyewe.

Wenyewe kule waliko wana matatizo ya kila aina na hakuna anayeonyesha kuwajali. Watoto wao wamekosa vyumba vya madarasa hivyo hawakuendelea na shule. Waliobahatika kupata madarasa chini ya miembe wanaandikia chini huku wakiwa wamekaa juu ya mawe. Mzazi gani ataacha kuyafikiria matatizo haya ya watoto wao akamuwazie tajiri kijana mwenye ukwasi mkubwa -Mohamed Dewji? Hata kwa mashabiki wa Simba waishio mijini, Simba ikimfunga Yanga tu wanasahau kama tajiri yao aliishawahi kutekwa. Lakini kwa kuwa baba umelianzisha, basi wanao hatuna jinsi, wacha tuende nalo ila tuende nalo bila unafiki.

Tujiulize, ni nini kilichofanya jambo hili likafukuliwa? Pili, ni kwanini likafukuliwa sasa? Mohamed Dewji hakuwa mtu wa kwanza kutekwa.

Kabla yake waliishatekwa wengi tena kwa mateso makubwa, na wengine inapita miaka sasa hawajulikani waliko! Mohamed ndiye Mtanzania zaidi?

“Halahala mti na macho’’.

Mwanamwema mmoja hata simjui kama ni mtani wangu au vipi, lakini akanitania akasema, “Mwalimu Mkuu unazisifu sana jitihada za Rais Uhuru Kenyatta anazozifanya kuwaunganisha Wakenya na kwamba sasa yeye na wapinzani ni kitu kimoja wameunganisha nguvu zao, wanaijenga nchi yao ya Kenya. Usidhani hayo ni matakwa ya moyo wake, Uhuru Kenyatta!

Hayo ni matokeo ya mtu aliyeionja adha ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita iliyoko Uholanzi! Mwalimu Mkuu, kuna wachunguzi wa kimataifa kule ambao wakikutazama tu kwa makini mwenyewe unasahau jinsia yako!’’ Asante kwa ujumbe.

Ulipoendelea ulisema, “Alikutwa Gymkhana usiku. Watu wakajiuliza

aliendaje pale? Na bunduki zikaachwa pale. Watu wakajiuliza, je, wangekutana na polisi waliokuwa wanawatafuta ingekuwaje!’’ Hapa pana shaka. Umesema Watanzania siyo wajinga sana. Watakaofikiri kuwa waliomteka Mohamed Dewji, ndio hao hao polisi ambao wengine wanadhani kulikuwa na wengine waliokuwa wanawatafuta. Wakifikiri hivyo kuna kosa? Wao walijua yameisha ndiyo maana hawakuzihitaji silaha tena. Wangezihitaji silaha za nini tena wakati kazi wamekwishaikamilisha? Watakaofikiri hivi, wanawema, watakuwa wamekosea wapi! “Wakajaribu kulichoma gari.’’ Watanzania wanajiuliza ili kufuta ushahidi gani? Bado walipewa ofa ya fedha taslimu bilioni moja tunaambiwa hawakuzichukua. Hata Kamanda Mambosasa hakuzihitaji kweli fedha hizi?

Baba uliposhtua ni pale uliposema, “Baadaye tukamwona aliyetekwa anakunywa chai na Mambosasa huku maelezo hayapo! Labda ndiyo mambo ya kisasa kama lilivyo jina la Mambosasa aliyeko hapa Dar es Salaam.’’

Alipofukuliwa Roma Mkatoliki na wenzake, walipelekwa moja kwa moja

hospitalini wakachunguzwe afya zao kwa sababu walijua kuwa walipigwa na kuteswa sana. Kama aliyewapeleka hospitali ndiye aliyewateka na

kuwatesa, hatujui. Roma waambie Watanzania nyinyi chai mlikataa? Aliyekupa kazi ya ualimu kwenye shule ya serikali alikuwa ni mtu wa serikali? Kamanda Mambosasa alikuwa na uhakika wa afya ya mtekwa wake. Alijua hakudhuriwa na alikuwa salama, hivyo wakijipongeza kwa kunywa chai na kachori kuna ubaya gani?

Baba ukaendelea, “Baadaye tukaambiwa aliyekuwa anawa- ‘feri’ (kuwasafirisha) ni huyu hapa. Watanzania walitegemea kesho yake wangemwona mahakamani. Huyu angewataja. Baadaye Watanzania wakaambiwa nyumba alimokuwa amefungiwa hii hapa. Watanzania walitarajia kumjua huyo mmiliki aliyewaachia nyumba watu asiowafahamu. Lakini kimya mpaka leo! Miezi imepita! Hata kama Watanzania watanyamaza, lakini mioyo yao, haitakuwa, ‘clear’, (haitakuwa radhi)’’

Baba kumbuka enzi za uwaziri wako ulivyokuwa kipenzi cha wengi. Kuwa Rais ghafla umekuwa mchapakazi hatari! Kila kukicha unavunja rekodi.

Ni kipi umefanya katika kipindi hiki kifupi ambacho kimeitikisa

milingoti iliyolishikilia jua? Waswahili wanasema mtumikie kafiri upate mradi wako.  Wapuuze hao ni wasaka tonge tu japo hawavunji amri za Mungu!

Ukiwa na mshauri Ninja atakupa ushauri wa kininja hata kama wewe mwenyewe ni mnyenyekevu wa moyo. Atakwambia hakutekwa, bali aliikimbia familia yake baada ya kushindwa kuilisha. Umesema mwenyewe kuwa Watanzania sasa siyo wajinga sana, wanafahamu na wanajua kuana-‘laizi’ mambo. Maninja watakaposoma katika mitandao kuwa zamani ukiwa na fedha nyingi Tanzania uliweza kufanya lolote, lakini sasa ukiwa na fedha nyingi Tanzania unaweza kufanywa vyovyote, Baba hutayaamini macho yako pale utakapowaona maninja wakisukumana kukukimbia! Hili la Mohamed Dewji ni fundo moja katika mnyororo wenye mafundo mengi yanayofunguka. Yatafufuka mengi na mengine ya kutisha zaidi. Utabaki peke yako!

Baba karibu mezani tuongee! Tunachotaka sisi ni amani katika nchi yetu! Tukae kwa amani kama zamani. Kinachotugombanisha tukijue. Je, ni uroho wa kutaka kutawala watu wa Mungu?

Labda ni kweli baba sifai kuwa mshauri wako mzuri. Ungeniaga kuwa unaenda katika ule mkutano ningekuomba usisahau kuchukua majina mawili. Moja la kwenda kumbadili Ninja na la pili la kumbadili Mambosasa. Ukishafanya hivyo unawaambia hao makamanda wapya, “Mmeona? Haya, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu!’’

531 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!