‘Niliondolewa kijeshi’, Mugabe

Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amesema tukio la kuondolewa kwake
madarakani kwa kutumia nguvu za kijeshi, haina tofauti na mapinduzi ya kijeshi yanayoweza
kutokea kokote kule duniani.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) kwa mara ya kwanza tangu
alipoondolewa madarakani Novemba mwaka jana, amesema mapinduzi ya aina hiyo hayana
budi kulaaniwa na kila mwanamapinduzi.
Sikudhani Mnangagwa atanigeuka
Amesema hakufikiria kama Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, kwa
kushirikiana na jeshi kama angeweza kumgeuka na kumwondoa madarakani kama
ilivyoshuhudiwa na wengi.
Amesema Mnangagwa ambaye alimlea na kumwingiza serikalini na pia kumwokoa pale
alipotakiwa kunyongwa, amekuwa ni miongoni wa watu waliomhujumu na kumsaliti katika hali
ambayo hakutarajia.
Mugabe (94), amesema alilazimishwa na jeshi la nchi hiyo kuondoka madarakani baada ya
kupanga kuumaliza utawala wake wa miaka 37 na kwamba Mnangagwa amechukua madaraka
kinyume cha sheria na katiba.
Wachambuzi wanaamini kuwa uwezekano wa Mugabe kurejea katika siasa ni mdogo sana,
licha ya hivi karibuni mfuasi wake wa karibu, Brigedia mstaafu Ambrose Muntinhiri, kutangaza
kuanzisha chama kipya cha kisiasa kinachomuunga mkono.
Mugabe: Siutaki tena urais
Katika mahojiano mengine na kituo cha televisheni cha Uingereza (ITV), Mugabe alisema hana
hamu ya kurejea madarakani, kwani hataki tena kuwa rais na kuongeza kuwa kipindi
alichokikalia kiti hicho kinatosha.
Amesema hamchukii mrithi wake, lakini akamfananisha na mtu aliyelisaliti taifa zima na
anapaswa kuifuta aibu hiyo, na kuongeza kuwa Zimbabwe inatakiwa kuwa nchi inayoheshimu
katiba pamoja na sheria.
Mugabe alilazimika kuondoka madarakani baada ya jeshi kuingilia kati na kusababisha
maandamano ya umma pamoja na chama chake cha ZANU-PF kuanzisha mchakato wa
kumvua madaraka.
Mugabe alipewa kinga ya kutoshitakiwa na kuhakikishiwa usalama wake atakapokuwa raia wa
kawaida tangu aondoke madarakani. Mugabe amekuwa akiishi na mkewe, Grace, katika jumba
lake la kifahari mjini Harare.
Mmoja wa wafanyabiashara wa Zimbabwe, Munyaradzi Chihota, ameliambia shirika la habari la
Ufaransa (AFP) kuwa tangu Mugabe aondoke madarakani, hawajahisi mabadiliko ya aina
yoyote na badala yake hali inazidi kuwa mbaya, na kuongeza kuwa walichokuwa wanataka ni
kubadilishwa kwa mfumo mzima wa ZANU-PF na siyo mtu mmoja.