Biashara ya kusafirisha watu kwa njia ya pikipiki, maarufu kama bodaboda, imeleta neema na majanga sawia hapa nchini.

 Biashara hiyo inaonekana kuwaneemesha wale wanaoiendesha, hususan vijana ambao wanazidi kuongezeka huku ajira kikiwa ni kitendawili kinachokosa mteguzi hata pale inapotolewa ahera kama mji kwa atakayekitegua.

Usafiri wa bodaboda, ukiangaliwa kwa jicho jepesi, unaonekana ulivyoleta neema mara mbili kwa maana ya wanaosafirishwa na wanaosafirisha.

Kwa wanaosafirishwa usafiri huo ni wa haraka kwa vile unaweza kumfikisha abiria anakotaka kwenda bila kusubiri abiria wengine wapatikane kama ilivyo kwa usafiri wa mabasi na aina nyingine za usafiri ambazo si rahisi kumsafirisha mtu mmoja ikiwa ni lazima chombo kijae kwanza ndipo kiondoke.

Kwa maana hiyo watu kwa sasa wana uhakika wa kusafiri kwa muda waliojipangia kwenda wanakokutaka na kufanya shughuli zao kisha kurudi walikotoka bila kukwamishwa na chochote.

Usafiri wa haraka uliozoeleka ni wa kutumia taxi ambao nauli yake sio rafiki kwa wananchi walio wengi, pia taxi zinashindwa kufika katika baadhi ya sehemu kulingana na mazingira ya sehemu nyingine kutotoa nafasi kwa magari hayo kuzifikia, wakati bodaboda zikijitahidi kuyafikia kwa wepesi.

Lakini wakati limejitokeza wazo la kuanzisha biashara hiyo ya usafiri wa bodaboda pia kulijitokeza vigingi vingi vilivyowekwa na vyombo vya serikali ikidaiwa kwamba usafiri huo haufai, kwamba pikipiki hazifai kukodishwa kama taxi. Zilitolewa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai ya kwamba chombo kisicho na matairi mawili nyuma hakipaswi kufanya biashara ya kukodishwa.

Lakini watetezi wa wazo hilo la kuanzisha biashara ya bodaboda tukiongozwa na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kagera kwa muda mrefu, Pius Ngeze,  tulijifunga kibwebwe tukitumia hoja za uhakika mpaka biashara hiyo ikahalalishwa.

Pamoja na mambo mengine tulisema kwamba kama pikipiki imetengenezwa kwa ajili ya usafiri ikiwa inaruhusiwa kubeba abiria, kwa nini ionekane tofauti linapokuja suala la kukodishwa? Ugumu wa jibu la swali hilo ndio ukawa mwanzo wa mamlaka husika kulegea na kutoa ruksa kwa biashara hiyo ya bodaboda.

Lakini kutokana na biashara hiyo kuruhusiwa shingo upande haukufanyika utaratibu maalumu wa kuiendesha, kinachoonekana mpaka sasa ni kama “potelea mbali watajijua wenyewe”!

Baada ya hapo vijana wengi waliokuwa hawana ajira wakaivamia biashara hiyo bila ukaguzi wowote, kijana anajifunza kuendesha pikipiki siku moja na kesho yake anakuwa dereva wa bodaboda, akikaguliwa hana leseni na wala hajui sheria hata moja ya barabarani!

Matokeo yake ni ajali za kila dakika ambazo zimewageuza vijana wengi viwete kwa kukatwa miguu, mikono na sehemu nyingine za viungo vyao achilia mbali vifo vingi vya kutisha vinavyosababishwa na uzembe huo.

 Nimesikitika sana baada ya kufika sehemu moja Bukoba Vijijini ambayo ina bodaboda zisizopungua 35 na kugundua kuwa hakuna kijana yeyote kati ya hao wanaoendesha bodaboda anayejua leseni ni kitu gani!

 Wao walichojipangilia ni umoja, akitokea mmoja wao akasababisha ajali wanamuandama yule aliyehusika kwenye ajali, iwe ni pikipiki, gari au baiskeli, wanajichukulia sheria mikononi kwa kumuadhibu kwa kutumia wingi wao  bila kujali kwamba mwenzao ndiye mwenye makosa.

 Siku chache zilizopita katika maeneo ya Rwamishenye kwenye viunga vya manispaa ya Bukoba, dereva mmoja wa bodaboda alichomoka kama ilivyo kawaida yao, na kujichomeka kwenye gari dogo na kusagika mguu.

 Aliyekuwa anaendesha gari hilo ikabidi ajaribu kukimbia kwa usalama wake baada ya kuona idadi ya vijana wa bodaboda inaongezeka na kila mmoja wao akidai mtu huyo amemgonga mwenzao. Vijana hao wakalikimbiza gari hilo na kulizuia, kisha wakamtoa dereva na kuanza kumpiga vibaya na baadaye  wakamsukumiza chini ya gari ili waliwashe moto na kumuunguza.

 Mungu bariki alikuwepo askari akamnusuru mtu huyo na kumpeleka kituo cha polisi. Lakini gari liliharibiwa vibaya sana kwa kuvunjwa vioo vyote pamoja na kuiba kila kilichokuwemo kwenye gari hilo ikiwa ni pamoja na simu na pesa zote za jamaa huyo.

 Majanga ninayoyaeleza katika biashara hiyo ya bodaboda ni kama hayo, pamoja na kwamba ajali nyingi zinazohusu bodaboda zinasababishwa na watu wenyewe wa bodaboda lakini wao wamejiwekea utabatiri wa kuwahukumu wale wengine wanaohusika kwenye ajali hizo bila kujali kuwa wenzao ndio wanaozisababisha.

 Majanga ya bodaboda yako hivi, wao wanasababisha ajali za barabarani kutokana na kutozijua sheria za barabarani pamoja na kutohalalishwa kuendesha vyombo vya moto, kwa maana ya kutokuwa na leseni, lakini wao ndio wanaogeuka watu wa kuhukumu mahali inapotokea ajali inayomhusu mwenzao!

Haiwezekani wakawakamata waliohusika kwenye ajali na kuwapeleka kunakohusika sababu wanajua wazi kuwa mwenzao ndiye atakayekuwa kwenye hatia. Hivyo hukumu wanaitoa wao palepale hata kama mwenzao atakuwa kapoteza viungo au maisha.

Kitu ambacho serikali ingekifanya baada ya kuzidiwa hoja kwenye usafiri wa bodaboda kingekuwa ni kuwasajili waendesha biashara hiyo wote na kuwapangia maeneo wakiwa na sare pamoja na namba za kuwatambulisha. Kabla ya hapo wote wangetakiwa kuwa na leseni ambazo zingekuwa zinafanyiwa uhakiki wa mara kwa mara.

 Hiyo ingefaa kuonyesha kuwa serikali inayajali maisha ya watu wake ikiwa imewanusuru na majanga yaletwayo na biashara ya bodaboda. Ni kweli bodaboda zimekuwa na neema sanjali na baraa. Bila kuliangalia hilo kwa umakini tujue kwamba maisha ya wananchi wengi yamewekwa rehani.

1302 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!