Wiki iliyopita niliandika makala yaliyokuwa na kichwa “Unahitaji gia ya uvumilivu kumudu biashara”. Nilieleza visa kadhaa vilivyonitokea katika harakati za kibiashara. Mamia ya wasomaji kutoka pande mbalimbali za nchi wameonesha kuguswa na yaliyowahi kunitokea.

Wengi wamenitumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), wameniandikia baruapepe na kunipigia simu wakinipa pole na ushauri mbalimbali. Hata hivyo, ninapenda kuutambua mchango wa msomaji mmoja aliyenitumia SMS. Mchango wake ndiyo msingi wa makala haya ya leo.


Msomaji huyu ni Mchungaji Ency Mwalukasa wa Dar es Salaam. Anasema, “Halo kaka Albert! Nimefurahia sana shuhuda za mapito katika biashara zako. Hata kwenye huduma ya Mungu mapito ni hivyo hivyo.


Nimeguswa nikushirikishe kinga na ulinzi wa mali na fedha zetu: ni kumtolea Mungu fungu la kumi au zaidi.”


“Kwa kufanya hivi inaleta ulinzi na baraka. Malaki 3:8-12. Mungu ameahidi unapotii ni lazima atende. Au asilimia fulani ya fedha na mali zako wape wahitaji utazidishiwa na kupokea ulinzi wa mali na fedha zako. Mtu wa Mungu ni lazima upate mafanikio ya kudumu.”

 

Ninapoendelea na makala haya, ninasukumwa kuweka wazi mambo mawili ili nisilete migongano ya kifikra na kimaslahi. Mosi; ninapenda nitangaze maslahi yangu kiimani. Mimi ni Mkristo niliyezaliwa mara ya pili.


Kwa  hiyo leo ninaandika ulinzi wa biashara zetu kwa mtazamo wa tamaduni na sheria za kibiashara lakini pia kutoka katika Biblia. Pili; si lengo langu kuhubiri katika makala haya; hivyo kama nitarejea mafundisho ya kidini ijulikane kuwa ni nukuu tu za kutusaidia.

 

Kama alivyosema Mchungaji Mwalukasa, ni kweli kuwa mfanyabiashara unatakiwa kutoa fungu la kumi pamoja na sadaka nyingine. Kiimani, utoaji wa sadaka huleta ulinzi wa kiroho katika biashara zako. Ukiacha ulinzi, utoaji wa sadaka huachilia nguvu za uweza wa Kimungu katika fahamu na fikra za mfanyabiashara anayetoa sadaka; kiasi ambacho kunakuwa na mtiririko wa mawazo ya kibiashara (constant flow of business ideas), unakuwa mbunifu na unakuwa na nguvu za kuendelea mbele hata vinapotokea vikwazo.

 

Mimi ni msomi wa masuala ya biashara lakini pia najivunia uzoefu nilionao na ninaoendelea kuupata kwa kufanya biashara kwa vitendo.


Hata hivyo; kule darasani na kwenye vitabu vya biashara kuna jambo ama linafichwa au linapuuzwa. Jambo hili ni nafasi ya Mungu katika kumfanikisha mtu kibiashara.


Watu wanapofundishwa masomo ya biashara hawaambiwi kuwa ukitaka kuwa na mafanikio ya kweli lazima uanze kuimarika kiroho (spiritual mindset). Mimi kamwe sitaacha kuitaja na kufundisha wazi nafasi ya Mungu katika mafanikio ya watu.


Kwa sababu kama tukiwaficha watu kuhusu Mungu tutakuwa tunajenga mafanikio yasiyo ya kudumu. Nimewahi kuandika huko nyuma, “Mtu yeyote anayepata mafanikio ya kifedha ama mali, ikiwa hajaijenga roho yake kwa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu; basi mtu huyo ameuchuma msiba.”


Pengine changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi ni namna gani ya kutoa hizi sadaka.


Mathalani, sadaka ya fungu la kumi ni asilimia kumi ya faida unayoipata katika biashara. Sasa, utajuaje asilimia kumi ya kumtolea Mungu ikiwa hujui unapata faida ya shilingi ngapi kwa wiki, kwa mwezi, au kwa mwaka?

 

Asilimia kubwa ya wajasiriamali na wafanyabiashara nchini wanaendesha biashara kienyeji na kwa kubahatisha. Wengi hawajui ni faida gani anazalisha kwa wiki, mwezi au mwaka na hili linatokana na kutokuwa na utamaduni imara wa kutunza kumbukumbu. Jambo hili ni hatari sana linapokuja suala la kumtolea Mungu sadaka; kwa sababu utajikuta ama unamwibia Mungu, au unamwongezea unapotoa sadaka. Ni heri ukamzidishia Mungu kuliko kumwibia!

 

Binafsi nilijifunza mapema uhusiano uliopo kati ya sadaka na mafanikio ya mtu kibiashara.

Kitu ambacho kilinitesa kwa muda mrefu ilikuwa ni namna ya kujua nimtolee Mungu kiasi gani; kwa sababu biashara nyingi nilikuwa nazifanya kimazoea, kwa kukisia. Nilipokuwa nachanganyikiwa zaidi ni pale inapotokea faida imerudi ‘juu kwa juu’ katika mzunguko na ikaongezea kwenye mtaji.

 

Unapofika muda wa kutoa sadaka nabaki nimechanganyikiwa maana sielewi mtaji ni kiasi gani na faida ni shilingi ngapi kwa muda gani.


Huenda hata mimi nilikuwa mmoja wa waliokuwa wanamwibia Mungu sadaka. Lakini kwa sasa nimepata mwarobaini. Nilikuja kubaini kuwa biashara ili zifanikiwe na ukitaka usigombane na Mungu wako kwa “kumdokolea” sadaka; ni vema kuendesha biashara katika mifumo rasmi.

 

Ndipo nilipoamua kusajili kampuni ambapo biashara zangu zote ninaziendesha kikampuni.

Uzuri wa kufanya biashara katika mifumo rasmi ni kwamba unalazimika kuwa na utaratibu wa uendeshaji biashara, utunzaji wa kimahesabu na mipango ya biashara iliyochambuliwa (business plan).


Pale kwenye kampuni huwa ninapata fedha kwa njia mbili. Mosi; ni kupitia mshahara ninaolipwa kila mwezi. Pili ni gawio la faida inayotokana na mchanganuo wa idadi ya hisa ninazomiliki.

 

Nimetaja habari ya mshahara ninaolipwa kila mwezi. Wengine wanaweza kushangaa kidogo, inakuwaje kampuni ya kwangu halafu tena ninalipwa mshahara? Hapa ndipo wajasiriamali wengi wanapoteleza. Unapokuwa na biashara hata kama iwe ndogo kiasi gani, unatakiwa uwe unajilipa mshahara kiwango maalumu na si kutumia faida ama fedha ya mtaji kadiri unavyojisikia.

 

Sasa linapokuja suala la sadaka sisumbuki. Katika ule mshahara ninaolipwa (ama uite ninaojilipa) kila mwezi, ninatenga fungu la kumi na kumalizana na Mungu. Vile vile inapokuja suala la gawio la faida za hisa, iwe faida itarudi kukuza mtaji ama nitaichukua; ni kwamba kabla ya chochote ninatenga asilimia kumi na ninamalizana na Mungu. Hii nimeona inanisaidia sana, na niwe muwazi; ninauona ulinzi wa Mungu katika biashara na mipango yangu mingi.

 

Ninapoeleza habari za sadaka na mafungu ya kumi mtu anaweza kusema, ‘huyu Sanga mbona analeta habari za kiroho hapa?’ Kwa taarifa yako, ulinzi wa biashara zetu kwa njia ya sadaka unatajwa hata katika sheria na taratibu za biashara.

 

Waanzilishi wa sheria na taratibu zote zinazotumika katika biashara duniani pote ni Waingereza.


Wao katika sheria hizi wanashauri na kulazimisha kuwa biashara inapozalisha faida; ni vema ikarudisha sehemu ya faida yake kwa jamii inayoizunguka. Faida hii ndiyo sadaka. Tena mjasiriamali usisubiri hadi uwe na mamilioni ili kutoa sadaka.

Anza na hiyo faida ndogo unayozalisha hata kama ni shilingi mia tano – toa!

 

Biashara yako inapowasaidia watu kuna mambo mawili yanatokea. Mosi; biashara yako inakaa akilini na mioyoni mwa watu kwa hiyo unaendelea kuwa na wateja waaminifu. Pili; biashara yako inakuwa inaheshimika na jamii unayoisaidia kwa sababu wanajua kuwapo kwa biashara yako ndiyo kupona kwao, hivyo watailinda kwa nguvu zote.

 

Pamoja na juhudi zetu za utaalamu na kanuni za kuzingatia kibiashara, mjasiriamali usisahau kuwa njia bora ya kulinda biashara zako ni wewe pamoja na biashara yako kumtolea Mungu sadaka, kuwasaidia wahitaji na kupeleka sehemu ya faida kuongeza thamani za maisha ya jamii inayokuzunguka.

 

Wajasiriamali tunahitaji ushindi.

tel: 0719 127 901

[email protected]

By Jamhuri