DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Sinohydro wanaojenga barabara ya mabasi yaendayo haraka kutoka Kariakoo hadi Mbagala wamefukuzwa kazi huku wengine wakirejeshwa licha ya kufanya mgomo wiki iliyopita wakishinikiza kulipwa fedha za usafiri, chakula na malazi.

Wafanyakazi hao zaidi ya 1,000 waliogoma kwa siku sita na kumaliza mgomo wao wiki iliyopita, wanasema fedha hizo zinapaswa kulipwa kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi waliyokubaliana na Sinohydro kwa miaka miwili sasa.

Wakizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, wafanyakazi waliofukuzwa wanasema wenzao wamerudi kazini licha ya madai yao kutoshughulikiwa.

“Wenzetu wengi wamerudi kazini kwa sababu wanaogopa vitisho vya kufukuzwa kazi na tuliofukuzwa ni wachache, wamerudi lakini yale madai yetu hayajatatuliwa na sisi tumefukuzwa kazi kwa sababu tulionekana ni vinara wa kuanzisha huo mgomo wakati ukweli ni kwamba tulikuwa tunadai haki zetu,” anasema Pascal Gervas aliyekuwa anawasimamia madereva wa Sinohydro.

Naye Noel Ambonike ambaye ni dereva anasema licha ya kufukuzwa pia wamekosa sehemu sahihi ya kufikisha malalamiko yao ili yaweze kushughulikiwa kwa haraka.

“Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba tuliofukuzwa kazi tuko kati ya 18 hadi 20, kwa sababu tulionekana sisi tunawashawishi wenzetu wafanye mgomo wakati kile tulichokuwa tunakilalamikia ni haki yetu wote. 

“Tangu nianze kazi pale nina miezi mitano na madai yale nimeyakuta muda mrefu, changamoto za pale ni nyingi na hakuna mahala pa kusema, ile kampuni ina Watanzania lakini wanashindwa kutusaidia tupate haki zetu na kuna badhi ya viongozi wanajua madai yetu lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa ili kutusaidia,” anasema Ambonike.

Kiongozi wa wafanyakazi wa Sinohydro, Abedi Pazi, aliyekamatwa pamoja na wenzake watano kwa kudaiwa kuwa ni vinara wa mgomo huo ameachiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke.

Abedi ambaye naye amefukuzwa kazi alinukuliwa na vyombo vya habari siku ya mgomo huo akisema kuwa stahiki zao wameanza kuzidai tangu Aprili, mwaka huu lakini hakuna hata kimoja kilichoanza kushughulikiwa.

“Haya tunayoyadai yamo katika mkataba wetu na tuliambiwa fedha za chakula, malazi na usafiri zitajumuishwa katika mshahara, lakini siyo sisi tuliofukuzwa kazi wala hao waliorudi kazini ambao wameingiziwa hizo fedha.

“Kila tukijaribu kuulizia stahiki zetu tunatishwa kwamba tutafukuzwa kazi, alikuja Mkuu wa Wilaya ya Temeke hapa na akatoa siku saba madai yetu yashughulikiwe lakini hadi hivi sasa hayajashughulikiwa,” anasema Abedi.

Kwa upande wake, Amadeus William, aliyekuwa kitengo cha maabara hapo Sinohydro anasema hata makato ya mishahara yao kwa ajili ya kwenda kuchangia katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) hayapelekwi.

“Tunakatwa mishahara yetu kwa ajili kuchangia NSSF na watu wamefukuzwa kazi lakini tukienda kule NSSF tunaambiwa mwajiri wenu alikuwa hachangii na tukija kuulizia huku tunazungushwa na kupigwa chenga.

“Si hivyo tu, pia tunafanya kazi katika mazingira magumu na kuna baadhi ya wafanyakazi walikuwa wanaumia wakiwa katika majukumu yao kazini lakini wanajitibu kwa fedha zao wenyewe za mfukoni na si za ofisi,” anasema William. 

Naye mmoja wa wafanyakazi aliyerudi kazini ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuhofia kufukuzwa kazi, anasema licha ya madai ya stahiki zote wanazozilalamikia kuandikwa katika mikataba yao kwa Kiswahili, lakini hakuwahi kufuata masharti yake, pia anashindwa kulipwa mishahara na marupurupu ya kutosha. 

Pia mfanyakazi huyo anazidi kusema kuwa wakati mwingine wanapewa vifaa vichache vya usalama na kinga katika maeneo ya kazini, tofauti na utaratibu wa kazi unavyotaka.

JAMHURI lilimtafuta Ofisa Rasilimali Watu wa Sinohydro, Goodluck Minja, ili kufahamu kama madai ya stahiki za wafanyakazi hao yameanza kutatuliwa, lakini kupitia simu yake ya mkononi hakupokea, licha ya kupigiwa kwa siku kadhaa mfululizo na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno pia hakujibu, licha ya kuonyesha ameupokea.

Katika hatua nyingine, wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari vilizuiliwa na walinzi wa Sinohydro kumuona ofisa mwajiri ili azungumzie mgomo huo, kwa madai kwamba alikuwa katika kikao cha kuwajadili watu waliogoma.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila, amenukuliwa wiki iliyopita akisema anaufahamu mgomo huo lakini baada ya kufuatilia wamebaini katika mikataba ya wafanyakazi hao hakuna kipengele kinachoeleza wanatakiwa kulipwa stahiki hizo.

By Jamhuri