Ndugu Rais, kukumbuka tuliyoyaona na kuyasikia Mbeya wakati wa sherehe za Mei Mosi au Sikukuu ya Wafanyakazi ni kujirejeshea huzuni na simanzi mioyoni! Lo! Maandamano yalikuwa marefu yale! Du! Mabango yalikuwa mengi yale, lakini yote yalibeba ujumbe uliofanana. “Tanzania ya Uchumi wa Kati Inawezekana. Wakati wa Mishahara na Masilahi Bora kwa Wafanyakazi ni Sasa’’.

Du! Wafanyakazi walitema nyongo. Walisisitiza nyongeza ya mishahara kwa nguvu zao zote, lakini kistaarabu. Kistaarabu kwa sababu katika nchi nyingine wakifikishwa hapa walipofikishwa hutangaza mgomo. Hawa wetu hawajagoma. Hapa ni kazi tu!

Maskini wafanyakazi wale walikuwa wanyonge, lakini waliojawa matumaini makubwa. Baada ya tamko la kutokuwa na ongezeko la mishahara ghafla wote ni kama waliugua. Sauti zilizokuwa zimejaa bashasha zikimjibu baba: “Mbeya oyee!” Zilififia.

Hata ilipotangazwa kuwa sasa tupunge mikono juu kumuaga rais wetu anaondoka, ah! Hali ilisikitisha! Hakuna aliyekuwa na hamu tena na yeyote. Wahenga walisema, akufukuzaye hakuambii toka! Yalikosekana maturubai tu, lakini palifanana sana na mahali penye msiba wa mtu mzito. Wanao tunaokupenda tulikuhurumia baba yetu kwa sababu ulitia huruma sana. Tulitamani tukunong’oneze upoze japo kidogo, lakini ulinzi wako, uzio wake ulikuwa kama seng’enge ya umeme.

Tulipokikumbuka kipigo cha mbwa koko alichoshushiwa yule kijana mnyonge wa Makambako, wenyewe tuliifunga midomo yetu! Yeye alidhani palikuwa na baba yake pale! Tuliyoyachuma Mbeya yanatuumiza sasa, lakini yatatuumiza zaidi mwakani. Watu wanatafuta fursa. Mtetezi wa wanyonge katika nchi hii bado hajazaliwa?

Baba, wananchi wengi wa kawaida hawajaeleweshwa vya kutosha faida ya ndege kwao, wakaelewa. Wanaona ni moja kati ya uamuzi uliosababisha maisha yao kuwa magumu zaidi. Walipoambiwa nchi yao ni tajiri sana, wakaona ametokea mkombozi.

Wakora walipokuwa wanajichukulia utajiri wa nchi hii watakavyo, maisha ya wananchi yalikuwa magumu. Leo utajiri wao haujulikani unapelekwa wapi. Mbona maisha yao ndiyo yamezidi kuwa magumu zaidi? Baba, maisha ya watu wako sasa ni magumu na ya kinyonge!

Ni kweli, bure ni ghali! Walisema tembea uyaone. Wanafunzi 150 wa Kijiji cha Kwakibuyu, Muheza, Tanga – wa darasa la nne, tano na sita wanatumia darasa moja wakiwa wamegeuziana migongo na wengine katikati huku wakifundishwa na walimu watatu kwa wakati mmoja.

Elimu bure? Wanaotenga mabilioni ya elimu bure hawajui kuwa wanafunzi wanahitaji kwenda chooni? Iweje wanafunzi 242 watumie tundu moja la choo? Mwalimu Mkuu Msaidizi, Boniventura Mwafute anasema shule inahitaji walimu wanane, lakini wapo wanne tu.

Kule Shule ya Msingi Mlowola, Kilosa, mkoani Morogoro, Mwalimu Elizabeth Mbilinyi anahangaika na watoto 342 wa darasa moja asijue pa kuwaweka. Amewarundika wote sakafuni katika darasa moja kama mifugo.

Watoto wa wananchi wanyonge maskini hawana madawati. Vitabu hawana, lakini hata kama wangekuwa navyo wagevisomaje? Hata hiyo elimu bure wataipataje bila kufundishwa? Mwalimu mmoja afanye nini mama huyu maskini wakati nchi imo katika harakati ya miradi mikubwa?

Hali ya hospitali zetu huko nyuma ilikuwa mbaya, lakini leo ni dawa gani unayoikuta hospitalini? Wagonjwa wanatibiwa kwa vikaratasi wanavyoandikiwa dawa wakanunue. Tunaopitapita mitaani kila mtaa watu ni kulalamika na kulaani. Wamebaki kujiuma vidole.

Baba, uamuzi wako wa ununuzi wa ndege nyingine tatu tena kwa mpigo, hauwezi kupingwa na mwanao yeyote. Lakini baba, kama itakupendeza, nunua ndege mbili kwanza. Fedha ya hii ya tatu sikiliza vilio vya wajawazito wanaoishi katika Kijiji cha Pangamlima, Kata ya Makole, wilayani Muheza, Tanga wanaodai kujifungua watoto wakiwa njiani kutokana na umbali mrefu wa kufuata huduma za afya.

Ndugu Anita Chavike, mshukuruni mbunge wenu Balozi Adadi Rajabu kwa ahadi yake ya kuchangia tani mbili za saruji. Mwombeni asiogope kumsihi baba asinunue ndege ya tatu. Ampelekee ombi langu hili – rais wetu ni msikivu. Wananchi wamechoka na makelele yetu ya kila siku majukwaani. Oh! Tumetenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya afya, lakini hospitalini na katika zahanati zetu hakuna dawa wala huduma bora vya kutosha.

Viongozi wetu wote wanajisikiaje wanaposikia katika hii Awamu ya Tano wajawazito bado wanajifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wa kufuata huduma za afya? Hawa kuwatangazia kununua ndege nyingine tena tatu kwa mpigo ni sawa na kuwachoma vidonda vyao ambavyo havijakauka damu kwa msumari wa moto! Tumwachie Mungu atahukumu!

Kama utaratibu utakaotumika ni ule ule uliotumika kununua ndege zile nyingine tusiwalaumu wananchi wanaodhani kuna faida fulani kwa wanunuzi wa ndege hizo. Wananchi hawashirikishwi wala wawakilishi wao bungeni. Mbona wabunge wetu ni wengi, kinachotufanya tuogope kufuata utaratibu uliopangwa na nchi katika ununuzi wa umma ni nini? Ni kweli watu wengi zaidi wakijua, watajua mengi zaidi?

Ndugu Rais, wewe ndiye baba yetu. Kwa imani ya kitoto baba akiona mbele, anaona mbele zaidi. Watoto wanaposhindwa kuona umbali anaouona baba yao, lawama zao hawazielekezi katika umbali, bali kwa baba yao.

Wengine watasema baba anataka kututesa. Baba muelewa hujitahidi sana anapotekeleza miradi mikubwa kama vile kujenga nyumba ya ziada, anahakikisha maisha ya wanafamilia hayabadiliki na kuwa ya mateso. Busara ni kwamba kama wanafamilia walikuwa wanakula wanashiba waendelee hivyo. Wasilazimishwe kufunga eti kwa kuwa baba anajenga nyumba ya ziada anayotaka kuifanya nyumba ya kulala wageni, eti itaongeza kipato cha familia ikikamilika hapo baadaye.

Lakini baba, kama maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana bila kuwa na ndege za ziada, kuna ubaya gani kama tungepiga ndege mbili mbili kila mwaka ili kuruhusu ununuzi wa ndege uende sambamba na wananchi wanaokula na kushiba, watoto wao wanapatiwa elimu huku na wao na watoto wao wanatibiwa ipasavyo?

Hata katika vitabu vya kale vya wafalme, wafalme ambao wakati wao wananchi waliishi maisha magumu, ilikuja kuthibitika baadaye kuwa ufalme wao haukutoka kwa Mungu, bali ulipatikana kwa hila! Haiwezi kuwa sahihi hata kidogo kufanya miradi mikubwa kama kujenga mapiramidi huku watoto wa Ifakara na wenzao wa sehemu nyingine wakijishibisha kwa uchafu wanaochakurachakura kama kuku majalalani!

By Jamhuri