*Kampuni iliyoghushi, ikafungiwa yaelekezewa ulaji

*Yakaribia kupewa zabuni nono ya Sh bilioni 440

*Ni mkopo wa maji utakaolipwa na Watanzania

NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Wizara ya Maji imebariki kampuni kutoka nchini India isiyo na sifa kwa mujibu wa sheria za ununuzi za Tanzania kuwania zabuni ya ujenzi wa miradi miwili mikubwa ya maji nchini.

Miradi hiyo ni sehemu ya mradi mkubwa wa maji wa miji 28 wenye thamani ya dola milioni 500 za Marekani (Sh trilioni 1.15) ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India.

Mapema mwezi huu uongozi wa Benki ya Exim India ulifika nchini kujiridhisha na mwenendo mzima wa mambo kabla ya kuachia fedha za utekelezaji wa miradi hiyo iliyokwama kuanza.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alilalamika kuchelewa kwa mradi huo; jambo ambalo JAMHURI imebaini limesababishwa na kasoro nyingi za ‘makusudi’ zinazofanywa na wataalamu upande wa Tanzania.

Kampuni ya Larsen and Toubro (L&T) ndiyo inayodaiwa kukosa sifa za kutekeleza zabuni mbili ilizoomba zenye wastani wa dola milioni 192 za Marekani (Sh bilioni 441.6).

Pamoja na L&T, kampuni nyingine kwenye kinyang’anyiro hicho ni Mega Engineering Infrastructure Limited (MEIL), AFCON-Vijeta JV, GVPR Engineering Limited, JMC Projects Limited, Laxmi Civil Engineering Kolhapur Limited, na JWIL Infra Limited. Kampuni zote saba ni za India kama moja ya utekelezaji wa masharti ya mkopo.

Licha ya kukosa sifa kisheria, na ingawa viongozi wa Wizara ya Maji wanajitahidi kujiondoa kwenye lawama, L&T inadaiwa kupigiwa debe huku kampuni nyingine zikilalamika.

Machi 8, 2013 Benki ya Dunia ilitoa taarifa ya kuifungia Kampuni ya L&T kujihusisha na zabuni zake zozote kwa miezi sita kutokana na makosa ya kughushi. Kampuni hiyo ilifanya makosa hayo kwenye ujenzi wa miradi ya afya nchini India.

Kwenye mradi huo wa usambazaji vifaa tiba, L&T ilighushi nyaraka 13 za ufanisi – kazi ikilenga kushinda zabuni ya kusambaza mashine 10 za ultrasound. Uchunguzi wa Benki ya Dunia ulibaini kuwa hati hizo zilikuwa zimeghushiwa.

JAMHURI limewasiliana kwa barua pepe na Ofisi za Benki ya Dunia zilizoko Washington, Marekani na kuthibitishiwa na ofisi hizo kuwa ni kweli L&T iliadhibiwa na kuitumikia adhabu hiyo ya miezi sita.

Sheria za ununuzi za Tanzania kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinaagiza kampuni yoyote ya nje ya nchi – ambayo imekuwa blacklisted kwa makosa ya – Kughushi au Rushwa – kuongezewa adhabu ya miaka 10 zaidi hapa nchini.

Adhabu ya miezi sita ambayo L&T ilianza kuitumikia Machi 7, 2013 ilimalizika Septemba 7, 2013. Ili kukidhi matakwa ya kisheria ya Tanzania kwa mujibu wa kifungu cha 62 (2) (a) cha Sheria ya PPRA inayohusu ‘blacklist’, L&T ilipaswa isiruhusiwe kushiriki mchakato wa zabuni yoyote hapa nchini hadi Machi 8, 2023.

Mkurugenzi wa Ununuzi katika Wizara ya Maji, Christopher Nditi, amezungumza na JAMHURI mara mbili. Mosi, amezungumza kama mkuu wa kitengo hicho, na pili, amezungumza baada ya maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.   

Awali, Nditi alisema sheria ya Tanzania ya kifungo cha miaka 10 inafanya kazi pale tu ambako kampuni inayoomba zabuni ikiwa inatumikia kifungo.

“Kama kampuni imefungiwa, kwa mfano mwaka mmoja huko nje, na ndani ya kipindi hicho ikawa inaomba zabuni nchini mwetu, haiwezi kupewa kwa sababu ina kifungo. Lakini ikiwa imefungiwa na imemaliza kifungo chake hata kama ni cha miezi sita, ikija kwetu kuomba kazi inapatiwa, maana inakuwa haimo kifungoni,” anasema.

Nditi anatetea hoja yake kwa kutoa mfano wa kampuni za hapa nchini zilizofungiwa, lakini baadaye zikamaliza kifungo na sasa zinapewa zabuni. 

“Ni jambo la kawaida kampuni ikimaliza adhabu inapewa zabuni, tunazo kampuni, kwa mfano…(anaitaja),” anasema Nditi kwa namna ambayo kauli yake inapingana na Sheria ya Ununuzi ya PPRA. 

Anasema kinachoendelea ni msuguano wa kampuni hizo kutoka India kutokana na masilahi tu. “Najua wanapita pita sana, hawa hawataki wale wapate, wale hawataki hawa wapate, ni vita.”

 Anasema Kampuni ya L&T ambayo ndiyo inayolalamikiwa zaidi, ilikwisha kutekeleza miradi mingine nchini, kwa hiyo hakuna sababu ya kushangaa kuona ikiomba miradi mingine.

Kauli ya aina hiyo ameirejea alipozungumza na JAMHURI, safari hii baada ya kupewa maelekezo na katibu mkuu. 

Anasema kinachoendelea ni vita miongoni mwa wazabuni, na kwamba Wizara ya Maji kwa nafasi yake haina nguvu zozote za uteuzi kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji miradi inayokusudiwa. 

Anaitetea L&T akirejea sifa ilizomwagiwa na Rais John Magufuli ilipotekeleza kwa mafanikio makubwa mradi wa maji wa Tabora – Nzega – Igunga mwaka jana.

“Hili suala bado liko hatua za ndani, kusudio la nani apewe zabuni bado, maana kuna hatua tatu. Zabuni zilianza na pre-qualification (kwa maelezo ya Nditi kazi hii inafanywa na India pekee).

“Kigezo kimojawapo ni suala la kampuni ambazo ni blacklisted, kwa sasa sisi (Tanzania) hatuna lolote la kufanya, isipokuwa majina yatakayoletwa na India ya kusudio la kutoa zabuni ndiyo yatawekwa hadharani kwa siku saba ili mwenye pingamizi aweke pingamizi. Taratibu za sasa bado ni siri,” anasema. 

Hata hivyo, maelezo yake yanakinzana na kifungu 3.8 (e) 3.12 kinachohusu kampuni zilizo blacklisted kama ilivyoainishwa kwenye maelekezo kwa wazabuni (ITT) wote wanaokusudia kuomba zabuni. 

Aidha, kwenye mchakato wa kampuni zote saba zilizopitishwa (pre-qualified) mchakato wake ulihusisha India na Tanzania, na hivyo kuondoa madai ya kwamba ni India iliyoamua hata L&T isiyokuwa na sifa kisheria iwemo.

Nditi ameulizwa kama ni sahihi kwa wao kukaa kimya na kupeleka India majina ya wazabuni licha ya wengine kukosa sifa, naye amesema kazi yao inakuwa mwishoni kabisa ili kupokea na kufanyia kazi mapingamizi kama yatakuwapo. 

JAMHURI limethibitishiwa kuwa uongozi wa wizara unatambua bayana ukosefu wa sifa wa L&T kwa mujibu wa Sheria za Ununuzi za PPRA, lakini hilo limekuwa likijibiwa kisiasa zaidi.

Hilo linathibitishwa na taarifa za ndani zinazoonyesha kuwa licha ya L&T kuwa na gharama za juu kwenye lot mbili na kuonekana hivyo siku ya ufunguzi wa zabuni, ghafla kwenye usahihishaji ikawa na gharama za chini kuliko kampuni nyingine.

Kwa upande wa L&T kwa wiki mbili sasa wamegoma kujibu maswali waliyopelekewa kwenye barua pepe ya ofisi yao. 

Nditi ana shaka kwa waandishi wa habari wanaofuatilia suala hili, akionyesha dukuduku kwamba huenda wanasukumwa na masilahi binafsi yanayotokana na msuguano wa wazabuni. Lakini kwa upande wa watoa habari wetu, nao wana shaka na waandishi wakidhani kusuasua kuandika taarifa hizo kunasababishwa na kutishwa na wabariki zabuni.

JAMHURI limezungumza na mmoja wa maofisa waandamizi wa PPRA aliyegoma kabisa kuandikwa jina lake gazetini. Amesema: “Sheria za ununuzi ziko wazi, kama kampuni imefungiwa kwa makosa ya kughushi au rushwa itamaliza adhabu yake huko nje, na bado hapa nchini itakabiliwa na kifungo cha miaka 10. Hiyo ndiyo sheria.”

Kuhusu Benki ya Dunia kuiadhibu L&T kwa makosa ya kughushi, ofisa huyo amesema: “Kama walimaliza adhabu huko sawa, lakini kwa sheria zetu miaka 10 haijakamilika, kwa hiyo hawastahili kupewa zabuni wala kuwamo kwenye shortlist ya waombaji zabuni.”

Mkutano wa Waziri Aweso, EXIM

Mwanzoni mwa mwezi huu, Waziri wa Maji, Aweso alikutana na uongozi wa Benki ya Exim India kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 ambao ni moja ya miradi ya maji iliyopangwa kutekelezwa na serikali.

Kikao hicho kilifanyika Dodoma kikilenga kukamilisha taratibu muhimu na kuanza utekelezaji wa mradi huo. 

Uongozi wa Benki ya Exim India ulikuja nchini kwa kazi moja maalumu ya kukutana na serikali ili kuona utekelezaji wa mradi huo unaanza. Mradi huo umekwama licha ya kutakiwa uanze Januari, mwaka huu. Lengo la serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi inafika asilimia 95 mijini, na asilimia 85 vijijini. 

Aweso aliwataka Exim kutoa kibali haraka ili mikataba ya ujenzi wa mradi wa miji 28 isainiwe baada ya kuchelewa kwa muda mrefu.

India ni miongoni mwa washirika wakuu wa sekta ya maji. Walitekeleza mradi wa maji wa Tabora – Igunga – Nzega kwa Sh bilioni 600. Wananchi zaidi ya milioni 1.2 wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Kwenye kikao hicho Aweso alisema Wizara ya Maji si kikwazo cha kukamilika kwa miradi ya maji, ingawa JAMHURI limepata nyaraka kadhaa kutoka India zikihoji ‘uchakachuaji’, hivyo kuwafanya wawe wazito kuidhinisha utoaji fedha. 

Katibu Mkuu Mhandisi Sanga amesema japo mradi huo umechelewa kuanza, kupitia vikao hivyo na uongozi wa Exim kuna matarajio makubwa ya kuanza kwa mradi huo.

Ujumbe wa Benki ya Exim India uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Gaurav Bhandari, ambaye aliahidi kuwa kampuni bora zitatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini. 

By Jamhuri