Leo (Jumamosi Oktoba 10) naandika makala hii ikiwa zimesalia siku 15 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika. Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 25, siku ya Jumapili. Kanisa Katoliki tayari limetangaza kuwa ibada ya Jumapili kwa baadhi ya majimbo itafanyika Jumamosi ya Oktoba 24, kwa nia ya kuwapa fursa waamini wao waweze kupiga kura siku ya Jumapili.

Katika uchaguzi wa mwaka huu tumeshuhudia kibwagizo cha mabadiliko kikegeuka kuwa sera ya karibu kila chama. Vipo vyama vinavyomaanisha kweli kufanya mabadiliko na vipo vyama vinavyoigiza kuonyesha kuwa vitafanya mabadiliko pia vikipewa nafasi kwa kuwa wimbo huu umebainika kunoga katika masikio ya wapigakura.

Sitanii, yapo mambo mawili si sera, bali yanazungumzwa kwenye mikutano ya vyama vya siasa kwa muhemko mkubwa. Mambo haya ni wizi wa kura na wapigakura kulinda au kutolinda kura. Kabla sijaingia katika undani wa mada hii, kwa kuwa zimesalia wiki mbili kufanya uchaguzi, naomba nichukue fursa hii kumuaga Mhe. Rais Jakaya Kikwete.

Namuaga Mheshimiwa Kikwete si kwa jingine, bali kumkaribisha uraiani. Uraiani kuna mazuri mengi huku. Wastaafu wanalindwa lakini si kwa kiwango cha ulinzi wako wa sasa. Kuna siku nimeshuhudia una wapambe (aide de camp) watatu. Sawa na Kanali Mohamed Gaddaffi kati yao walikuwapo walinzi wa kike na wa kiume. Wingi na idadi ya walinzi ikanitisha.

Najua Mheshimiwa ulizoea kusafiri mara nyingi nje ya nchi. Sina kumbukumbu katika uongozi wako ni lini umelala Tanzania kwa mwezi mzima. Najua ulikuwa unapata mialiko, lakini siamini kuwa waalikaji walikuwa wakikulipia nauli, gharama za malazi na wasaidizi wako bila kutumia hata senti ya Watanzania. Fedha zilizotumika sina uhakika kama unazifahamu.

Hata hivyo, Mheshimiwa nisamehe kidogo na nivumilie nikueleze haya yafuatayo. Pengine bila kujua, kwa muda uliokuwa unakaa nje ya nchi kiwango cha wafanyabiashara kukwepa kodi kiliongezeka mara dufu. Hospitalini dawa ziliisha, na hata hivi ninavyoandika hazipo, bali nje ya kila hospitali ya serikali madaktari wamejenga maduka ya dawa.

Mahakamani ndiko usiseme. Mlalamikaji anaweza kushinda kesi mwaka huu, na asiipate hukumu milele. Mfano mimi gari langu liligongwa mwaka 2008. Nikaenda Mahakama ya Wilaya Ilala. Kesi iliendeshwa nikashinda kesi, baada ya hapo nikaandika barua ya kuomba hukumu. Amini usiamini hadi leo sijapewa nakala ya hukumu. Nilifuatilia hadi nikakata tamaa. Bahati nzuri hata bima ni waelewa, walinitengenezea gari wakasema ningekuwa wa kwanza kuipata hukumu kati ya wateja iwapo ningefanikiwa.

Sitanii, Mheshimiwa Kikwete inawezekana walio karibu na wewe hawakwambii  ukweli. Bei za bidhaa mitaani ni kichaa. Ile inayoitwa Tume ya Ushindani wa Haki haifanyi kazi tena. Kwa mfano mgonjwa anayeumwa shinikizo la damu, akiwa anatumia vidonge kama Repace – H, akienda Kariakoo anauziwa kidonge Sh 450, akienda Temeke anauziwa Sh 1,000 na akiwa Ngara kidoge hicho hicho kinauzwa 1,200.

Leo wakati tunasema uchumi wa nchi shilingi imeshuka, wala tusijiulize. Watanzania hawamuoni mwenye kuusimamia uchumi. Nyumba za kupanga uswahilini watu wanapangisha kwa dola. Maembe na nyanya zinauzwa kwa dola. Mwananchi asiye na safari nje ya nchi ananunua dola idadi atakayo na kuzitunza nyumbani kwa madai kuwa shilingi haiaminiki.

Nikiri kuwa kama nchi tunafahamu aina ya madini tunayochimba, lakini hatujui kiasi gani tunachimba au tunauza nje ya nchi. Kwa hisani na huruma tu, wawekezaji wanatumegea makombo. Shilingi yetu haiwezi kuwa imara wakati hakuna tunachouza nje ya nchi. Pamba, kahawa, korosho, mkongo, mawese, karafuu na kila zao liwalo la biashara limekufa.

Tulikuwa na viwanda vya nguo 12, leo Mheshimiwa Kikwete sijui kama tukiacha watoa nakala wanaochapa kanga na vitenge baada ya kununua vitambaa (clothes) kutoka nje ya nchi wakati pamba tunayo hapa kwetu, iwapo tuna hata kiwanda kimoja cha kusokota nyuzi. Hatusokoti nyuzi tena, tumebaki kuwa watu wa kudalizi. Tafuta kwenye maduka yote, ukute kitu kilichoandikwa MADE IN TANZANIA.

Sitanii, nikuhakikishie kuwa vipo vitu vingi vinatengenezwa hapa nchini, lakini vinaingizwa sokoni kwa magendo. Juzi hapa nilitaka kufungua kibanda cha kuranda mbao. BRELA sina shida nao. Ukitaka kusajili kampuni kwa sasa hakuna shida. Sasa ngoma nenda kutafuta leseni. Nilipofika Ilala Manispaa nikaambiwa napaswa kuilipia leseni Sh 200,000, nilipie gharama za kukagua eneo ilipo biashara na ikaongezwa kuwa ili niweze kupatiwa hiyo leseni ni lazima niwe na tax clearance kutoka TRA.

Nikaenda ofisi moja ya Shaurimoyo kuomba tax clearance nikaambiwa nilipe kodi. Nikawauliza nalipaje kodi kabla zijaanza hata biashara na wala sijui kama biashara itatembea au itanidodea? Wakasema hilo ndilo sharti la msingi, na hawawezi kunipa tax clearance hadi nilipe kodi. Baada ya kuelezwa hayo nikarudi nyumbani na kwa kuwa mtaji pekee niliokuwa nao ni wa kununua mashine ya kuranda mbao, nikaamua nilipie ada wanangu maisha yaendelee.

Hapa hapa nchini, wakati mimi mzawa nadaiwa kodi kabla ya kuanza biashara, akija anayeitwa mwekezaji anapewa kitu kinaitwa msahama wa kodi (tax holiday) kwa miaka mitano. Huyu, anapewa na cheti cha ubora benki zinamkopesha. Mimi nikifanya ubishi nikasema nifungue biashara yangu bila leseni, watatumwa mgambo wa jiji, si tu watakusanya bidhaa ninazouza pekee, bali nitafikishwa na mahakamani kwa kosa la kufanya biashara bila leseni.

Sitanii, nimegusa kwa uchache hospitalini, mahakamani, nenda polisi kama una kesi ndipo utajua hata karatasi ya kuandikia maelezo inabidi ukainunue. Kwenye daladala sisi malofa tunapanda kupitia madirishani, wakubwa wanaotafuna nchi yetu wanasiliba magari yao kwa makaratasi ya giza (tinted) maana wanajua sehemu ya haramu ndani ya fedha walizonazo. Inauma sana. Haya ni machache kati ya mengi yanayowafanya watu watake mabadiliko.

Sasa nirejee katika mada ya msingi. Kuna hofu kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaweza kumtangaza mgombea ambaye hakushinda, kwa maana ya mtu mwenye kura chache. Jamii pia imeaminishwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema Tume ikiishamtangaza mtu kuwa ndiye ameshinda urais basi hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kuhoji ushindi huo.

Nikilitazama suala hili, nasema lina ukweli nusu. Kwanza ifahamike kuwa Mahakama ni Muhimili wa dola uliopo kwa ajili ya kuhakikisha sheria zinatafsiriwa inavyostahili. Mtu, chombo au taasisi yoyote ikiwamo NEC ikitafsiri vibaya sheria, ni jukumu la Mahakama kuitafsiri inavyostahili kutokana na kitu kinachoitwa Mamlaka ya Asili ya Mahakama (Court Inherent Powers).

Eneo hili la kutangaza matokeo linatawaliwa na Ibara ya 41. Katika Ibara hii Ibara Ndogo ya 6 na 7 zinasema: “(6) Mgombea yeyote wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.

“(7) Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Wanaotafsiri Ibara hii kwa masilahi yao, wanaegemea kwenye Ibara ndogo ya 7. Wanachosahau ni kuwa Katiba ibara zake zinasomwa kwa kutegemeana kama ilivyo Biblia Takatifu. Ibara ya Ndogo ya 7 inapata uhalali wake kutoka Ibara Ndogo ya 6. Ibara ndogo ya 6 inasema ni lazima huyu atakayetangazwa awe “amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.”

Huyu aliyepata kura nyingi kuliko mgombea mwingine yeyote ndiye ana kinga inayotolewa na Ibara ya 41 (7) inayozuia kuhoji ushindi wake. Ikitokea NEC ikamtangaza mwenye kura chache kuliko baadhi ya wagombea au mgombea yeyote, Mahakama itaitisha (invoke) Kanuni ya Mamlaka ya Asili kutekeleza wajibu wake wa kulinda sheria isitafsiriwe au kutekelezwa kinyume na uhalisia.

Kwa mantiki hiyo, iwe ni chama tawala au chama vya upinzani, kazi waliyonayo ni kuhakikisha mawakala wao hawadanganyiki. Kifungu cha 2.3.1(c) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 kinawaruhusu mawakala wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kusindikiza masanduku ya kura hadi kufikisha mahali pa kujumulishia kura, kwa kuzingatia maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekwishatoa maelekezo kura zihesabiwe kwenye vituo na matokeo kubandikwa. Baada ya mawakala kutia saini idadi ya kura alizopata mgombea au chama wanachokiwakilisha na kupewa nakala, wanapaswa wasikubali masanduku kuondoka kituoni bila wao kuyasindikiza kwenda mahala kura zinapojumlishiwa.

Sitanii, hapa nieleweke. Kwenye vituo wanatangaza matokoe ya kituo na kwa Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Halmashauri) masanduku ya kura yanapelekwa pamoja na fomu za matokeo yaliyopatikana kwenye kituo kwa nia ya kuyajumulisha na vituo vingine vya kwenye kata moja hadi nyingine na kutoa jumla kuu kwa madiwani, wabunge na rais.

Wakizubaa hapo ndipo nafasi pekee ya mchezo kuchezwa. Mawakala wasiposindikiza masanduku ya kura, kuna wataalam wa miandiko. Saini zitaghushiwa na kwa joto la kupokwa ushindi, hadi kubaini kuwa saini si yenyewe na ukasikilizwa huku joto la uchaguzi likizidi kupanda itakuwa ndoto za alinacha.

Lakini kama mawakala watakuwa wamesindikiza masanduku ya kura, zikigushiwa saini kwenye fomu matokeo yakatofautiana na nakala walizonazo kwa kuwa masanduku ya kura yanakuwa bado yako mbele yao, wanayo haki ya kutaka zihesabiwe upya na hilo kisheria linaruhusiwa.

Nafasi inazidi kuwa finyu. Kuna hili la wafuasi kupiga kura wakaenda nyumbani. Huko uswahilini wanasema mkulima wa mahindi akiwasusia ngedere mahindi, anaweza kuvuna mabua. Nasema kama tulivyokwishakubaliana, busara inanituma kuwa wafuasi wawe wafuasi wa CCM, wawe wafuasi wa CHADEMA na Ukawa wanapaswa kukaa umbali wa mita 100 kama tulivyowaelekeza miaka yote.

Kitendo cha kubadili ghafla mawazo kuwa wapige kura waende nyumbani, mtawatia wasiwasi bure. Watajua kuna jambo baya mnataka kufanya. Pia, kwa nini muwaze kuwa wanajipanga kufanya fujo, badala ya kuwaza kuwa wansubiri matokeo ya ushindi kwa mgombea wao washangilie? Kwa nini mnakuwa na mwazo hasi? Hivi wakishinda wasubiri kutangaziwa redioni au kufuatwa majumbani kuja kusherehekea ushindi? Uchaguzi una raha yake mshindi anapotangazwa ukiwapo jamani, mwee!

Sitanii, liwe lolote liwalo, amani na iwe kipaumbele kwetu. Tusipigane, tusitukanane, tusibezane na kila upande uwe tayari kupokea matokeo. Na nakuhakikishia mpendwa msomaji, matokeo ya mwaka huu si tu yatashangaza wengi, hao wenye kutarajia vya kunyonga, vya kuchinja sijajua itakuwaje kwao. Tujiandae kisaikolojia. Mungu dumisha amani yetu. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri