Viongozi wa kijiji wajichotea fedha ‘kiulaini’

 

Vigogo watatu wa Kijiji cha Mawemeru kilichopo katika Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita, mkoani hapa wanatuhumiwa kujigeuza “Miungu-watu” kwa kutafuna fedha za wanakijiji Sh 50 milioni.

Kwa nafasi hiyo, vigogo hao wanadaiwa kukigeuza kijiji hicho “shamba la bibi” huku wananchi wanaojitokeza kuhoji taarifa ya mapato na matumizi wakitishwa na wengine wakiishia kuswekwa ndani.

Vigogo waliokumbwa na tuhuma hizo ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Agness Matibu, Mwenyekiti wa Kijiji, Mussa Maduhu, pamoja na Mchumi, Philipo Kamuye, ambao, kwa kushirikiana wanadaiwa kutafuna kiasi hicho cha fedha.

Fedha hizo, zaidi ya Sh 50 milioni zinatokana na vyanzo vya ndani vya mapato yatokanayo na kijiji. Kadhalika sehemu ya fedha hizo hutokana na mapato yatokanayo na wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi.

Vyanzo vya gazeti hili vilidai kuwa vigogo hao kwa pamoja wameshirikiana kufisadi mapato ya kijiji na kwamba suala lolote linalohusu fedha zitokanazo na vyanzo hivyo, hakuna mwananchi anayeruhusiwa kuhoji na hawajawahi kusomewa taarifa za mapato na matumizi tangu mwaka 2011.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa vyanzo vya mapato ambavyo fedha zake zimetafunwa na vigogo hao ni pamoja na ushuru unaotokana na Myalo ya kuoshea unga unaodhaniwa kuwa na dhahabu; makarasha ya kusaga mchanga unaodhaniwa kuwa na dhahabu pamoja na miradi ya visima vya maji.

Vyanzo vingine vya mapato vinavyokiingizia fedha kijiji hicho kabla ya kuishia mifukoni mwa vigogo hao, ni asilimia itokanayo na mauzo ya vitu vya kijiji hicho kama viwanja, nyumba na mashamba. Kadhalika fedha nyingine zinatokana na ushuru unaolipwa na mwekezaji wa ndani ya kijiji hicho, Swalehe Juma, anayemiliki shule na stoo ya kutunzia baruti zinazotumika kulipulia miamba ya dhahabu.

Mbali na hilo, gazeti hili limebaini pia kuwa fedha za ushuru zinazotokana na wawekezaji wa ndani ya kijiji wanaomiliki kampuni za uchenjuaji wa marudio ya dhahabu, nazo hazijulikani zilipo.

Wamiliki wa kampuni hizozya uchenjuaji marudio ya dhahabu ambao wamekuwa wakilipa ushuru kijijini hapo ni pamoja na Evarist Paschal, Baraka E. Nyandu, Golden Hainga na Maduhu Mlola-mmiliki wa Mine Extech.

Pamoja na hilo, kuna ushuru unaotokana na migodi ya uchimbaji wa dhahabu ndani ya kijiji hicho inayomilikiwa na kampuni za Nsangano Gold Mine Project, Onesmo Gelewa Gold Mine Project, Yusuph Gold Mine Project, Hangwa Gold Mine Project, Mariatabu Gold Mine Project na Excel Abdallah Gold Mine Project.

Vyanzo vya mapato vitokanavyo na wawekezaji wa ndani kutoka nje ya nchi ni pamoja na Kampuni ya Cassiko inayochenjua marudio ya dhahabu, kampuni ya Kichina ya kuchimba madini ya dhahabu na kampuni ya Mussa inayochimba na kuchenjua dhahabu.

Uchunguzi yakinifu uliofanywa na gazeti hili umeweza kubaini hadi idadi ya vyanzo vya mapato vilivyo ndani ya Kijiji hicho cha Mawemeru, ambapo kwa upande wa Myalo ni 45 na Makarasha 67 na kufanya jumla kuu ya vyanzo hivyo kufikia 112 ambavyo vyote vinatozwa ushuru sawa.

Utaratibu uliowekwa na uongozi wa kijiji hicho ni kwa kila mradi kulipia Sh 10,000 kwa mwezi na pesa inayodaiwa kutafunwa kwa upande wa Myalo na Makarasha kuanzia 2011-2013 ni Sh 19,040,000 kabla ya miradi hiyo kurudishwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Machi mwaka jana.

Uchunguzi huo umebaini baada ya ushuru unaotokana na Myalo na Makarasha kuanza kukusanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kuanzia Aprili mwaka jana kiasi cha Sh 19,040,000 kilikusanywa ambapo kijiji kilipatiwa Sh 3,808,000 kama ruzuku ya mapato ya kijiji ambapo, hata hivyo, matumizi ya fedha hizo hayafahamiki.

Hata hivyo, ni Myalo na Makarasha pekee ndiyo yaliyorejeshwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita, huku vyanzo vingine vya mapato vitokanavyo na wawekezaji wa ndani bado ni mali ya kijiji hicho.

@@

 

MTAA WA KANGEME

Tangu mwaka 2010 hadi Julai mwaka huu, malundo matano ya marudio ya dhahabu yaliuzwa na kutoa tripu 1,028 za magari. Kila tripu moja ililipiwa kiasi cha Sh 10,000 kama ushuru wa kijiji hicho na kiasi cha Sh 10,280,000 kilichotokana na ushuru wa marundo hayo, kilikabidhiwa na wahusika akiwamo Mchumi wa Kijiji cha Mawemeru, Kamuye, lakini pesa hiyo inadaiwa kuyeyuka.

 

MTAA WA MGOMBANI

Tangu mwaka 2010 hadi Julai 2014 malundo ya marudio ya dhahabu yaliyobainika kuuzwa ni 12, kati ya malundo hayo, moja tu ndilo lilibainika kuwa na jumla ya tripu 50 ambako thamani yake ni Sh 500,000 ambazo zilikusanywa na Mchumi Kamuye kwa mgongo wa kijiji hicho.

 

KITONGOJI CHA ZIWANI

Tangu Juni Mosi 2011 hadi Oktoba 30, 2011 wanakijiji Kuluha Kahendele na Magdalena Mwidibo walikabidhi kwa Mchumi Kamuye kiasi cha Sh 560,000 kiasi kilichotokana na mradi wa maji uliopo katika Kitongoji cha Ziwani kijijini hapo, ambapo wao walikuwa wasimamizi wa mradi huo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Januari 2012 hadi Januari 2013, mradi huo wa maji ulikodiwa na Mlekwa Nassoro aliyeilipa Serikali ya Kijiji Sh 1,200,000 ambazo, hata hivyo, hazijulikani zilipo.

Februari mwaka jana hadi Januari 10, 2014; Yuda Thomas naye alikodi mradi huo wa maji kwa makubaliano ya Sh 1,000,000 pesa ambayo pia ilikabidhiwa kwa Mtendaji wa Kijiji hicho na mbele ya Mchumi Kamuye kabla ya kuyeyuka.

Julai 12 hadi 18, 2014 Christina Pastory akiwa msimamizi wa mradi huo wa maji kwa siku saba, aliweza kukusanya kiasi cha Sh 70,000 alizowasilisha kwa Mchumi Kamuye pia hazijulikani zilifanya kazi gani kwenye kijiji hicho.

Julai 19 hadi Agosti 7, 2014, mkazi mwingine Zawadi John akiwa msimamizi wa mradi huo wa maji wa kitongoji hicho cha Ziwani, kwa muda wa siku 15 alikusanya kiasi cha Sh 150,000 ambazo pia zilikabidhiwa kwa Mchumi Kamuye.

 

MCHUMI AWA MBOGO

JAMHURI ilipotaka kupata ufafanuzi wa tuhuma zake, Kamuye aligeuka mbogo kwa madai kuwa hana mamlaka ya kutoa maelezo yoyote yale kwa mtu yeyote isipokuwa ofisi ya mtendaji wake wa kijiji na si vinginevyo.

 

KITONGOJI CHA MAKANISA

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Agosti mosi, 2013 Kampuni ya Aurum Enterprises ilikabidhi kwa Serikali ya Kijiji cha Mawemeru mradi mkubwa wa maji ambapo kijiji kiliteuwa wasimamizi wa kukusanya mapato yatokanayo na mradi huo ambao ni Salum Dotto na Magdalena Mwidibo.

Imebainika wasimamizi hao kwa siku waliweza kukusanya  Sh 60,000 ambapo kwa hesabu za haraka haraka, kuanzia tarehe ambayo mradi huo ulikabidhiwa kwa kijiji hicho hadi Juni 30, 2014 kiasi cha Sh 19,800,000 zilikuwa zimekusanywa (kwa kipindi hicho cha miezi kumi na moja) kwa kila mwezi Sh 180,000 na kukabidhiwa kwa mtendaji wa kijiji hicho cha Mawemeru.

 

WASIMAMIZI WATOA YA MOYONI

Wasimamizi hao kwa nyakati tofauti walieleza kuwa katika kipindi chote walichopangwa kusimamia mradi huo wa maji, kiasi cha pesa kilichopatikana walikabidhi kwa Mtendaji wa Kijiji hicho, Agnes Matibu.

Elizabeth Daud alidai kuwa alianza kusimamia mapato ya kisima hicho kuanzia Julai 2-29, 2014 na katika siku hizo aliwasilisha kwa mtendaji huyo kiasi cha Sh 185,000. Mosi Yatabu alidai kusimamia kuanzia Julai 2 hadi Agosti 10, 2014 na kiasi cha Sh 160,000 alichokusanya alikabidhi kwa mtendaji wa kijiji Matibu.

Kwa mujibu wa wasimamizi hao, pesa zote tajwa zilizotokana na mradi huo wa maji, ambazo walikusanya na kuzikabidhi kwa mtendaji huyo wa kijiji, zimepokewa bila kukatiwa risti. Kwa upande wake, Christina Pastory alisema alianza kusimamia Agosti 4 hadi 22, 2014 na kukusanya Sh 179,000 ambazo alizikabidhi kwa mtendaji huyo na kupatiwa risti Na. 327403.

JAMHURI pia imebaini kuwa fedha Sh 3 milioni zilizokusanywa kama ushuru wa kijiji za mnara wa simu uliopo katika Kitongoji cha Makanisa pamoja na ile ya sungusungu Sh 305,000 hazijulikani zilipo na hakuna mkazi wa eneo hilo anayejua kijiji kinapata mapato kiasi gani ya asilimia ya mauzo ya mashamba, viwanja na nyumba.

 

MYALO, MAKARASHA MTAA WA KANGEME

Uchunguzi umebaini pia kuwa mbali na wawekezaji hao kulipa ushuru kutokana na shughuli wazifanyazo kijijini hapo, pia wamekuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za maendeleo ya Kijiji hicho. Mathalani mwaka 2010, wamiliki wa Myalo na Makarasha iliyopo Mtaa wa Kangeme, Kitongoji cha Ziwani, katika Kijiji hicho cha Mawemeru walichangia viti 10 vya plastiki kijijini hapo.

Mwanzoni mwa mwaka 2012 walitoa mifuko 21 ya saruji, fedha Sh 90,000 zilizokatiwa risti, lakini ilipofika Desemba, mwaka huo walitoa tena Sh 770,000 ambazo hazikukatiwa risiti na katika hali ya kushangaza, Katibu wa Mtaa huo, Gideon Shenda, aliyewakilisha kiasi hicho cha pesa alikamatwa kwa amri ya Mtendaji huyo wa Kijiji, Matibu, na kuwekwa ndani kwa kudai risiti ya fedha alizotoa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Nyarugusu, kabla ya kudhaminiwa na Emmanuel Mabina, Mwenyekiti wa Myalo na Makarasha.

Shenda akizungumza na JAMHURI kijijini hapo, alikiri kukamatwa kwa amri ya mtendaji huyo na kuwekwa mahabusu ya kituo kidogo cha polisi Nyarugusu. Alisaidiwa na mkuu wa kituo hicho ambaye alimtoa kwa dhamana.

Kesi hiyo ilihamishiwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Thobias Ikangala, aliyeamua kuimaliza kesi hiyo kwa kumuonya mtendaji huyo kutorudia kuweka ndani mwananchi anayehoji masuala ya msingi kama alivyofanya Shenda.

JAMHURI imebaini kuwa mwaka 2011 Katibu wa Kitongoji cha Makanisani, Amiri Abdallah, alichangia matofali 1,000 ya kuchoma yaliyokabidhiwa ofisi ya mtendaji huyo wa kijiji pamoja na fedha Sh 180,000 ambazo pia hazikukatiwa risiti.

Mbali ya kunyimwa risiti hakuchoka kuchangia shughuli za maendeleo ya kijiji hicho na ndani ya mwaka huo aliweza kuchangia madawati matano yenye thamani ya Sh 300,000 ambayo pia yalikabidhiwa ofisini kwa Matibu.

Uchunguzi umeweza kubaini Mwenyekiti wa Myalo na Makarasha katika Mtaa wa Migombani, Kitongoji cha Makanisa, Elisha Kinunuri, aliwahi kuchangishwa na mtendaji huyo, Sh 132,500. Hata hivyo, fedha hizo zililipwa kama ifuatavyo, Februari 25, 2011 (Sh 10,000 kwa risiti Na. 0161706); Aprili 20, 2011 (Sh 10,000 risiti Na. 115130); Julai 11, 2011 (Sh 20,000 risiti Na. 0161726); Desemba 29, 2011 (Sh 5,000 risiti Na. 0219422); Machi 30, 2012 (Sh 37,500 risiti Na. 0224614) na Januari 24, 2013 (Sh 20,000 risiti Na. 0268822).

 

ATHARI ZITOKANAZO NA UFISADI HUO

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mbali ya kijiji hicho kuwa na vyanzo vingi vya mapato ya ndani, akaunti ya kijiji hicho iliyofunguliwa mwaka 2011 katika Benki ya NMB Tawi la Geita, imefungwa. Chanzo chetu kutoka ndani ya benki hiyo kimesema sababu ya kufungwa kwa akaunti hiyo ni kuwa tangu ilipofunguliwa hakuna pesa iliyowahi kuingizwa wala kutolewa kwenye akaunti hiyo.

Taarifa zinasema kwamba akaunti ya kijiji hicho iko mifukoni mwa mtendaji, mchumi na mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho.

JAMHURI imebaini pia kuwa kijiji hakina eneo la soko, standi ya magari madogo, eneo la maziko na zahanati.

 

MTENDAJI WA KATA ANENA

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Ikangala, alipohojiwa na JAMHURI kuhusiana na tuhuma dhidi ya mtendaji wake, alidai; Tatizo katika kijiji hicho halipo kwa mtendaji bali Mwenyekiti wa Kijiji Maduhu ambaye ndiye chanzo cha upotevu wa pesa hizo.

“Tatizo hapa si mtendaji… mtu anayelalamikiwa sana ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji. Huyu ni tatizo sana hasa katika mambo yanayohusu fedha,” alisema Ikangala.

 

MWENYEKITI ARUKA VIUNZI

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mussa Maduhu alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa tuhuma zinazomkabili alidai; “Sihusiki na tuhuma zozote  za upotevu wa pesa za kijiji hicho kwa kuwa shughuli zote zinazohusu kijiji hicho hupitishwa na wajumbe wa halmashauri ya kijiji hicho, ambao hufanya kazi na mtendaji, na kama kuna suala linalohusu pesa aulizwe mtendaji na wajumbe wake.”

 

MTENDAJI AIKIMBIA JAMHURI

Mtendaji wa kijiji hicho, Matibu, alipopigiwa simu na JAMHURI kujibu tuhuma zinazomkabili, hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani, hakujibu.

 

MKURUGENZI HALMASHAURI NAYE AKIMBIA

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ally Kidwaka, alipopigiwa kupitia simu yake ya kiganjani iliita bila majibu. JAMHURI ina nakala ya barua iliyoandikwa na tume iliyoteuliwa na wananchi wa kijiji hicho, ya kubaini vyanzo vya mapato katika Kijiji cha Mawemeru kwenda kwa mkurugenzi huyo wa halmashauri, ikimtaka amwamuru mtendaji huyo kusoma taarifa za mapato na matumizi, barua iliyoandikwa Agosti 28, mwaka huu.

Barua hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Himbizi Madata, na Katibu wake, Gabriel Kinyunzi, na nakala zake kupelekwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, PCCB, Usalama wa Taifa, Katibu Tarafa Busanda, Diwani Nyarugusu, Weo Nyarugusu, OCS Nyarugusu na Mwenyekiti kijiji Mawemeru.

Katika barua hiyo, pamoja na mambo mengine, inamuomba mkurugenzi huyo kuingilia sakata hilo ili wananchi wasomewe taarifa za mapato na matumizi.

2743 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!