Leo naandika makala hii nikiwa mkoani Tanga. Naandika makala hii zikiwa zimesalia wiki tatu kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25. Nimepata fursa ya kusafiri maeneo mbalimbali ya nchi hii. Nimezungumza na watu mbalimbali. Nimesikiliza ahadi za wagombea urais Edward Lowassa na Dk. John Pombe Magufuli, nimewasilikiza wananchi. Kimsingi kwa wale wagombea wengine sita uchaguzi kwao umekwisha.

Ni jambo jema kuwa hakuna harusi isiyo na wapambaji, ambao huonekana mno kabla ya maharusi kuingia ukumbini, na baada ya maharusi kuingia kazi ya wapambaji hukoma, bali husubiriwa kuanua majamvi baada ya harusi. Inawezekana nisikumbuke kuwashukuru mbele ya safari. 

Nachukua fursa hii mapema kuwashukuru wagombea hawa ambao hata sidhani kama nitawatendea haki kuwataja majina yao. Niseme tu kwa ujumla kuwa asanteni kwa kushiriki katika demokrasia.

Sitanii, ukiacha hawa wagombea waliojitokeza pengine kutangaza sura au kuuza majina yao ‘wafikiriwe’ mbele ya safari, naamini uchaguzi pia unaelekea ukingoni kwa wagombea wawili wanaochuana vikali. Niseme wazi na mapema kuwa wapigakura walio wengi hadi hivi sasa ninavyoandika makala hii, wamekwishafahamu ni nani rais ajaye, kinachosubiriwa ni tangazo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Ukipita katika mikoa mbalimbali kwenye maeneo ya starehe, vijiwe vya wazee, vijana, wanawake na watoto, basi unabaini kuwa kuna mwamko wa pekee. Ni kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza mshindi, hivyo mimi hapa leo sitatumbukia kwenye mtego wa kutangaza mshindi, lakini nakubaliana na mawazo ya rafiki yangu mmoja.

Nikiwa mjini Masaka wiki moja iliyopita, rafiki yangu aliniambia nasikia huko Tanzania mnajiandaa kufanya uchaguzi hivi karibuni, nikamwambia ndiyo. Akasema rais wenu ajaye ni nani? Nikamwambia nitamjuaje kabla hatujapiga kura, akasema wewe kama mwandishi hupiti kwa watu ukasikia wanamtaja nani watampigia kura? Nikamwambia si kwa watu tu, zinaendeshwa hata kura za maoni, ila matokeo yanatuchanganya.

Mwandishi huyo anayefuatilia kwa karibu siasa za Tanzania akaniambia, wala usipoteze muda. Akasema kura za maoni kama tatu zilizotangazwa na kumpa ushindi mmoja wa wagombea wanaochuana vikali, si za kutilia maanani. Akasema walioziendesha huenda wana mafunzo kutoka nchini China. Akasema matokeo hayo yametangaza kumfurahisha mfalme (iwe ni upinzani au chama tawala).

Mtu huyu akaniambia, yapo makundi yaliyoendesha utafiti yakatangaza matokeo halisi, lakini kwa bahati mbaya yakapuuzwa na hayo matokeo yaliyobezwa, huyo ndiye atakayeibuka mshindi. Kauli hii sasa ikanichanganya. Nikakumbuka hapa kwetu kura za maoni zilizompa ushindi Lowassa zimepuuzwa, na kura za maoni zilizompa ushindi Magufuli zimepuuzwa. Nikajiuliza sasa ni nani? Nikakumbuka kauli yake, ya kuwa wapigakura wanamtaja nani? Msomaji toa jibu mwenyewe.

Sitanii, mjadala huu umenikumbusha mazungumzo niliyopata kufanya na marafiki zangu watatu tukiwa nchini Afrika Kusini miaka miwili iliyopita. Tulianza kuzungumza masuala ya uchaguzi. Rafiki yangu mmoja kutoka Botswana, akatamba. Akasema wao wamepiga hatua. Akasema matokeo ya uchaguzi nchini mwao hufahamika ndani ya siku moja tangu kura zipigwe.

Tulikuwa na Mmarekani katika mafunzo hayo. Yeye akamshangaa huyu rafiki yetu kutoka Botswana. Akamwambia mbona mnatumia muda mwingi kiasi hicho? Akasema wao matokeo ya uchaguzi kutokana na kukua kwa teknolojia huyafahamu ndani ya muda wa saa tatu tu baada ya kumaliza kupiga kura na vituo kufungwa rasmi.

Pembeni tulikuwa naye kijana kutoka Zimbabwe. Kijana huyu alicheka sana. Akasema nchi zote hizo hazijaendelea. Akasema kwao Zimbabwe matokeo ya uchaguzi hufahamika mwaka mmoja kabla ya kufanya uchaguzi. Nikawauliza uchaguzi huo wote unakuwa huru na wa haki, wote wakanijibu kuwa tena bila wizi wa kura.

Sitanii, hapa kwetu tunajiandaa kuingia kwenye uchaguzi. Sheria inataka matokeo yatangazwe ndani ya siku saba tangu siku ya kupiga kura. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, amesema anataka kutangaza matokeo ndani ya siku tatu. Amekwenda mbali zaidi akasema kwa hofu ya wizi wa kura anataka matokeo yote yabandikwe kwenye mbao za vituo vya kupigia kura.

Ukiacha joto lililopo la nani ataibuka mshindi, wagombea tayari tumewasikia. Lowassa anasema anauchukia umaskini. Amejinadi kufuta ada katika elimu na kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu. Wiki iliyopia ametangaza vipaumbele 13 atakavyotekeleza ndai ya siku 100 za kwanza ikiwa atachaguliwa kuingia madarakani.

Ametaja vipaumbe hivyo kuwa ni:- 1. Uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi wa akinamama. 2. Umeme wa uhakika nchi nzima. 3. Kupunguza foleni jijini Dar es Salaam. 4. Kuondoa kero kwa wafanyabiashara wadogowadogo na waendesha bodaboda (wakiwamo mama ntilie). 5. Kumaliza tatizo la maji nchi nzima, na 6. Mfumo bora na rafiki wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Lakini pia 7. ametangaza kufuta ada na michango kwa wanafunzi. 8. Kupunguza kodi ya mshahara kwa wafanyakazi. 9. Kufuta kodi zote za mazao ya wakulima. 10. Mkakati wa kukuza michezo na sanaa. 11. Kuunda tume ya kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima. 12. Kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma za Serikali, na 13. Kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na walimu. Ameahidi kuimarisha Muungano na kuwapa wananchi Katiba mpya.

Lowassa anasema hayo ni nyongeza juu ya ajenda za msingi ambazo ni kufuta umasikini, elimu bure, ajira kwa vijana na kuimarisha utawala wa sheria ambapo wananchi watafaidi matunda ya rasilimali za nchi badala ya mfumo wa sasa ambapo utajiri wa nchi hii wanaufaidi wachache. Ametamba kuwa atawakata ‘kilimilimi’ wanaombeza kwa kutoa utumishi uliotukuka kwa Watanzania na kuonesha mfano kuwa kumbe kuleta maendeleo inawezekana Tanzania.

Sitanii, kwa upande wake Magufuli anajinadi kwenye kampeni kuwa atahakikisha anaipa nchi utumishi uliotukuka. Anasema atapambana na rushwa, mafisadi na wizi wa mali za umma. Anawaambia waliobinafsishiwa viwanda na kushindwa kuviendeleza kuwa wajue akishinda atawanyang’anya.

Magufuli ameahidi elimu ya chekechea hadi kidato cha nne kuwa bure, ajira, kuboresha maslahi ya wakulima kwa Serikali kuacha kuwakopa mazao, naye kama Lowassa akasema atahakikisha anawaondolea kodi za kero Wamachinga na Mamalishe, na ataangalia upya maslahi ya wasanii na wanamichezo.

  Ameahidi pia kuimarisha Muungano, umoja, amani na mshikamano, huku akiimarisha ulinzi wa Taifa, usalama na kuweka mipaka kati ya mihilimili ya dola. Madini anataka yanufaishe Watanzania, anataka kuboresha huduma ya maji, afya, elimu ya juu, kuboresha maslahi ya wafanyakazi, hasa walimu, kuweka matumizi sahihi ya gesi, kuunganisha mikoa yote kwa lami, kujenga reli ya kisasa, barabara na viwanja vya ndege.

  Pia ana mpango wa kuboresha maslahi ya watumishi wa maliasili, wafanyabiashara, waandishi wa habari na walemavu. 

Katika mikutano mbalimbali, Magufuli amewaasa Watanzania wasichague upinzani kwa maelezo kuwa nchi hii inaweza kuingia kwenye vurugu kama Libya. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameikosoa hoja hii wakisema kwa Libya, Kanali Muammar Gaddafi aliingia kwa kupindua, ila chama tawala hapa nchini kiliingia kwa kura, hivyo mfano huo hauna uhalisia.

  Mgombea Mwenza wa Magufuli, Samia Suluhu Hassan, ameahidi na ameungwa mkono na Magufuli kuwa atahakikisha serikali yao inatoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji.   

Ukimsikiliza Magufuli unaona bayana kuwa anazungumza lugha tofauti na lugha zilizozoeleka ndani ya CCM za ‘Kidumu Chama Tawala’, ‘CCM ina wenyewe…

Magufuli sasa amebadili utaratibu. Anapiga ‘push-up’ kwenye majukwaa ya kisiasa, anaruka kutoka kwenye malori na anapitia kwenye tundu la kuhutubia na kuruka nje ya gari kuwahi kuhutubia wapigakura. Akiwa kwenye mikutano ya hadhara anarukaruka juu kuthibitisha kuwa ni mwenye siha njema.

Kwa kauli, mwonekano na kaliba ya Magufuli, wapo wanaosema anaweza kuiletea maendeleo Tanzania. Katika mijadala ninayokutana nayo baadhi wanasema Magufuli akishinda uchaguzi ataiondoa CCM katika chumba cha wagonjwa mahututi. Wanasema ikiwa hataminywa na mfumo, anaweza kuijenga Tanzania ya viwanda na kubadili sura ya nchi.

Sitanii, wakati hao wakiwaza hivyo yapo mambo yanayoifanya safari ya Magufuli kwenda Ikulu kuwa sawa na kupanda Mlima Kilimanjaro kwa maelezo ya wachambuzi. Kwamba hoja iliyotolewa na wapinzani kuwa pamoja na uzuri wa Magufuli hawezi kubadili mfumo wa CCM, inaonekana kupenya kwenye masikio ya wapigakura.

Kuna dalili kwamba kuna wimbi katika uchaguzi wa mwaka huu. Wimbi la mabadiliko. Magufuli anataja mabadiliko, Lowassa anataja mabadiliko. Wapigakura wanataka mabadiliko kwa maendeleo. Wanamtaja Lowassa kama mzee wa ‘Maamuzi Magumu’. Ukiacha historia yake ya utendaji, wanasema hata ile kuamua kutoka CCM kwenda upinzani ni ishara kuwa huyu si mwoga. Si mwanasiasa wa kutishiwa nyau.

  Ukiacha hilo wimbi la mabadiliko, ambalo sheikh mmoja hapa Tanga ameniambia anachokishuhudia katika uchaguzi wa mwaka huu kwa umri wake wa miaka 65 hajapata kukiona, zamu hii karibu asilimia 60 ya wapigakura ni wale wanaopiga kura kwa mara ya kwanza. Hawa, kama baba yake, hawafanyi kazi serikalini au ndani ya chama tawala, wanaisikia CCM, hawaijui.

Sitanii, kama ilivyotokea hivi karibuni, Serikali ikabadili utaratibu wa kufanya mitihani ya darasa la saba na kuwa ya kuchagua yote hadi hesabu, hatua ambayo imewafanya hadi baadhi ya vijana wasiojua kusoma au kuandika kushinda darasa la saba, hilo likitokea kwenye sanduku la kura CCM isishangae. Ninachosema hapa ni kila mgombea, kila chama kijiandae kisaikolojia. Lolote laweza kutokea. Tujiandae kwa mambo mawili – kupiga kura na kulinda amani yetu. Mungu ibariki Tanzania.

3003 Total Views 4 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!