Ndugu Rais, imeandikwa kuwa mwenye busara akiamua kujenga nyumba, kabla hajafanya chochote, hukaa chini, akachukua kalamu na karatasi na kupiga hesabu! Naye akishapata gharama kamili ndipo huanza ujenzi.

Kazi ya ujenzi na kuistawisha nchi haina tofauti na ujenzi wa nyumba. Nchi yetu kama ni nyumba inahitaji kujengwa upya! Nyumba ikishabomoka hadi katika msingi haiwezi ikakarabatiwa nayo ikawa imara tena kama mwanzo. Inaonyesha hatukukaa chini kabla ya kuanza ujenzi!

Ndugu Rais, uongozi ni karama itokayo kwa Mungu mwenyewe ambayo mwanadamu huzaliwa nayo toka tumboni mwa mama yake! Mwenye masikio ya kusikia na utayari wa kupokea ushauri mwema pia anaweza kuwa kiongozi wa watu. Nchi hii ilibahatika kuwa na Julius Kambarage Nyerere.

Mtu huyu kama wewe ndugu Rais alikuwa mwalimu. Alikuwa rais wetu kwa zaidi ya miaka ishirini na tatu na tangu apite hatujawahi kumpata rais wa kumfananisha naye! Wengine walikuja wakaharibu hata kile chema alichotujengea. Alikotokea wenye kuamini hatukujui mpaka leo! Tumebaki kusema tu, Butiama, Butiama!

Watanzania katika ujumla wao walimtangaza kuwa ndiye Baba wa Taifa lao! Hivi sasa wanawema wako katika mchakato wa kumtangaza kuwa mtakatifu! Chema gani kinaweza kutoka Butiama?

Pamoja na mamlaka makubwa aliyokuwa nayo kama kiongozi wa nchi na mtu ambaye hakudhibitiwa na chama chake wala sheria yoyote, Julius Kambarage Nyerere alijiita ndugu. Akatuita na sisi watu wake, ndugu. Na sisi watu wake kwa kumpenda, kumheshimu na kumwogopa tukamwita ndugu. Nchi ikawa ya wana ndugu tangu rais mpaka makabwela.

Ndugu Rais, watumishi wa wananchi wote ambao ni waheshimiwa, hao siyo riziki! Achana nao! Kama Baba wa Taifa hakuwa mheshimiwa wewe kujiita mheshimiwa ni kuonyesha unyang’au wako! Jitofautishe nao na wewe uwe ndugu kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere! Tatizo la mwanadamu ni kiburi na kujiona. Huwezi kuwa mheshimiwa kwa watu uliowaomba kura ili uwe hapo ulipo!

Baba wa Taifa aliipenda nchi yake bila kuacha shaka yoyote. Aliwapenda sana Watanzania! Hata siku yake ya kuitwa na Muumba wake ilipomfika, akiwa juu ya kitanda chake cha mauti alisema: “Kwa ugonjwa huu najua siwezi kupona! Najua Watanzania watalia sana, lakini mimi nitawaombea kwa Mwenyezi Mungu!” Akanyamaza kimya! Akaitoa roho yake kurudi kwa Muumba wake! Ah! Dunia tambara bovu! Tangu kifo kilipomchukua Baba yetu, Watanzania tumebaki yatima mpaka leo!

Ndugu Rais, kazi unayowafanyia watu wako inawajaza matumaini kuwa huja siku moja watakuja kumpata kiongozi mfano wa Nyerere. Ndiyo maana ya kusema watengenezee Watanzania rais mwingine. Rais mwingine anaweza pia kuwa wewe! Achana na mafisadi wakweli, achana na wakora, achana na manyang’au wote waliowafikisha masikini wa nchi hii hapa walipo.

Nyerere ni upendo, umoja na mshikamano. Achana nao wote waliotumia miaka mingi na fedha nyingi za masikini wa nchi, kuizunguka nchi kuhubiri chuki, wananchi wachukiane kwa ukora wao tu! Ambatana na wananchi wako! Wengi wanakuunga mkono. Kama unawekewa figisufigisu kupewa uenyekiti ni kwa sababu umeonyesha woga katika kuwatumbua majipu yao! Watumbue hadharani wananchi watakuombea! Wacha wabane; wenyewe wataachia!

Julius Kambarage Nyerere katika kuidhibiti volkano inayotutishia kulipuka sasa baada ya pengo la walionacho na wasionacho kupanuka, akatujengea Azimio la Arusha. Katika Azimio la Arusha Watanzania tuliishi kwa haki sawa kwa wote. Viongozi manyang’au waliwekewa vidhibiti mwendo wasiwaibie masikini. Lakini wachafuzi walipokuja bila kitu cha kuwafanyia Watanzania, walianza kuhubiri chuki wananchi wachukiane ili wapate kuwaibia watakavyo! Wamewaibia sana!

Ndugu Rais, kwa kuwa Nyerere alitaka tupendane kama alivyotupenda yeye, alitujengea Azimio la Arusha ndani yake akaweka maadili na miiko ya uongozi ili viongozi manyang’au wasiwaibie wanyonge. Kulitaja Azimio la Arusha mwanamwema aliyejitambulisha kuwa ni Mkinga bila kutaja kama ni jina lake au ni kabila lake akaniandikia akisema: “Bado mpaka leo katika dunia hii ya mwanga unawaza Azimio la Arusha? Unataka wananchi wanyang’anywe mali zao kama Mwalimu alivyofanya?”

Wanawema hawa msiwajibu kwa sababu imeandikwa: “Usimjibu mpumbavu kulingana na upumbavu wake, usije ukafanana naye!” Baadaye watawaambia majipu wanaotumbuliwa na Ndugu Rais anawadhulumu mali zao. Wanapoongea mishipa ya shingo na kichwa inawasimama huku mate yakiwatoka kwa kuwatetea mabwana zao wezi waliowaibia masikini kwa muda mrefu. Walidhani wanyonge wa nchi hii watabaki wanyonge milele. Leo Ndugu Rais yuko na wanyonge wake. Wakati wao wa kujutia dhuluma waliowafanyia Watanzania umewadia.

Ndugu Rais, wanaokufananisha na Nyerere wapuuze kwa kuwa hufanani naye. Lakini kwa urais wako umepewa fursa ya kufanana naye au hata zaidi kama utaamua kujivua utukufu wako wa kujiita mheshimiwa ili uwe ndugu kati ya ndugu zako kama alivyokuwa Mwenyeheri Julius Kambarage Nyerere.

Hata kama siyo kwa kulirudisha Azimio la Arusha zimazima, lakini ukitaka unaweza kuwajengea watu wako hali itakayowarudishia masikini na wanyonge wa nchi hii upendo, umoja na mshikamano wao walivyofaidi ndani ya Azimio la Arusha!

Rudisha maadili na miiko ya uongozi iliyokuwamo ndani ya Azimio la Arusha ili viongozi manyang’au wauheshimu utu wao masikini na wanyonge. Wananchi wameporwa kiasi cha kutosha!

974 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!