DODOMA

Na Javius Byarushengo

Miongoni mwa nadharia zinazohusiana na chanzo cha uhalifu katika jamii ni ‘nadharia ya migogoro’ (conflict theory). 

Nadharia hii inaeleza kuwa tabia potofu ni matokeo ya kutokuwapo usawa wa kiuchumi na kisiasa katika jamii.

Wananadharia wanasema migogoro huuchukulia uhalifu kwa kuuhusisha na misukosuko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi iliyoanza kutokea katika miaka ya 1960 (Adler, Mueller & Laufer, 2001).

Nadharia za kijamii kuhusu uhalifu na makosa mfano nadharia ya migogoro huenda mbali na kuibua maswali mengi kuwa mifumo ya kiutamaduni na kisheria katika jamii vipo kwa ajili ya kulinda masilahi ya kundi fulani linaloshikilia uwezo wa kisiasa.

“Kwa mantiki hiyo msingi wa nadharia ya migogoro unaohusu dhana ya uwezo/mamlaka/nguvu ndiyo yenye mizizi ya uasi, migogoro ya kitabaka na kifalsafa.” (Shoemaker, 1990).

Nadharia ya migogoro ndiyo huashiria kwamba mwenye uwezo, kwa maana ya mwenye nacho ndiye huongezewa na ndiye mwenye nguvu katika uamuzi wa kufanya jambo lolote.

Kusigana kati ya wenye nacho wachache na wasio nacho wengi ndiyo husababisha migogoro mikubwa katika jamii na mwishowe baadhi ya makundi yanayodhani yameachwa nyuma kuamua kutafuta mbinu za kujikwamua kisiasa na kiuchumi.

Ni katika mazingira haya ya kupambana kujikwamua kuondokana na unyonge ndipo mbinu nyingine hasi hutumiwa na walengwa.

Kwa muda mrefu wanasiasa wakubwa serikalini, hususan wabunge, mawaziri na wengine, hunyoshewa vidole na wanajamii kuwa wanalipwa mishahara na marupurupu makubwa ilhali wananchi/wapiga kura ni maskini wa kutupwa.

Hebu tutazame mishahara, posho na marupurupu mengine wanayopata wabunge.

Taarifa iliyowahi kutolewa na Zitto Kabwe wakati akiwa Mbunge wa Kigoma Mjini mwaka 2015, inaonyesha kwamba mshahara wa mbunge mmoja wakati huo ulikuwa Sh milioni 3.8 kwa mwezi; posho ya ubunge Sh milioni 8 kwa mwezi; posho ya kujikimu Sh 120,000 kwa siku na posho ya kikao bungeni Sh 200,000 kwa siku.

Kwa upande mwingine, ufafanuzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu stahiki na mshahara wa Mbunge wa zamani, Tundu Lissu unasema kuwa tangu Septemba 7, 2017 mpaka Desemba 31, 2018, Lissu alilipwa Sh Milioni 207.
Kiasi hicho ni fedha za miezi 15 tu, ambacho ni sawa na Sh 13,800,000 kwa mwezi bila kuhusisha posho ya mahudhurio ya vikao vya Bunge inayosemekana kuwa ni Sh 350,000 kwa siku (hakuhudhuria kwa kuwa alikuwa nje ya nchi kwenye matibabu).
Ukitazama kwa makini utagundua hatari iliyopo, kwa kuwa kuna kada nyingine za wafanyakazi hulipwa Sh 400,000 tu kwa mwezi!

Mwalimu wa shule ya msingi (ngazi ya cheti) anayehangaika na vumbi la chaki kumkomboa mtoto kifikra, analipwa shilingi ngapi kwa mwezi?

Ni hatari kwa maana kwamba tofauti hii kubwa kiasi hiki katika taifa ambalo watu wake ni maskini, lazima italeta migogoro ambayo katika jamii inaweza kuzaa uhalifu.

Mazingira kama haya huchochea wengine kuiba, kunyang’anya kwa nguvu ili wazibe pengo la kiuchumi au kujaribu kukaribiana au kufanana na maisha wanayoishi wenye posho kubwa kubwa.

Mishahara mikubwa ya wanasiasa ndiyo husababisha baadhi ya watumishi wa umma au sekta binafsi wenye kipato duni ambao si wacha Mungu, kujihusisha na rushwa na ubadhirifu kwa kuziba pengo la kiuchumi au kutaka kufanana kimaisha na wengine.

Mishahara mikubwa ya wabunge na wengineo huchochea tamaa ya baadhi ya watu kugombea vyeo vya kisiasa wakitafuta ushindi kwa gharama yoyote hata kwa njia haramu kama kupiga ramli; kutoa kafara na ushirikina.

Ni mishahara kama hii inayosababisha unyanyapaa wa baadhi ya wasomi kwa taaluma zao wenyewe na kuingia kwenye siasa. 

Hivi daktari akiacha kazi hiyo na kuingia kwenye siasa si anakuwa amehatarisha afya za wananchi wanaohitaji huduma yake?

Wahadhiri wakubwa wa vyuo vikuu wanapoamua kuacha kufundisha na kujiunga kwenye siasa, hususan kugombea ubunge ili kupata kipato kikubwa ni kuhatarisha mustakabali wa elimu ya taifa letu.

Kwa hakika mishahara minono hujenga chuki na uhasama kati ya kundi moja na jingine (wenye nacho na maskini.)

Usitegemee mtoto wa mwanasiasa anayeishi kama yuko peponi, akila na akisaza, matibabu bora, malazi mazuri na shule za maana atakuja kupendwa na mtoto wa maskini anayekula kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Usitegemee vijana maskini waliomaliza shule, vyuo na vyuo vikuu wakirandaranda mitaani kusaka ajira watawapenda vijana wenzio kutoka familia za wanasiasa wenye mishahara mikubwa wanaopewa fursa ya kuchagua kazi wanazotaka kufanya.

Serikali inapotafakari namna ya kutokomeza uhalifu unaoibuka mara kwa mara licha ya adhabu zilizopo, isisahau kuangalia chanzo chake, ikiwamo tofauti ya kipato kati ya mabwana wakubwa na wanyonge wanaolalia uji wa dona bila sukari.

javiusikaijage@yahoo.com, 0756 521 119

418 Total Views 10 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!