TABORA

Na Benny Kingson

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Magharibi imemkamata mtumishi wa Kituo cha Afya wilayani Kaliua, Maila Mdemi, kwa tuhuma ya wizi wa vitendanishi.

Maila ni mmiliki wa Duka la Dawa la Nansimo ambalo limekutwa likiuza vitendanishi vya serikali vya kupimia maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi, Dk. Christopher Migoha, anasema Maila amenaswa na wakaguzi wa TMDA wanaofanya ukaguzi wa kushtukiza.

“Tumembana aeleze alikovitoa, wapi hakuwa na jibu la moja kwa moja. Maila anafanya kazi serikalini na vifaa hivyo ni mali ya serikali,” anasema.

Dk. Migoha anasema TMDA imekuwa ikiwaonya mara kwa mara wauzaji wa maduka ya dawa na wamiliki kutojihusisha na hujuma, hasa wizi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Anaahidi kuwa wote wanaokaidi onyo hilo watanaswa kwa kuwa mamlaka ipo makini muda wote na itaendelea kufanya msako mara kwa mara.

Maila na wengine watakaokamatwa watafikishwa mahakamani taratibu zitapokamilika.

By Jamhuri