DAR ES SALAAM

Na Dk. Boniphace Gaganija

Kwa mfululizo, matoleo mawili ya Gazeti pendwa la JAMHURI, Bernard Membe, amekuwa akiwaelezea Watanzania chuki yake dhidi ya Serikali ya Awamu ya Tano na CCM kwa kipindi hicho.

Swali langu ni je, hivi Membe ni mtu mashuhuri aliyechanganyikiwa?

Swali hili ni kwa sababu hii ni mara ya pili kuibuka na hoja za ajabu ajabu. Membe aliwahi kuibuka na ajenda ya Tanzania kujiunganisha na Organization of the Islamic Cooperation (OIC), ili tupate misaada kutoka nchi za Ghuba.

Wakati huo alijisahau kabisa kuwa anatoka katika moja ya mikoa yenye gesi asilia nyingi na uzalishaji wa korosho bora duniani kwa kiwango cha kutohitaji msaada wa nchi yoyote.

Mazungumzo yake yamejaa lawama na tuhuma nzito kwa viongozi wa CCM na Serikali ya Awamu ya Tano. Nimeendelea kusoma kwa makini sana maelezo yake na inanipa swali moja kubwa, kwa nini ameibuka wakati huu?

Swali hili anaweza kulijibu yeye mwenyewe, lakini kwa upande wangu ninamuona Membe kama mtu mashuhuri aliyechanganyikiwa.

Nasema amechanganyikiwa kwa sababu ya yeye kushangaa, kulaumu na kulalamika kama mtu mwingine yeyote asiyejua kitu chochote.

Katika mazungumzo yake anaonekana kuguswa binafsi na matukio ya watu kupotea au uwepo wa watu wasiojulikana katika Awamu ya Tano.

Kwa kifupi ninapenda kumkumbusha kuwa usalama wa nchi yetu ulianza kulegalega kipindi yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nje; wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Itakumbukwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne upande wa usalama wa raia kulikuwa na udhaifu mkubwa sana na hofu kubwa mno ilitanda kwa wananchi.

Magenge ya kihalifu, dawa za kulevya yalitikisa mitaa na mikoa. Ni kipindi cha Awamu ya Nne benki zilivamiwa na kuporwa fedha, watu walipigwa risasi, kuuawa na kunyang’anywa mali au fedha.

Vibaka nao hawakubaki nyuma kutetemesha mitaani. Ni kipindi hicho hicho wafanyabiashara ya madini waliuawa sana mkoani Arusha, wahuni wenye silaha za moto waliteka mapango ya Amboni mkoani Tanga na kuua watu, vituo vya polisi vilivamiwa silaha zikaibwa na askari kuuawa.

Membe ulikuwamo serikalini, tena tunaamini ulikuwa mmoja wa mawaziri pendwa sana na werevu wa masuala ya ulinzi na usalama.

Hatukuona faida ya wewe katika kuikabili vita hii na kuwasaidia wananchi kupona na kulinda mali zao!

Tukizingatia kwamba wewe ni nguli katika masuala ya usalama na kazi hii ya kuhakikisha Tanzania iko salama uliifanya kwa miaka mingi sana, ndiyo maana nimekuita mtu mashuhuri.

Ukiwa waziri wa Mambo ya Nje, ulikuwa na nafasi hata ya kuomba msaada wa mataifa makubwa kutusaidia kukabiliana na wahalifu hao waliowaua ndugu zetu na kuchukua mali zetu. Haukufanya chochote. Je, hukuona haya yakitokea?

Membe ulikuwapo wakati miji ya Liwale na Masasi ikichomwa moto kwa hasira za wananchi kutapeliwa mauzo ya korosho.

Ni ukweli usiopingika kuwa ujambazi, ugaidi na ujangili vilitamalaki Awamu ya Nne na kufikia kiwango cha hata kuzoeleka.

Vitendo hivi hatari viliendelea mwanzoni kabisa mwa Awamu ya Tano. Utakumbuka mauaji ya kutisha Mkuranga, Kibiti na Rufiji yaliyotokea mwishoni mwa 2016 na mwanzoni mwa 2017.

Hadi leo hakuna jibu la moja kwa moja la ni wapi hasa makundi haya ya mauaji yalikotoka na kuzua tafrani ya aibu Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Wauaji hawa walipenya na kukaribishwa na jamii iliyo kata tamaa baada ya dhuluma kubwa juu yao kupitia mazao ya misitu; fito, kuni, mkaa na mauzo ya korosho.

Kwa takriban muongo mmoja, Tanzania ilikuwa na makundi matatu gizani, kwa sehemu kubwa giza hili la hofu lilitawala wakati wewe ulikuwa kiongozi mkubwa serikalini.

Yaani, kundi la watu lililoendesha mauaji, ujangili, uporaji, dawa za kulevya na dhuluma. Kundi la pili ni serikali; ikijitahidi kukabiliana na hatari kubwa ya usalama; na kundi la tatu ni la wananchi tuliojaa hofu na shaka juu ya usalama wetu.

Kwa hiyo Awamu ya Tano ilirithi changamoto hii mbaya sana kwa mustakabali wa Tanzania. Lakini kwa juhudi kubwa Serikali ya Awamu ya Tano ilikomesha kabisa uhalifu huu, dhuluma na dawa za kulevya yakakabiliwa vizuri sana.

Watanzania bado tuna maswali yafuatayo: Je, ni nani aliendesha ugaidi, mauaji na uporaji huo? Je, ndugu zetu waliopotea hadi sasa walikuwa raia wema? Au walisaidia serikali kuwapata magaidi?

Na magaidi wakawateka na kuwapoteza kama kisasi? Au walikuwa sehemu ya magaidi ambao vyombo vya ulinzi na usalama viliwashughulikia?

Bernard Membe, umesema wazi kuwa una mtandao wako (Network) inayo kusaidia kujua mambo mengi kabla ya kukupata. Je, mtandao wako unaweza kutusaidia kupata majibu ya maswali haya na kujua ndugu zetu waliopotea wako wapi? 

Azoli, Ben Saanane n.k wako wapi? Ni nani alimpiga risasi Tundu Lissu? Lengo ni kuliponya taifa letu. Lakini kama hauna majibu ya maswali haya, basi tulitegemea wewe mtu mashuhuri ungelikuwa na ajenda binafsi, kuomba uchunguzi ufanyike kujibu maswali haya badala ya kulaumu na kushangaa. 

Ungelisukuma ajenda ya tume huru ya uchunguzi, matokeo yake pia yangelitusaidia Watanzania ambao leo ni wakimbizi wakiwakimbia watu wasiojulikana walejee tujenge Tanzania yetu.

Mungu ibariki Tanzania.

0787766401

733 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!