Nimrod Mkono aumizwa

*Nyumba ya Sh bil. 7 inauzwa kulipa Sh mil. 30

*Familia yapambana usiku, mchana kunusuru

* Tayari ofisi zake ghorofa 2 zimepigwa mnada

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Nyumba ya makazi ya mwanasheria na mwanasiasa nguli nchini, Nimrod Mkono, inapigwa mnada kulipa madeni, JAMHURI limethibitishiwa.

Miongoni mwa wanaomdai ni waliokuwa wafanyakazi katika Kampuni ya Uwakili ya Mkono & Company Advocates.

Mkono alikuwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), na baadaye Butiama kuanzia mwaka 2000. Mwaka 2015 alishinda ubunge kwa mara nyingine, lakini tangu mwaka 2016 yuko nchini Marekani kwa matibabu.

Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi jijini Dar es Salaam imebariki kuuzwa kwa nyumba ya Mkono iliyopo Msasani jijini humo.

Kuuzwa kwa nyumba hiyo kunatokana na kesi iliyofunguliwa na mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya Mkono & Company Advocates, Aisha Sinda. Katika madai yake, Aisha, anaidai kampuni hiyo malimbikizo ya mishahara na stahiki nyingine vinavyofikia dola 13,000 za Marekani (Sh milioni 30.134). Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, dola moja ya Marekani iliuzwa kwa Sh 2,318.

Familia ya Mkono inapinga uamuzi huo wa mahakama kwa maelezo kuwa thamani ya nyumba na ardhi inayouzwa ni zaidi ya Sh bilioni saba.

Binti wa Mkono, Leah, amezungumza na JAMHURI na kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo.

“Kweli kuna uamuzi wa mahakama, lakini tumeupinga kupitia kwa mawakili wetu, naomba uwasiliane nao wakupe maelezo zaidi,” anasema Leah.

Japo familia imegoma kuingia kwa undani katika suala hili, kuna taarifa kuwa nyumba inayouzwa si mali ya Kampuni ya Mkono & Company Advocates; bali ni ya familia ya Nimrod Mkono.

Mahakama ya Kazi imeamuru kuuzwa kwa nyumba hiyo kupitia shauri Na. 380/2020. Kazi hiyo amepewa Dalali wa Mahakama, Abdallah Abeid wa Kampuni ya Tambaza Auction Mart & General Court Brokers. Amri hiyo ya Agosti 4, mwaka huu, imesainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama, W. Ng’umbu.

Novemba, 2019 Benki ya Exim ilitangaza kupiga mnada mali za Kampuni ya Baobab Properties Limited ambayo Mkono ni mdhamini wake. Mali hizo ni zilizopo ghorofa ya nane na 10 katika Jengo la Exim lililopo Dar es Salaam.

Taarifa ya Exim Bank Tanzania inasema hatua hiyo inatokana na muda uliotolewa kwa kampuni hiyo kushindwa kulipa mkopo licha ya kuongezwa muda.

Exim ilifungua kesi Na. 21/ 2018 na Na. 59/ 2018 katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara. Kesi hizo ziliamuliwa kutokana na masharti ya kesi nyingine ya biashara Na. 59/2019 ambayo pia ilimhusu Mkono.

Exim inasema Juni, 2014 iliikopesha Baobao dola 750,000 za Marekani (Sh bilioni 1.7) Mkono akiwa mdhamini.

“Baobab ilishindwa kutimiza malipo. Hatua hiyo ilisababisha benki kutoa notisi ya kisheria ya kushindwa huko kwa Baobab na mdhamini Juni 13, 2016. Licha ya notisi hiyo na majaribio kadhaa ya benki, Baobab na mdhamini wake walishindwa kulipa mkopo huo kama ilivyotakiwa,” Exim inasema katika taarifa yake.

Baada ya kushindwa kulipa, benki hiyo ilianza kufuatilia dhamana ambazo ni mali za mkopaji Baobab zilizopo Kunduchi, Dar es Salaam. Baobab ilifungua kesi kupinga hatua hiyo. Benki ilifungua kesi Na. 59 ya 2018 kuomba amri ya mahakama ili Baobab ilipe mkopo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na benki dhidi ya Kampuni ya Baobab iliyoshindwa kulipa deni pamoja na mdhamini wake.

Kesi ikiwa inaendelea mahakamani, Baobab na mdhamini wake waliingia katika majadiliano ya kirafiki yaliyofikishwa mahakamani na kutolewa hukumu iliyoweka makubaliano kati ya pande mbili kusuluhisha jambo hilo.

Exim walisema Baobab na mdhamini wake walishindwa kutekeleza masharti, hivyo kuifanya benki hiyo irejee mahakamani kufungua kesi Na. 56/2018 kukazia makubaliano yaliyofikiwa.

“Hatua hii inaendelea chini ya amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kufuata utaratibu na sheria,” inasema sehemu ya taarifa ya benki hiyo.

Mkono alizaliwa Agosti 18, 1943 katika Kijiji cha Busegwe, Kata ya Busegwe, Wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Mkono ni miongoni mwa matajiri wachache nchini waliojitoa kwa hali na mali kusaidia maendeleo ya kijamii.

Katika Jimbo la Musoma Vijijini na baadaye Butiama, Mkono amejenga shule za msingi na sekondari nyingi. Baadhi ya shule hizo ni Chifu Ihunyo, Chifu Wazangi, Oswald Mang’ombe, Shule ya Sekondari Butuguri na Shule ya Sekondari Kasoma.

Shule zote hizi zimegharimu mabilioni ya shilingi. Shule mbili – Oswald Mang’ombe na Busegwe aliikabidhi serikali. Chifu Wanzagi inaendeshwa na madhehebu ya dini.

Jimbo la Musoma Vijijini lililokuwa na kata 36 na vijiji 119, hakuna sehemu ambayo haikupata kufikiwa na Mkono kimaendeleo.

Pamoja na shule, Mkono amechimba visima vingi katika vijiji vingi. Amejenga vyumba vya madarasa na maabara, amefungua barabara zote za enzi ya utawala wa wakoloni na mpya, amejenga mabweni katika shule nyingi kuanzia Busekela (magharibi) hadi Kyagata na Sirori Simba (mashariki). Amejenga zahanati, vituo vya afya, wodi, vituo vya polisi na majengo ya utawala sehemu nyingi.

Pia amejenga na kukarabati mabwawa na ameshirikiana na serikali kufanikisha kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Nyerere. Majengo ya Sekondari ya Oswald Mang’ombe yamekubaliwa yatumike kuanzisha chuo hicho.