Katika dunia kuna mambo yakitokea unajiuliza kwa nini yametokea. Unajiuliza ni hivi hivi au kuna msukumo, ila yote kwa yote nimejiwekea utaratibu wa kusimamia ukweli. Mara zote naamini ukweli unamweka mwanadamu huru, na hapa leo kama nifanyavyo siku zote nitajaribu kueleza ukweli ninaoufahamu.

Sitanii, leo nazungumzia ajenda moja tu — urais 2015. Nimefuatilia kwa karibu na kuwasiliana na watu mbalimbali kuhusiana na mchakato wa urais mwakani. Nimeshuhudia mwenendo wa baadhi ya magazeti, redio na televisheni jinsi yanavyoandika habari kuhusiana na wanaodhaniwa kuwa ni wagombea watarajiwa.

Ni wazi si jambo baya kuieleza jamii kinachozungumzwa kwa sasa kuhusu wagombea watarajiwa, juu ya mtazamo wao katika haiba, uadilifu, historia ya utendaji wao, malengo yao kwa Taifa na uwezo binafsi wa mgombea mtarajiwa. Haya ni mambo tunayopaswa kuyasema kwa nia ya kuwasaidia wapigakura kufahamu wanamchagua nani na kwa nini.

Nimesema sitajizuia kusema ukweli. Kuna habari iliyochapishwa na gazeti ninaloliheshimu kwa kiwango kikubwa, ikanikumbusha siasa alizoziita ‘Maji Taka’, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta. Sitta alipata kusema kuwa tuwaache wananchi wamchague rais mwenye uwezo bila kumwekea vikwazo mgombea.

Maneno ya Sitta yalinikumbusha maneno ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba alichompangia mtu Mungu hutokea. Mkoa ninakotokea kuna lugha ya kimataifa ambayo maneno yake yanasema hivi: “Omugisha mbeo, nolwo wakukinga olwigi elabamu.” Tafsiri ya maneno haya ni kuwa ‘bahati ni sawa na baridi, hata ukifunga mlango inapita’.

Naelewa mbio zilizopo. Nafahamu majina yanayotajwa kuwa watakuwa wagombea urais mwakani, akiwamo Samuel Sitta, Bernard Membe, Edward Lowassa, Stephen Wasira, Emmanuel Nchimbi, Anna Tibaijuka, Dk. Asha-Rose Migiro na wengine waliojitangaza akina January Makamba, Dk. Hamis Kigwangalla na wengine.

Sitanii, kilichonisukuma kuandika makala hii ni mfumko wa habari ninazoamini tusipoziweka sawa tutakuwa tunaipotosha jamii. Tunatumia nafasi yetu kutimiza malengo yetu kisiasa, ambayo kimsingi tunaweza kuishia kuilisha sumu jamii bila kujua. Katika makala hii nitazungumzia habari inayohusu mradi wa maji ya Ziwa Victoria.

Kabla sijaujadili mradi huu, niweke hapa chini Katiba inasema nini. Msomaji wangu soma ibara hizi za 54 na 55 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) kisha urejee habari hiyo ninayosema ilinichefua na kuona imeshusha heshima na kiwango cha taaluma ya wanahabari, kwani yapo mambo hustahili kuwa mwanasheria kuyafahamu.

Ibara ya 54 (1) inasema; Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Mawaziri wote.(2) Rais atahudhuria mikutano ya Baraza la Mawaziri na ndiye atakayeongoza mikutano hiyo. Na endapo Rais hayupo basi mikutano itaongozwa na Makamu wa Rais na kama wote wawili Rais na Makamu wa Rais hawapo, Waziri Mkuu ndiye atakayeongoza mikutano hiyo. (3) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara ya 37(1) ya Katiba hii, Baraza la Mawaziri litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais juu ya mambo yote yanayohusika na utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, na litamsaidia na kumshauri Rais juu ya jambo lolote litakalowasilishwa kwenye Baraza hilo kwa mujibu wa maagizo maalum au maagizo ya jumla yatakayotolewa na Rais. (4) Mwanasheria Mkuu wa Serikali atahudhuria mikutano yote ya Baraza la Mawaziri na atakuwa na haki zote za mjumbe wa mikutano hiyo isipokuwa hatakuwa na haki ya kupiga kura katika mikutano hiyo. (5) Suala kama ushauri wowote, na ni ushauri gani, ulitolewa na Baraza la Mawaziri kwa Rais, halitachunguzwa katika Mahakama yoyote.

55 (1) Mawaziri wote ambao ni wajumbe wa Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 54, watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

(2) Pamoja na Mawaziri waliotajwa katika ibara ndogo ya (1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, kuwateua Naibu Mawaziri. Naibu Mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri. (3) Rais aweza kuteua idadi yoyote ya Naibu Mawaziri ambao watawasaidia Mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao. (4) Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge. (5) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) ikitokea kwamba Rais anahitajiwa kumteua Waziri au Naibu Waziri baada ya Bunge kuvunjwa, basi aweza kumteua mtu yeyote ambaye alikuwa mbunge kabla ya Bunge kuvunjwa.

Sitanii, nimesoma makala iliyoandikwa na gazeti moja juu ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria katika mahojiano na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo. Si nia yangu kumjibu Diallo wala kuanzisha malumbano na gazeti hilo ila nataka kuweka kumbukumbu sawa.

Sitarejea kila alichokisema Diallo isipokuwa machache tu, kwa nia ya kunisaida kueleza ninachokikumbuka kuhusu mradi wa Maji Ziwa Victoria kutoka Mwanza hadi Shinyanga na Kahama. Naamini kumbukumbu zangu ni sahihi na nitawataja waliokuwapo wakati yakitokea hayo nitakayoyasema kwa mwenye kutaka kujiridhisha awaulize.

Kwamba naanza na hili la kisheria. Katika mahojiano hayo, Diallo amesema yeye ndiye aliyesimamia mradi wa Maji wa Mwanza, Shinyanga na Kahama na Lowassa alikuwa anasimamia DAWASCO. Lowassa alikuwa Waziri wa Maji wakati huo. Na Diallo amesema yeye kupitia Baraza la Mawaziri ndiye aliyependekeza mradi huo na njia ya kupata fedha. Katika hili sitazungumza sana ila nakuwekea nukuu za Katiba ya Tanzania.

Ibara ya 55 (2) inasema, Pamoja na Mawaziri waliotajwa katika ibara ndogo ya (1), Rais aweza, baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, kuwateua Naibu Mawaziri. Naibu Mawaziri wote hawatakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri.

Ibara ya 55 (3) inasema, Rais aweza kuteua idadi yoyote ya Naibu Mawaziri ambao watawasaidia Mawaziri katika utekelezaji wa kazi na shughuli zao.

Hapo sitaongeza neno. Nilishtuka sana Diallo aliposema alishiriki kufanya uamuzi ndani ya Baraza la Mawaziri, ambalo yeye kama Naibu Waziri Katiba inatamka wazi kuwa naibu mawaziri wote si wajumbe wa Baraza la Mawaziri. Diallo atwambie aliingiaje kwenye Baraza? Anataka kusema Rais Benjamin Mkapa alivunja Katiba kwa kumwingiza Diallo kwenye Baraza la Mawaziri akiwa Naibu Waziri? Naomba jibu.

Kuhusiana na hilo, kuna Sheria ya Baraza la Mawaziri Na 15 ya Mwaka 1984. Sheria hii inataja kazi za Naibu Mawaziri kuwa ni wasaidizi wa Mawaziri. Kwa maana nyingine kila kazi anayofanya Naibu Waziri anakuwa ametumwa na Waziri wake, anatekeleza maelekezo halali ya waziri wake na hivyo anafanya kazi kwa niaba ya waziri. Ikiwa Diallo alifanya hivyo, alifanya kwa maelekezo ya waziri wake Lowassa. Pia sheria hii inaeleza vyema kuwa kazi ya msingi ya Naibu Waziri ni kujibu maswali bungeni. Hawa ni makatibu wa Bunge katika wizara, basi. Kwa Kiingereza imetamkwa bayana kuwa Naibu Mawaziri ni Parliamentary Secretaries. Kumbe hii sheria inatwambia hata kama Diallo alifanya kazi hiyo kweli, alikuwa akitekeleza jukumu la kikatiba la kumsaidia Waziri wake, Lowassa.

Sitanii, ingawa Diallo anasema Lowassa hastahili hata chembe ya sifa kwenye mradi wa Maji wa Mwanza, Shinyanga hadi Kahama, ninalo la kukumbuka. Mwaka 2004 nilipata kusafiiri katika ujumbe wa Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Mataifa (UN) kutoka Tanzania kwenda Cairo, Misri. Katika msafara huu tulikuwa na wabunge na waandishi wa habari. Nia ilikuwa kumaliza mgogoro wa maji katika Mto Nile, baada ya Tanzania kufanya uamuzi wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga na Kahama.

Kiongozi wa msafara alikuwa Edward Lowassa. Wabunge nitawaorodhesha hapa chini. Tulifanyia mkutano katika Hoteli ya Conrad katikati ya Jiji la Cairo. Tulitembelea miji ya Abu Simbo, Aswan na Alexandria.

Tulishuhudia jinsi Wamisri wanavyotumia maji ya Mto Nile kufanikisha kilimo. Kwenye jangwa wamejenga mitaro mirefu yenye kuchukua maji kwa kiwango cha mita za ujazo 55 kwa sekunde.

Katika mkutano na Waziri wa Maji wa Misri, Dk. Abu Zeid, aliyekuwa ameshikilia wadhifa huo kwa miaka 24 mfululizo, uliohudhuriwa na mawaziri wengine tisa akiwamo ninayemkumbuka kwa jina moja, Dk. Atia ndipo uamuzi halisi wa mradi huu ulipofanyika. Wamisri walikuwa wamejiandaa kupigana hata vita ikibidi, kuhakikisha Tanzania haichukui maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Shinyanga na Kahama kwa maelezo kuwa walikuwa na mkataba na Uingereza unaozizuia nchi zote zilizokuwa makoloni ya Uingereza kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria bila kibali cha Misri.

Lowassa alijenga hoja mbili katika mkutano huo na kuhitimisha kama ifuatavyo: “Kwanza sisi tunachukua ujazo wa mita 1.5 kwa sekunde kwa ajili ya watu wetu, wakati nyie mmechepusha mita za ujazo 55 kwenda kumwagilia mazao yenu jangwani. Sielewi mnapata wapi ujasiri wa kuona heri watu wetu wafe kwa kiu ya maji, lakini nyie muendelee kuyatumia mtakavyo.

“Pia nataka ifahamike kuwa sisi Tanzania si sehemu ya mkataba huo. Mkataba unasema makoloni ya Uingereza, sisi Tanzania hatujawahi kuwa koloni la Uingereza, bali nchi yetu iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, hivyo kama mnayatafuta makoloni, Tanzania si mojawapo… kuhusu suala la vita, kwa ajili ya kulinda uhai wa watu wetu tuko tayari kwa hilo hata leo.”

Zilikuwapo habari nyingi kwenye magazeti ya Misri zikitoa tishio kuwa ikibidi Misri iipige vita Tanzania kwa kuchukua maji kwenye Ziwa Victoria kupeleka Shinyanga na Kahama. Baada ya kauli hii nzito ya Lowassa, mawaziri tisa wa Misri waliokuwa kwenye mkutano huo walilegea ghafla, hasa kwa hoja ya koloni, wakajikuta hawakulijua hilo na ile hoja ya kwamba Tanzania haiogopi vita.

Sitanii, ghafla msimamo wa Wamisri uliyeyuka baada ya majibu hayo, wakaanza lugha za kuangalia jinsi ya kushirikiana kufanya kazi pamoja. Wakaanza lugha ya jinsi gani Misri inavyoweza kuisaidia Tanzania katika harakati zake za kuondoa umaskini. Kwa kulijua hilo, mwaka 2005 Lowassa alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Misri ilituma ujumbe mzito wa mawaziri 12 kuja Tanzania kuleta salamu za pongezi kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Wakati Lowassa anatoa maneno haya makali jijini Cairo walikuwapo wabunge ambao baadhi nawakumbuka. Walikuwapo Thomas Ngawaiya (Moshi Vijijini-TLP), Shaweji Abdallah (Kilosa-CCM), Charles Kagonji (Mlalo-CCM), Said Nkumba (Sikonge-CCM) na Kidawa Himid Salehe (Viti Maalum-CCM).

Kwa upande wa waandishi wa habari nakumbuka waliokuwapo na vyombo walivyokuwa wanafanyia kazi na walipo sasa kuwa ni Lucas Liganga (Daily News-Citizen), Neville Meena (Star TV-Mwananchi), Obed Mwangasa (ITV- Kujitegemea), Magreth Chambiri (TVT/TBC-Tume ya Taifa ya Uchaguzi), Badra Masoud (Mtanzania-Wizara ya Nishati na Madini), Manyerere Jackton (Majira-Jamhuri) na mimi Deodatus Balile (Mwananchi-Jamhuri).

Sitanii, wiki iliyopita nilishtuka sana Diallo aliposema yeye ndiye aliyeamua wakiwa Ethiopia kuwa Tanzania lazima itekeleze mradi huu. Nafasi inazidi kuwa ndogo. Nimeona nieleze haya ninayoyafahamu kuhusu mradi huu, si kwa nia ya kumshushua yeyote kwa mamlaka yake au utashi wake kisiasa, bali kuweka kumbukumbu sawa. Namba yangu ipo hapo juu Diallo au yeyote anayetaka ufafanuzi wa ziada katika hili anipigie.

2287 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!