Joe Beda Rupia

Kustaafu ni kama kifo. Ndiyo. Ukianza kazi siku ya kwanza tu, unaanza safari ya kustaafu. Hakika utastaafu na neno hili linaweza kuwa chanzo cha tatizo.

Sawa. Kwa wiki mbili zilizopita nimekuwa nikiandika tanzia; kwanza ya Jenerali Tumainiel Kiwelu, kisha ya Chrisant Mzindakaya.

Kabla ya kuanza hoja ya leo, kustaafu, niweke sawa kumbukumbu kama zilivyowekwa na wasomaji kadhaa wa safu hii.

Kwanza ni kwamba, Jenerali Kiwelu alirejea tena Sumbawanga wakati wa sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kushangiliwa sana na wananchi.

Awali nilisema hadi mauti yanamkuta, mwamba huyu hakuwahi kurejea Sumbawanga. Pili ni kwamba, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ilikuwa Kantalamba, si Bomani, maeneo ya Posta.

Sawa. Turejee kwenye ‘kustaafu’; kwa maana ya kumaliza muda wa mtu kuendelea kufanya kazi ama binafsi au ya kuajiriwa. 

Yaani kupumzika harakati za utafutaji wa nguvu kutokana na umri kuwa mkubwa. Ndiyo. Kustaafu ni kama kifo. Ukianza kazi lazima utastaafu tu.

Lakini siku zote wanaoanza kazi huwa ni vijana. Aghalabu, vijana huwa hawafikirii sana ‘kuzeeka’ kwa hiyo husahau kuwa siku moja kuna kustaafu. 

Ndipo swali la msingi linapojitokeza; ni lini mtu anapaswa kuanza kuwekeza kwa ajili ya kustaafu?

Jibu ni mapema iwezekanavyo. Yaani ikiwezekana siku unapoanza ajira mara moja anza kuwekeza hata kama ni kidogo kidogo kwa ajili ya kustaafu.

Ni vema wazazi tukawa tukiwakumbusha watoto wetu kuwa siku moja wataanza kufanya kazi iwe ya kujiajiri au ya kuajiriwa.

Kwamba watakapoanza kazi, wafahamu kwamba ipo siku watastaafu, hivyo waanze mara moja kujiandaa kwa maisha ya baada ya kazi.

Iwekwe wazi kuwa ajira si kazi za serikalini pekee. Kwamba wanaostaafu ni wafanyakazi wa maofisini tu. Hapana. Uvuvi, kilimo, ufugaji, biashara, uchimbaji wa madini vyote hivi ni ajira na umri (mkubwa) ukifika, anayejishughulisha na haya anapaswa kustaafu.

Tuwafahamishe kuhusu maeneo stahiki ya kuwekeza mbali ya shughuli zao za biashara au ajira. Wazifahamu kampuni maalumu za masuala ya uwekezaji kama UTT AMIS.

Nimekuwa nikiizungumzia sana kampuni hii na kwa hakika wasomaji kadhaa wamenitafuta na ninaamini kwa sasa nao ni wawekezaji. Ni furaha kubwa kwangu.

Kuwekeza fedha kwenye kampuni hii kuna faida kubwa, hasa iwapo fedha hiyo itadumu kwa miaka mingi kwa ‘mameneja’ hao wa fedha za wawekezaji wanaotambuliwa na serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Uwekezaji huu hufahamika kama ‘uwekezaji wa pamoja’ na kwa hakika ni muhimu sana kwa wastaafu watarajiwa, hasa vijana.

Kwa kijana, muda ni silaha. Kijana anapaswa kuzingatia au kufanya mambo kama; kutathmini umri wake, kutathmini muda ambao angependa kustaafu; kutazama vyanzo vya kipato; gharama na mambo kadha wa kadha.

Kijana anapaswa kuchanganua ni kiasi gani cha fedha anaweza kukiweka kando kwa ajili ya kustaafu pamoja na kushiriki katika maisha ya ‘kula ujana’.

Mipango mingine ni kujikadiria miaka unayoweza kuishi baada ya kustaafu huku ukimshirikisha Mungu; pia ni muhimu kuchagua au kupafahamu mahali ambapo ungependa kuishi baada ya kustaafu na namna sahihi ya kuhudumia familia yako na wewe mwenyewe kiafya.

Wataalamu wanaweka wazi kuwa muda na maandalizi ya kina ndilo jawabu sahihi la kustaafu vizuri.

Hata hivyo, si rahisi kuwa sahihi kwa asilimia 100 kwa kuwa mipango mizuri kadhaa huingiliwa na hali halisi ya maisha, mwishowe unastaafu ukiwa na huzuni. 

Yaani badala ya kufurahia kustaafu salama, unastaafu kwa masikitiko.

Sawa, kwetu ambao bado tupo kazini, ni wazi kuwa tuna muda wa kujiandaa na kuiandaa tabasamu ya baadaye. Tuanze kuwekeza sasa. 

Ni hatari kuanza kuwekeza ukiwa umechelewa, kwani ni sawa na kupishana na faida za uwekezaji hasa zile faida jumuishi zinazopatikana katika uwekezaji wa kisasa kama kwenye mifuko ya UTT AMIS.

Mfano mzuri wa upatikanaji wa faida jumuishi ni pale unapowekeza Sh milioni 5 kama kiwango cha awali, kisha kila mwezi unawekeza Sh 200,000.

Ndani ya miaka 10 ya ajira yako utakuwa umewekeza Sh milioni 29. Iwapo riba ya fedha hizo ni asilimia 1.2 kwa mwezi, basi kwa miaka 10 utakuwa na Sh milioni 74!

Ni kama maajabu, lakini ndivyo ilivyo na watu wananufaika. Hata hivi sasa unaposoma makala hii, wapo.

Busara inaonyesha wazi kuwa wakati wa kustaafu si wakati muafaka wa kujenga nyumba; bali ni wakati wa kuziba nyufa zilizopo.

Kwa ambao hatukuwahi kuwa na nyumba wakati wa ajira, ushauri ni kwamba, baada ya ukomo wa ajira nunua nyumba ndogo tu utakayomudu kuiendesha. 

Mara nyingi ukubwa wa familia hupungua mtu anapostaafu. Watoto huwa wanajitegemea na si ajabu ukajikuta Bwana amempenda zaidi hata mwenza wako!

Sasa ukibaki na jumba kuuuubwa, linakuwa ni alama ya upweke badala ya ufahari huku kuliendesha kukila hata fedha chache ambazo zingetumika kwa masuala muhimu uzeeni, kama afya. 

Akiba wakati ukiwa kazini ni hazina baada ya kustaafu. Madeni ni tafsiri ya uchache wa akiba au uwekezaji kwa ajili ya kustaafu. Ni vema kujichunga sana; tusiingie au kujiingiza kwenye madeni makubwa na kujitwisha mzigo mzito uzeeni.

Bajeti. Hivi leo ukiulizwa ulitumia shilingi ngapi mwaka jana, unaweza kutoa jibu sahihi? Mwezi uliopita je? Wiki ijayo umepanga kutumia kiasi gani cha fedha?

Ukiniuliza mimi sina jibu. Kwa kweli sijui! Semina nyingi za UTT AMIS nilizowahi kuhudhuria huwa tunashauriwa kujua matumizi yetu ya chakula, usafiri na mambo yote muhimu na hata yasiyo muhimu. 

“Tumia kidogo na weka zaidi kwa ajili ya furaha ya baadaye,” wanasema wataalamu na kuongeza:

“Tawanya uwekezaji wako, chagua kwenye unafuu wa kodi, mfano mifuko ya UTT AMIS. Ukiwekeza kwenye mfuko mmoja unakuwa kama umewekeza sehemu nyingi.”

Hivi mwenza wako, kwa bahati mbaya akitangulia mbele ya haki mapema wakati ni yeye ndiye aliyekuwa kichwa cha familia, utafanyaje?

Sikiliza. Ili kukwepa mshtuko kama huo ni muhimu ulitambue hilo na uwe umejiandaa mapema kwa sababu mmoja akitangulia mambo mengi hubadilika.

Kipato, kodi, maisha yenyewe vyote huchukua mwelekeo mwingine.

Wenye akiba kwenye mifuko kama NSSF au PSSSF, huzua mjadala wa mara kwa mara kutaka wapewe fedha zao mara wanapozihitaji, eti kwa sababu ni zao! 

Lakini washauri wanaelekeza kuwa ni vizuri kudai au kuchukua kiinua mgongo wakati wa kustaafu utakapofika. 

Hii ni kwa sababu wengi hatuna mipango mizuri ya fedha, na pengine si wafanyabiashara au wawekezaji stadi. Kwa mantiki hii, ni vizuri kusubiri.

Kustaafu si ukomo wa kufanya kazi, bali ni muda wa kuanza jambo jipya ili kupata uzoefu tofauti. 

Zamani ilikuwa ukikoma kufanya kazi ukiwa na miaka 50, ukifikisha miaka 60 ni bahati. Lakini sasa baada ya kuboreshwa huduma za afya, elimu na uelewa wa ulaji mzuri pamoja na mazoezi, wengi wanaishi hadi miaka 90!

Ushauri wangu hapa ni kuchapa kazi na neno ‘kustaafu’ lisikutishe na kuwa tatizo kwako. Ukiwekeza vema, utaishi kwa furaha.

469 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!