Tuamke, muda unatukimbiza

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Nchi imo kwenye majonzi. Ni majonzi makubwa, hasa kwa mashabiki wa soka. Ni juzi tu tumetoka kufungwa mabao 0 – 3 na DRC. 

Kipigo hicho hakijaishia kutuumiza mioyo pekee, bali pia kimekatisha ndoto zetu za kwenda Qatar 2021 kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Tumefungwa kwenye ardhi yetu ya nyumbani; kwenye uwanja wetu. 

Huenda haya ndiyo matokeo yaliyotuuma zaidi sisi kama Watanzania katika miaka ya hivi karibuni. Kwa hakika yalikuwa na bado ni matokeo ya kikatili sana. 

Lakini hakuna namna tunayoweza kufanya zaidi ya kukaa chini na kujiuliza wenzetu wanafanikiwa wapi, sisi tunafeli wapi? Tunapaswa kujiuliza swali hili kwa makini na kuyasaka majawabu mujarabu bila kutafuta mchawi ni nani. 

Ligi zetu, kuanzia Ligi Kuu na nyinginezo, zimeshindwa kutuandalia wachezaji bora. Wachezaji wenye uwezo wa kupambana na kushindana na wachezaji wa mataifa mengine. 

Sasa tufanye nini? Kwa hali iliyopo kwa sasa ingependeza sana kama serikali itashirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuandaa vijana wa kuanzia umri wa miaka tisa hadi 15, wenye vipaji maalumu na kuwapeleka nje ya nchi kujiendeleza kielimu na kisoka.

Tanzania tumekuwa tukijipambanua kuwa na diplomasia nzuri ya kimataifa, kwamba tuna marafiki ‘wa kweli’ wengi tu. Hii maana yake kuna nchi kadhaa tuko nazo vizuri sana katika uhusiano wa kijamii na kidiplomasia.

Wakati umefika sasa kwetu sisi kuzitumia nchi hizo kuandaa wachezaji ambao watakuja kulipa faida na heshima taifa letu.

Zipo nchi nyingi zilizoendelea zinazoweza kuwapokea watoto hawa kwenye shule zao za soka (academy) wakajifunze mpira, huku na sisi tukiendeleza programu mbalimbali za kuandaa watoto na kuwapatia elimu bora zaidi ya soka la kisasa linalokubalika kimataifa.

Hili suala si la Rais wa TFF pekee, Wallace Karia, pamoja na maofisa wake pale Karume, bali hili ni jambo la wadau wote; kuanzia serikali, taasisi zake nyingine na hata sisi mashabiki wa soka mitaani; mijini na vijijini.

Zijengwe shule nyingi za michezo yote katika ujumla wake kadiri inavyowezekana. Serikali ikijenga miundombinu bora ya viwanja, bila shaka na hii ni hakika kabisa kwamba kila mwaka kuna hatua tutakuwa tunapiga katika michezo.

Tukiwa na mipango hii, ndani ya miaka mitano tutakuwa na viwanja bora 10 vya michezo mbalimbali. Hii itafanya tuendeshe michezo yetu kwenye ubora mkubwa wa kimaendeleo.

Lazima tuwe na shabaha za namna hii. Muda mrefu kama taifa tumepoteza muda kuja na mipango mingi tofauti ambayo haijatusaidia.

Zaidi linatupotezea muda na kutupa matumaini ya kitu ambacho hatukujiandaa nacho. Ni wakati wa kuamka Tanzania na twende mbele.

Naamini kama tukiwa na nia ya dhati mpira wetu utaanza kuonekana. Hizi ahadi, hamasa za zimamoto ni kitu kingine ambacho tunajaribu kuvuka mto wenye mamba kwa kuvaa ‘Life Jackets’ badala ya boti yenye injini.

Ukweli unauma, lakini ndiyo tiba. Ofisi ya TFF yenyewe haiwezi kufanya mambo haya peke yao na kutupa mafanikio. Ni lazima washikwe mkono.

Soka linahitaji uwekezaji mkubwa. Vituo vya TFF pale pale Kigamboni na Tanga ni vidogo, tunahitaji Center za namna ile nyingi katika kila mkoa. 

Lazima tujenge viwanja vya kisasa vyenye majukwaa na maduka makubwa ya vifaa vyote vya mpira wa miguu pamoja na majarida ya soka na miongozo ya ufundishaji soka.