Watu ni nguvu. Ukikaa na watu bora utakuwa mtu bora. Ukikaa na watu wa kawaida utakuwa mtu wa kawaida. Ukikaa na watu wanaowaza mambo hasi utaanza kuwaza mambo hasi, ukikaa na watu wanaowaza mambo chanya utakuwa mtu chanya.

Ukiwa na ndoto unahitaji kuambatana na watu wenye ndoto. Ukiwa na maono makubwa unahitaji kuambatana na watu wenye maono makubwa. Tai siku zote haruki na kunguru, bali huruka na tai wenzake. Waswahili wanakwenda mbali na kusema, “Kaa karibu na waridi unukie.”

Marafiki tunaowachagua na kuambatana nao wana mchango mkubwa katika kutimiza ndoto zetu. Marafiki wanaweza kusababisha ndoto yako itimie na marafiki wanaweza kusababisha ndoto yako isitimie pia. Unahitaji kuwa na hekima kubwa kuchagua ni nani wa kuambatana naye au ni yupi si wa kuambatana naye.

Yusufu alipotupwa gerezani, alifungwa pamoja na watu wenye ndoto. Je, watu wanaokuzunguka wana ndoto gani? Je, watu uliowaajiri wana ndoto na maono makubwa?

Hayo ni maswali muhimu ya kujiuliza leo hii. “Niambie rafiki zako, nikwambie tabia yako,” ni msemo wa Kiingereza. Marafiki zetu wanaonyesha sisi ni watu wa namna gani.

Marafiki tulio nao wanaathiri tabia zetu. Tabia walizonazo watu wanaotuzunguka mara nyingi huendana na tabia zetu pia. Ipo wazi kuwa marafiki ulionao leo hii ni kwa sababu kuna kitu kimoja mnachokipenda kinachowaunganisha.

Mara nyingi tunakuwa kama wale tunaotumia nao muda wetu mrefu. “Ukienda mahali wanapokula konokono, utaanza kula konokono pia,” ni msemo wa Kihaya.

Jimh Rohn aliwahi kusema, “Wewe ni wastani wa watu watano unaotumia nao muda wako mwingi.” Wataalamu wa mambo ya uchumi wanakwenda mbali na kusema ukichukua wastani wa kipato cha marafiki zako watano, utapata karibia kabisa na kipato chako wewe. Inawezekana una ndoto ya kumiliki kampuni yenye kutengeneza kipato cha shilingi zaidi ya milioni 200 ndani ya miezi miwili, lakini kwa sababu unaambatana na watu wenye akili za ukomo wa kutengeneza milioni moja tu kwa mwezi, si rahisi ndoto zako kutimia. Jichunguze leo unaambatana na kina nani.

Wewe pia unahitaji kuwa mtu bora kwa wale wanaokuzunguka. Kuwa mfano wa kuigwa kwa wale wanaokuzunguka. “Ee Bwana unifanye niwe chombo cha amani, palipo na chuki nilete upendo. Palipo na makosa nilete msamaha. Palipo na shaka nilete imani. Pasipo na matumaini nilete tumaini. Palipo na giza nilete mwanga. Palipo na huzuni nilete furaha. Ee Bwana unisaidie nitamani sana: kufariji kuliko kufarijiwa. Kufahamu kuliko kufahamika. Kupenda kuliko kupendwa,” aliomba Mtakatifu Fransisco wa Asisi.

Hauwezi kuchagua ndugu, lakini marafiki unaweza kuchagua. Kama unatafuta marafiki tafuta watu wenye ubora zaidi yako. Tafuta watu wanaoweza kukuimarisha na si kukubomoa, tafuta watu wenye mtazamo chanya. “Kama chumba ulichomo wewe ndiye bora, chumba hicho hakikufai,” (Grant Cardone).

“Nimefika hapa nilipo kwa kusimama kwenye mabega ya watu wengine,” alisema Albert Einstein. Wewe unasimama kwenye mabega ya kina nani? Tazama hapa, Socrates alimfundisha Plato, Plato akamfundisha Aristotle. Dunia inawatambua leo hii kama wanafalsafa wakubwa. Ndoto yako itatimia pale unapoambatana na watu wenye ndoto kama zako.

Achana na watu wasiokuwa na ndoto kubwa kama zako. Acha kuzungukwa na watu wasio na mchango mkubwa kwenye ndoto zako. “Uchunguzi uliofanywa na mwanasaikolojia Dk. David McClelland wa Chuo Kikuu cha Harvard, anasema, watu wanaokuzunguka muda mrefu wanachangia asilimia 95 ya mafanikio au kushindwa kwako,” ameandika Darren Hardy kwenye kitabu chake kiitwacho The Compound Effect.

Acha kuambatana na watu wanaolalamika kila kukicha, wanalalamika kuhusu kazi zao, wanalalamikia serikali, wanalalamika kwamba wazazi wao hawakuwasomesha, wanawalalamikia mabosi wao, wanalalamika karibia kila kitu. Ukiambatana na watu wa aina hiyo utakuwa kama wao. Watu wengi hufanana na vinyonga, wanabadilika kutokana na mazingira yanayowazunguka.

Kama unamiliki biashara na unaajiri watu, hakikisha unaajiri watu bora. “Kama kuna kitu kimoja muhimu ambacho huwa nakizingatia na watu wengi wanaotafuta ajira wanahitaji kukifahamu ni kuwa na mtazamo chanya,” anasema Patrick Bitatule, mfanyabiashara toka Uganda.

By Jamhuri