MBINGA

Na Mwandishi Wetu

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini (DKU), Dk. George Fihavango, pamoja na ujumbe wake wamefukuzwa na kukataliwa kuingia nyumbani kwa mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Leonard Myalle; JAMHURI limeshuhudia.

Siku ya tukio, askofu huyo na ujumbe wake walifika nyumbani kwa mzee Myalle (74) kwa ajili ya kumfariji kutokana na madhira aliyokumbana nayo kwa takriban miaka tisa mfululizo, hata hivyo, tukio hilo limemalizika kwa tafrani ya aina yake.

Akizungumza na JAMHURI baada ya tukio hilo, mzee Myalle anasema: 

“Sikumkasirikia askofu kwa kuja kunifariji, la hasha! Hiyo ni haki yake. Kilichosababisha nimtimue na sadaka yake ni uongo walioutumia yeye na ujumbe wake kupitia kazi ya Mungu. Huu ni mwendelezo wa maovu yaliyotangulia.” 

Mwaka jana gazeti hili liliripoti taarifa mfululizo kuhusu kisa cha mzee huyo mwenye miaka 74 kubambikiwa kesi ya mauaji na kukaa mahabusu kwa miaka 11 huku mtu anayedaiwa kuuawa akiwa ni mzima wa afya.

Waliohusika na kisa hicho ni wazee wa kanisa huku Fihavango akiwa msaidizi wa askofu, Myalle akidaiwa kumuua Mchungaji Leonard Kambo mwaka 2011. 

Baadaye, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ilimfutia kesi na mahakama kumuachia huru; lakini sasa yeye na familia yake wamezuiwa kusali katika usharika huo.

Msafara wa Askofu Fihavango kwenda nyumbani kwa mzee huyo uliongozwa na Mkuu wa Jimbo na Mchungaji wa Usharika wa KKKT Mbinga, Malaki Mwilongo, Katibu Mkuu KKKT DKU Njombe, Grayson Chilongoji, Mchungaji Johnson Gudaga na Gideon Mpilimi.

Sadaka ya faraja kwa mzee huyo iliyopelekwa na askofu na ujumbe wake na kukataliwa, inatambulika kama ‘kamwene’ na ilikuwa ni Sh 100,000, ngano na viazi mviringo.

Mzee Myalle anasema asubuhi ya siku ya tukio alipokea simu kutoka kwa Mpilime akisema siku moja atakwenda kuisalimu familia yake, lakini dakika chache baadaye, Mpilime akiongozana na askofu wakafika nyumbani hapo.

“Kama walikuwa na nia nzuri, kwa nini waseme uongo?” anahoji Myalle.

Wanawake wawili majirani, Filemona Ngalupela na Elenia Mhoka, waliitwa kuwa mashuhuda wa tukio hilo baada ya balozi wa Mtaa wa Hyera kutopatikana.

JAMHURI limeshuhudia Mama Filemona akimhoji askofu sababu ya kwenda kimyakimya kwa mzee huyo, akidai kuwa anakwenda kumfariji.

“Alipobambikiziwa kesi ulikuwa Msaidizi wa Askofu na ulilijua suala hili, kwa nini haukuja kumsaidia? 

“Kama ni kwa kuwa haukuwa na nguvu (mamlaka), hata ulipopata uaskofu haukuja. Leo umekuja kimyakimya, umebeba nini?” anasema mama huyo.

Fihavango alikuwa msaidizi wa Askofu Isaya Mengele ambaye kwa sasa amestaafu.

Elenia naye amemshambulia Askofu Fihavango akimwambia: “Mnatumia vibaya sadaka za Wakristo maskini wanaomtolea Mungu. Hakika zitawagharimu.

“Dhambi hii (kumbambikia kesi mzee Myalle) mliifanyia madhabahuni, msipoitubu madhabahuni hatapona mtu.”

Mwandishi wetu amezungumza na Askofu Fihavango, na anasema kwa kifupi: “Kuna kitu nimejifunza katika tukio lile. Sikujua kama tatizo ni kubwa kiasi hiki. Hakika hekima inahitajika sana.”

Ingawa mazungumzo hayo yaliyotawaliwa na vilio kutoka kwa akina mama majirani yalianza bila maombi, kabla ya kuondoka nyumbani hapo askofu aliyafunga kwa maombi.

Mmoja wa wainjilisti aliyeomba kutotajwa gazetini, anasema wote walioandaa njama na kumbambikia kesi ya uongo ya mauaji mzee Myalle, Mungu anawafuatilia.

“Ajali na madhira ya kila aina yanawaandama wahusika wote. Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kusini hadi maaskofu walionyamazia suala hili.

“Wafuatilie maisha yao kwa sasa. Ni majanga matupu. Si uchawi, ni majibu ya Mungu na tusipotubu Kanisa litaumia,” anasema.

854 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!