Amani Golugwa amendelea kudai kuwa wasomi wengi wameshangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kuwataka Watanzania wafuate uzazi wa mpango. Huo ni uzushi ambao CHADEMA ni kawaida yao.

Wanataka kutuaminisha kimakosa kuwa wasomi wote wa Tanzania wapo nyuma yao jambo ambalo halina ukweli wowote, wajinga watakuwa nyuma yao lakini hakuna wasomi wa kweli wasiona umuhimu wa uzazi wa mpango.


Tuseme tu kwamba Golugwa amepitwa na wakati na anaturudisha nyuma kwenye Tanzania ya kale ya vita ya kikabila ambapo kuzaana haraka haraka kulipewa umuhimu wa kipekee kwa kuwa kuliwezesha kabila kuongeza haraka haraka idadi ya askari wake. Siyo katika Tanzania ya leo ambayo haina vita ya kikabila.


Mwaka 1970 nilikuwa Afisa Habari wa Elimu wa kwanza wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) kilichoanzishwa kwa lengo la kuwaelemisha wananchi umuhimu wa kufuata uzazi wa mpango.


Kwa bahati mbaya UMATI ilianzishwa mwaka 1959 wakati mapambano ya kutafuta uhuru wa Tanganyika yaliyongozwa na TANU yakiwa yamepamba moto.


Hivyo baadhi ya wanasiasa waliona kwamba lengo la wazungu la kuwataka wananchi wazaane kwa mpango ilikuwa kupunguza idadi yao ili pakitokea vita kati yetu na wazungu watushinde kutokana na uchache wetu.


Kwa hiyo, katika kuokoa jahazi wazungu wa UMATI walinitoa Wizara ya Elimu nilikokuwa Afisa Vitabu wa kwanza mwananchi wakanitaka niwasaidie katika kuelimisha umuhimu wa uzazi wa mpango na kufungua matawi ya chama mikoani. Mpaka mwaka 1970 kulikuwa na tawi moja la Dar es Salaam.


Basi kwa kuanzia wazungu walihakikisha kuwa ninapata elimu ya kutosha kuhusu uzazi wa mpango ili nipate nafasi nzuri ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa suala hilo. Nikapelekwa kuchukua mafunzo huko Tehran (Iran), Accra (Ghana) na London (Uingereza).


Baada ya hapo nilichangia katika kuanzisha matawi ya UMATI katika mikoa ya Morogoro Iringa, Mbeya, Dodoma, Shinyanga, Tanga, Singida, Kilimnajaro, Mtwara na kadhalika.


Kitendo changu cha kuungana na wazungu katika kueneza Tanzania elimu ya uzazi wa mpango hakikuwa cha kusaliti Tanzania na watu wake, bali kilitokana na kutambua kwangu umuhimu na faida ya uzazi wa mpango kwa watu wetu.


Faida moja kubwa ya uzazi wa mpango ni kulinda na kuimarisha afya ya familia.


Sio siri, akina mama wanaozaa kila mwaka hupoteza damu nyingi na huchoka haraka Halafu baba anatafuta ‘nyumba ndogo’ baada ya ‘kumchakaza’ mke wake. Kwa upande wa baba mwenyewe akizingatia uzazi wa mpango anakuwa na nafasi nzuri ya kuipatia familia yake mahitaji muhimu.


Vinginevyo atakonda na afya yake itadhoofu kwa mawazo atakaposhindwa kuihudumia familia inayoongezeka watoto kila mwaka.


Na kwa upande wa watoto wanaopishana vizuri katika kuzaliwa (kama miaka miwili) wana nafasi ya kuhudumiwa vizuri zaidi na kuwa na afya nzuri kuliko familia inayozaliana kila mwaka.


By Jamhuri