BiasharaKimsingi fedha inapomjia mtu huwa inaambatana na nguvu fulani kubwa sana yenye chembe chembe za umiliki. Ni vema tukafahamu kuwa duniani kuna nguvu nyingi sana, lakini nguvu ya fedha pamoja na nguvu ya mamlaka zinatawala nguvu nyingine kwa sehemu kubwa.
Nguvu ya fedha na nguvu ya mamlaka zinaingiliana na kutegemeana ijapokuwa kuna sehemu zinaachana. Mathalani, mtu anaweza kuwa na mamlaka lakini asiwe na fedha lakini kila mwenye fedha ana mamlaka (hata kama siyo rasmi, na ndivyo mara nyingi inavyokuwa).
Niharakishe kusema kuwa nguvu ya fedha haitafutwi, isipokuwa humjia mtu ‘automatically’ kwa kadiri fedha zinapoongezeka. Nimekuwa nikichambua kitaalamu na kiuzoefu mbinu, mikakati na fursa za watu kuboresha uchumi wao (kupata fedha). Lakini nimeona ni busara tusaidiane kufunga vidhibiti mwendo dhidi ya nguvu inayoambatana na fedha.
Utakuwa ni msiba mkubwa (na nitahesabu kushindwa) ikiwa mikakati, fursa na mbinu ninazowapa watu kupata fedha, zikaishia kwa watu hao kupata fedha zitakazowaangamiza. Usipoifahamu nguvu ya fedha, na kama usipojihami kuimudu; lazima itakuangamiza!
Unapokuwa na fedha, kuna mambo makubwa mawili hutokea. Unakuwa na nguvu ya utiisho na unakuwa na mvuto mkubwa. Katika kipengele hiki ndipo hasa hutokea mamlaka. Kutokana na utiisho huo kila unachosema watu wanakitii, kila unakowatuma wanakwenda na kila unachokiagiza kina nafasi ya kufanyika. Kutokana na mambo hayo ni rahisi sana mjasiriamali kujisahau na kudhani kuwa kila muda upo sahihi.
Unapokuwa na fedha unakuwa kama umejipaka gundi iliyochanganyika na sumaku. Utajikuta unawavuta watu wengi wa kila aina kuja kwako. Wanaokuwa karibu nawe watakuganda na watanasa kwako muda wote. Kwa kuwa unawavuta watu wa kila aina kuja kwako; mara nyingi unawavuta maadui pia.
Kazi kubwa ya maadui hawa ambao mara nyingi huanza kama marafiki; ni kuhakikisha unachafuka, unabomoka ama unaanguka. Na kwa kadiri fedha inavyoongezeka ndivyo na maadui wanavyoongezeka pia. Hili lisikusumbue nitalichambua katika makala ya “Mjasiriamali na kigoda cha utajiri” katika wiki chache zijazo.
Nguvu ya fedha inapumbaza sana kwa sababu pia huambatana na manukato ya utakaso. Ukiwa na pesa unaonekana kuwa “handsome” hata kama sura na mwonekano wako hautofautiani na ngedere. Utakaso huu huwa unawaliza wajasiriamali wengi katika maisha yao. Kikawaida, manukato haya ya utakaso (ambayo yapo kwenye nguvu ya mvuto) huja katika umbo la mapenzi.
Kadiri fedha inavyoongezeka ndivyo unavyozidi kuvutia kimapenzi kwa wanawake wengi. Sote tu mashahidi kuwa wajasiriamali wengi husaliti ndoa zao kwa kujihusisha na vimada mara tu mambo yanapowanyookea kiuchumi.
Mwanzoni utakuta mjasiriamali anasota kutafuta fedha na mke wake wa ndoa lakini zikishawajia anaanza kuhangaika na vimada wa nje. Kiukweli wengi huwa hawajitumbukizi katika mtego huu kwa makusudi; isipokuwa inawatokea bila hata kujitambua. Tunajifunza hata kutoka kwa Mfalme Suleman, Daudi, Samson na wengine wengi katika Biblia.
Mara zote ukipata fedha kubwa kuliko maono (malengo) yako ni lazima itakusumbua. Hili unaweza kulipima hata mitaani kwetu. Kuna mtu anaweza kuwa na vilaki viwili tu lakini akasumbua mtaa mzima – anaweza kupita baa hadi baa akifanya kufuru. Na wakati huo huo jirani yake anaweza kuwa na milioni kumi lakini ametulia.
Tatizo lililopo hapo ni utofauti wa malengo na maono yao. Yule wa laki mbili huenda amebabatiza fedha hiyo pasipo kuwa na malengo nayo, lakini huyu mwenye milioni kumi huenda ana malengo ya kujenga nyumba kwa maana hiyo hakuna hela anayoweza kuchezea.
Maadamu tunaendelea kuzisaka fedha, nguvu na usumbufu unaoambatana na fedha hautakoma kutuandama, lakini mjasiriamali unatakiwa kuwa na mfumo sahihi wa kimaisha kupambana nazo. Na ili uweze kuhimili mikikimikiki ya nguvu ya fedha ni lazima uwe na malengo unayoyaheshimu na unayoweza kuyasimamia.
Kwenye malengo yako lazima utangulie kumuweka Mungu kwanza, ufuate maslahi ya kifamilia; ndipo Mungu na familia yako wakuunge mkono katika harakati za kiuchumi (ujasiriamali wako). Wale wajasiriamali wenye utamaduni wa kuwaficha wake zao mipango yao ninawatahadharisha kuwa nguvu ya fedha itawamaliza. Isipowapata kiafya itatafuna furaha yao, isipotafuna furaha yao itawapenyezea kuyeyuka kwa upendo katika familia.
Imani yangu kuhusu ustawi wa kiroho naamini kuwa inasaidia kukuweka kwenye mstari wa kimaadili wakati wote. Kwanza huwezi kupunguza upendo kwa mke wako wakati wote iwe fedha imeongezeka ama mmepita katika upungufu. Kutokana na upendo huo (unaowezeshwa na nguvu za kiroho) ni sawa na ngamia kupenya tundu la sindano kwa wewe kumsaliti mke wako ama kuitelekeza familia yako kwa sababu ya kuogelea kwa vimada.
Shida nyingine inayoletwa na fedha ni kiu ya kuendelea kuongeza fedha kadiri unapopata fedha. Jambo hili mara zote hupelekea mjasiriamali kushindwa kubalance mambo. Akili inapokuwa kwenye fedha wakati wote ni rahisi kusahau mambo ya msingi kabisa.
Ndiyo maana si ajabu kumkuta mjasiriamali akiwa bize na biashara zake kiasi kwamba anasahau kabisa kutenga hata muda wa kumwabudu Mungu walau mara moja kwa juma. Kwa kufanya hivi tayari mjasiriamali anakuwa amepuuza ujenzi wa roho yake.
Kwa kuwa bize kutafuta fedha muda mwingi wajasiriamali wengi huwa wanasahau kutenga muda wa kukaa na familia (mke, watoto) na kuwaonesha upendo wao. Jambo hili ni hatari sana kwa sababu mwisho wa siku familia haitaona umaana wa mafanikio yako kiuchumi.
Wapo wake wa wajasiriamali ambao huwa wanaomba maombi rasmi kabisa kwa Mungu; ili waume zao wasifanikiwe katika miradi na biashara fulani, kwa sababu biashara na miradi hiyo inawakosesha wasaa wa kufurahia mapenzi na upendo kutoka kwa waume zao. Sasa angalia, mjasiriamali uko bize unatafuta fedha, Mungu umemsahau na familia umeisahau.
Mungu anakuchukia na familia inakuchukia! Kama unahangaika na fedha ambazo zinaharibu uhusiano wako na Mungu na zinavuruga mapenzi na upendo katika familia yako, basi fedha hizo hazina maana. Na kiuhalisia nakuthibitishia kuwa hautafika popote na kama ukiwa na mafanikio katika eneo hilo la uchumi; hutaiona ladha kamili ya mafanikio.
Wajasiriamali tunastahili ushindi wa kiuchumi, kifamilia na kiroho.

 

By Jamhuri