Enzi za Balozi Khamis Kagasheki, kama Waziri wa Maliasili na Utalii, tulishuhudia tani kadhaa za pembe za ndovu zikikamatwa na wahusika wakifikishwa kwenye vyombo vya dola. Moja ya maeneo ambako matukio ya ukamataji yalifanyika ni Mikocheni, Ruvuma, Kimara, Temeke na Zanzibar.

Vyombo vya habari vikiongozwa na Gazati la JAMHURI viliripoti vilivyo matukio haya na kupongeza juhudi za Serikali huku tukitaka hatua zaidi zichukuliwe kunusuru tembo wetu. Tulifanya hivyo, si kwa kuwa tulikuwa tunajipendekeza kwa yeyote. Tulifanya hivyo tukijua kuwa ni wajibu wetu kama raia wema wa nchi hii. Kama ni kununuliwa na majangili ili kuwasaidia kufanikisha uovu wao, basi tungenunuliwa wakati wa Kagasheki. Nani atakubali kumnunua mtu kukwamisha vita ambayo haipo?

Wakati Balozi Kagasheki na watendaji wizarani wanahangaika kupambana na ujangili, Naibu wake, Lazaro Nyalandu, alikuwa hajulikani aliko na nathubutu kusema kuwa  hakuonesha ushirikiano kabisa katika vita hii. Tulichoshuhudia ni kauli za Nyalandu ambazo zilikuwa na mlengo wa kumponda Kagasheki na kuhujumu juhudi zake za kupambana na ujangili. Yeye kipindi hiki akawa yuko bize kuishinikiza TANAPA itoe Sh milioni 560 kufadhili mashindano ya urembo ya Miss East Africa; akawa anamlazimisha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori atoe hati ya matumizi ya wanyamapori kwa kampuni ya Friedkin huko Meatu kwa kuvunja sheria; akawa anasaidia rafiki zake wa Ahsante Tours wakwepe kulipa kodi za serikali na akawa anashinikiza hoteli zilipe tozo sawia (flat rate) bila kujali kuwa hii ingeipotezea TANAPA kiasi cha Sh bilioni 70 kwa mwaka.

Wakati wa Opresheni Tokomeza, Nyalandu alipiga kambi mjini Arusha kwa shughuli zake binafsi bila kujali kuwa Taifa lilikuwa vitani kupambana na ujangili.

Mara tu baada ya Kagasheki kulazimika kujiuzulu, Nyalandu ‘akafufuka’. Wamarekani ambao ni rafiki zake wakaandika kwenye mitandao ya jamii wakimponda Kagasheki kuwa eti alikuwa hana weledi. Tukaambiwa kuwa wapo watu wanaoaminika kuwa majangili jijini Arusha waliandaa karamu kubwa! Wamarekani wakatumia rasilimali zao zikiwamo ndege kuhakikisha kuwa Nyalandu anazunguka nchini kujitangaza na kuulaghai umma kuwa yeye ndiye aliyekuwa anafaa kurithi mikoba ya Kagasheki.

Na kweli, mamlaka za uteuzi zikamuona na zikaridhika kuwa Nyalandu ni jembe! Baada ya kupata madaraka tukajuzwa kuwa majangili wale wale waliosherehekea kujiuzulu Kagasheki wakaangusha karamu nyingine! Wapo waliolinganisha uteuzi wa Nyalandu na hatua ya kumkabidhi fisi bucha ya nyama kulinda. Baada ya uteuzi, Nyalandu akawa kama kichaa aliyekabidhiwa rungu sokoni. Vurugu zake tumeziona! Asiyeona madudu ya Nyalandu, basi ni kipofu kama naye si fisadi papa.

Baada ya kashfa za hovyo na ubadhirifu wa kutisha wa Nyalandu kuibuliwa, hatimaye alifunguka. Kufunguka huku kulitokana na ukweli kwamba wabunge wazalendo walipania kumwajibisha kutokana na kashfa hizi. Aidha, kukataliwa kwa taarifa yake aliyoitoa mbele ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kulimtia kiwewe zaidi. Juhudi za rafiki yake, James Lembeli, kumkwamua kutokana na misimamo ya wana kamati ziligonga mwamba.

Nyalandu ametumia mwezi Oktoba, karibu wote, kuzunguka mikoani, kutumia baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari kukanusha tuhuma lukuki ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake. Nyalandu amekuwa akituhumiwa kwa kukosa maadili ya uongozi ikiwa ni pamoja na ubadhirifu, rushwa, ufisadi na utoro/uzururaji. Tuhuma hizi zimeanza tangu alipoteuliwa kuwa waziri kamili Januari, mwaka huu. Hata hivyo, Nyalandu hakuwahi kukanusha tuhuma hizi zaidi ya kuwakashifu waandishi akiwaita waandishi uchwara na kudai kuwa magazeti yao ni ya kufungia vitumbua. Ajabu, Martin Fletcher wa gazeti la Daily Mail la Uingereza aliyetukana taifa zima na Rais wetu akamzawadia ziara ya kuja nchini kwa kutumia mamilioni ya walipa kodi.

Juhudi za Nyalandu kuzunguka mikoani na kutumia baadhi ya wanasiasa na magazeti, zimemsaidia kwa kiasi fulani. Kama lilivyo lengo la propaganda, wapo aliofanikiwa kuwalaghai na kuwachanganya kiasi cha kumuonea huruma kuwa anasingiziwa na wabaya wake ambao yeye mwenyewe amewataja kuwa wako wizarani kwake na wengine ni wenzake walio kwenye Baraza la Mawaziri na wakubwa wengine serikalini.

Baadhi ya wanasiasa wametumika vibaya kuimarisha propaganda na uongo wa Nyalandu, pengine kwa kukubali kununuliwa kama nyanya zinavyonunuliwa sokoni. Naamini hivyo kwa kuwa mwanasiasa makini hashindwi kuchambua pumba na mchele. Hashindwi kuhoji kulikoni; anajua sheria na taratibu za nchi ambazo Nyalandu amezivunja kwa makusudi. Inapotokea mwanasiasa, tena naibu waziri, kudai kuwa kashfa za Nyalandu ni dalili njema za utendaji wake mzuri, basi hamna jina jingine zuri tunaloweza kumpa zaidi ya kumwita mzigo. Kwanini asiwe mzigo wakati anamsifia mwenzake kuwa ni mtendaji mzuri kwa kigezo cha kashfa wakati yeye hajawahi kuandamwa, lakini bado anang’ang’ania ofisi za umma?

Baada ya ziara hizi, mikutano na matumizi ya wanasiasa na magazeti, Nyalandu aliandaa kile alichokiita ‘Taarifa Rasmi ya Serikali’. Taarifa hiyo haikuwa na sahihi, nembo wala jina na cheo cha afisa yeyote wa Serikali zaidi ya kudaiwa kuwa imetolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Kitengo cha Mawasiliano cha Serikali.  Hata hivyo, taarifa za uhakika ni kwamba watumishi wizarani wameshangaa kuiona taarifa hiyo magazetini asubuhi, huku magazeti yanayombeba Nyalandu yakiripoti kuwa: ‘Tuhuma dhidi ya Nyalandu ni Uzushi”.

Katika Taarifa hiyo, Nyalandu amejibu 10 kati ya tuhuma lukuki zinazomkabili. Sina haja ya kurejea majibu ya Nyalandu kuhusu tuhuma hizo, ambazo JAMHURI Toleo Na. 161 (Novemba 4 – 10, 2014) limehoji majibu hayo kwa ufasaha mkubwa. Hata hivyo, ni juu ya Nyalandu mwenyewe na wale wanaomtetea kujibu hoja juu ya majibu yake ili umma uelewe kama kweli lengo lake lilikuwa kuweka ukweli wa mambo hadharani. Vinginevyo, huu utakuwa ushahidi mujarabu kwamba anachofanya Nyalandu ni propaganda, usanii, ulaghai na utapeli.

Katika majibu ya Nyalandu nimeguswa na jinsi alivyokuwa anahitimisha utetezi wake dhidi ya kila tuhuma inayomkabili ambako alimaliza kwa kibwagizo hiki: “Tuhuma hizi zimetolewa na watu wenye nia ovu  na zimelenga kuchafua jina la Wizara ya Maliasili na Utalii na kumchafua mheshimiwa Waziri Lazaro Nyalandu, kumshushia Heshima, kumdhalilisha kwa umma ili kumpunguzia dhamira, malengo na  kasi ya kupambana na ujangili.”

Kibwagizo hiki ndicho kilichonisukuma kuandika makala hii. Kwanza, ni ulaghai na hadaa kwa Watanzania kudai kuwa tuhuma zinazomkabili Nyalandu ni za wizara nzima, na kwamba si zake binafsi! Kwamba anapoamua kulala Arusha na kuamkia Dar es Salaam asubuhi na kurejea Arusha jioni kwa ndege ya Serikali anafanya kwa niaba ya Wizara; anapotuhumiwa kwa ujangili basi tuhuma hizo ni za wizara na hata zile tuhuma za kutanua na Auntie Ezekiel kule Marekani wakati wenzake wanahaha kupitisha Rasimu ya Katiba Dodoma ni za Wizara!

Ukweli ni kwamba tuhuma zinazomkabili Nyalandu ni zake kama mtu binafsi na wala si za wizara. Kwa mwenye tafakuri jadidi, inatosha kujua kuwa ni kwa nini Nyalandu anageuza kashfa zake binafsi kuwa za wizara na kujifanya anaitetea wizara wakati haijatuhumiwa.

Lakini linalonishangaza zaidi na kuniacha hoi bin taaban ni madai ya Nyalandu kwamba eti kashfa zote dhidi yake zinalenga ‘kumpunguzia dhamira, malengo na kasi ya kupambana na ujangili’. Eti hata ile kashfa yake na Aunty Ezekiel anaihusisha na mapambano dhidi ya ujangili! Ujangili upi anaopambana nao Nyalandu? Huu wa kusimama kwenye runinga na wimbo uliochusha wa “tutawasaka, tutawakamata popote walipo” wakati ndovu wanaendelea kuteketea? Au yale mabango yaliyowekwa JNIA baada ya kulazimisha rafiki yake alipwe mamilioni wakati askari porini hawana buti na dizeli kwa ajili ya doria? Hii kama siyo dhihaka ni nini?

Mimi namfahamu Nyalandu miaka mingi sasa. Tumesoma naye kidato cha tano na sita Ilboru. Alikuwa Rais wangu wa UKWATA (Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania). Mbinu alizotumia kupata nafasi hii na mwenendo wake kama kiongozi wa UKWATA ilikuwa aibu isiyoelezeka. Kwa hiyo, utukutu na ulafi wa Nyalandu havikuanza leo. Anaweza kufanya lolote mradi tu apate anachokitafuta. Utukutu ni kipaji alichokuwa nacho utotoni na bado anakiendeleza! Nyalandu aseme, anapodai kuwa kila linalosemwa leo juu yake linalenga ‘kumpunguzia dhamira, malengo na  kasi ya kupambana na ujangili’  anataka tuamini kuwa yale malalamiko dhidi yake akiwa kiongozi wa UKWATA yalikuwa yana lengo hilo hilo?

Nyalandu amewahi kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara. Tuliona jinsi alivyokuwa tatizo huko. Majuzi, Dk. Cyril Chami amekiri ugumu wa kufanya kazi na Nyalandu. Magazeti yaliwahi pia kuripoti vituko vya Nyalandu. Sikumbuki Nyalandu kudai kwamba alikuwa anaandamwa ili kupunguza dhamira na kasi yake ya kupambana na ujangili. Hoja yake kubwa ilikuwa kwamba mtu na dada yake (Waziri Dk. Chami na Katibu Mkuu Joyce Mapunjo) wanamnyanyasa. Issue kubwa ilitokana na kumdhibiti Nyalandu alipotaka kufanya mambo kinyume cha sheria na taratibu na kujichotea pesa kiujanja ujanja. Fitna zake hatimaye zikamng’oa Dk. Chami.

Itakumbukwa kwamba kwa zaidi ya mara mbili, Nyalandu alidai hadharani kuwa anawafahamu majangili 320 na kuahidi kwamba angewataja wote, hata kwa kuweka majina yao ubaoni. Akataja utaifa wao kuwa wanatoka Uingereza, China na Tanzania. Alipoulizwa bungeni juu ya majangili hawa akadai kuwa hawezi kuwataja kwa kuwa ni watuhumiwa tu! Baadaye akawashangaza watu alipodai kuwa ‘wanajulikana kwa vitendo tu, lakini si kwa majina’. Huyu ni Waziri aliyekabidhiwa dhamana ya Wizara nyeti! Kwa kauli hizi watu wanaaminishwa kuwa eti anapunguziwa dhamira na kasi ya kupambana na ujangili. Waziri ambaye hana kumbukumbu ya kile alichoongea jana!

Katika kipindi kifupi cha Balozi Kagasheki na Mkurugenzi Alexander Songorwa, tuliona kwa macho idadi ya pembe za ndovu zilizokamatwa. Tulishuhudia Profesa Songorwa akitibua mipango ya majangili porini huku akiwa sehemu ya askari wa doria. Wakati wa Operesheni Tokomeza, Nyalandu alijificha. Akajitokeza baada ya kujiuzulu kwa Balozi Kagasheki na kuanza kuusaka uwaziri kwa mbinde.

Baada ya kuukwaa uwaziri, alichofanya ni kuwatimua watumishi waadilifu na kuweka watu ambao anaamini kuwa wangeweza kuiva pamoja kwenye ulaji. Alifanya hivi akisingizia eti aliowatimua wameshindwa vita dhidi ya ujangili, japo majukumu yao yalikuwa hayahusiani na uzuiaji ujangili! Hata hivyo, akawapandisha vyeo watu ambao ndio chanzo kilichosababisha Operesheni Tokomeza kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yao.

Watu hawa amewang’ang’ania hata baada ya kuhamishwa vituo vya kazi hata kufikia kumkejeli Katibu Mkuu Utumishi ambaye kimsingi ndio mamlaka halali ya uteuzi na nidhamu kwa watumishi. Je, hii ndio dhamira na kasi ya Nyalandu kupambana na ujangili?

Mtu makini, badala ya kuamini nyimbo na porojo za Nyalandu, anatakiwa kuhoji kuwa hiyo dhamira na ari ya Nyalandu ya kupambana na ujangili inapimwaje? Inapimwa kwa idadi ya kashfa au kwa nyimbo tamu za ‘tutawasaka, tutawakamata popote walipo’? Au kwa idadi ya safari za Marekani? Au kwa hundi hewa kutoka kwa Michel Allard wa TGTS? Au kwa mabango ya rafiki yake yanayolipiwa milioni 45 uwanja wa JNIA?

Nyalandu anataka kuudanganya umma kuwa wanaoandika kashfa zake wanatumiwa na majangili, na pengine hii ndio hoja yake kudai kuwa lengo ni kumpunguzia dhamira na kasi yake ya kupambana na ujangili. Hili lingekuwa kweli, basi tusingemwacha Kagasheki maana ndiye ameongoza kutimua mipango mingi sana ya majangili pamoja na kukamata shehena kadhaa za pembe za ndovu.  Huu ndio ukweli, hata kama Nyalandu na wapambe wake hawataki kuusikia. Nyalandu kakamata pembe ngapi? Kakamata majangili wangapi? Mbona amekaa kimya hataki kuhoji hatma ya shehena alizokamata Kagasheki? Kama tatizo ni Mahakama au Polisi, mbona hata hatujasikia akilaumu vyombo hivi kumkwamisha? Hapa, tukisema kwamba naye ni mshirika (hasa kwa kuwa naye anatuhumiwa kuwa jangili), atalalama kuwa tunapunguza kasi na ari yake ya kupambana na ujangili?

 

Nyalandu anadai kuwa anapigwa vita wizarani kwake pamoja na wakubwa wenzake serikalini wakiwemo mawaziri na vigogo wengine. Tunataka kuwajua wakubwa hao serikalini wanaompiga vita. Hapa anatutangazia wazi kuwa bosi wake (Rais) ameshindwa kuwawajibisha mawaziri wenzake ambao ni majangili!

Nyalandu anajivunia helikopta iliyotolewa na Howard Buffet ambako kwenye mkataba alijaribu kuchomeka sharti la hovyo kumlazimisha Rais wetu juu ya yeye Nyalandu kuendelea kuwa Waziri wa Maliasili. Swali ni je, tunahitaji helikopta kuwakamata majangili 320 Nyalandu anaowafahamu tayari? Tunahitaji helikopta kuwakamata mawaziri ambao Nyalandu anadai wanamkwamisha?

Nyalandu anadanganya kuwa amelipia silaha zilizokwama bandarini muda wa miaka miwili wakati uamuzi wa kulipa aliutoa Kagasheki baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kugoma kusamehe kodi. Eti kaajiri wafanyakazi 430 na kaanzisha Mamlaka ya Wanyamapori. Madai haya ni ya kihuni na anataka kuhadaa umma kuwa yeye ndiye mwenye akili kuliko Mtanzania mwingine. Yeye ndiye utumishi? Anawalipa kwa pesa zake? Hatua za kuanzisha mamlaka zilianza mwaka 2011 na sasa ndio zimekamilika. Atadai vipi kaianzisha Mamlaka?

Mwenye akili timamu ameelewa; mnaomtetea Nyalandu ruksa, lakini mimi nitakuwa mtu wa mwisho na kamwe sitakuja kumuona Nyalandu kama shujaa. Ole wenu wanasiasa na waandishi mnaoendekeza njaa na kuwaumiza Watanzania wanyonge kwa kutetea ufisadi huu wa Nyalandu! Kamwe ufisadi huu hautafutika.

Mwisho, niwakumbushe rafiki zangu, waheshimiwa Lembeli na Peter Msigwa kuwa bado hawajachelewa. Nimefurahishwa na mchango wao bungeni juu ya suala la ESCROW. Wanajua wazi kashfa za Nyalandu; wanajua juu ya matumizi mabaya ya Leseni ya Rais – na kwa bahati nzuri wao kama viongozi na watch dogs katika sekta wanajua sheria inasemaje. Tunataka kusikia wakihoji vitendo hivi vya Nyalandu.

Vinginevyo, wajue kuwa nao ni mafisadi na kwamba uchangiaji wao ni unafiki; na kwamba nao wanafaidika na ufisadi wa Nyalandu kama ambavyo imekuwa ikiandikwa. Nililo na hakika nalo ni kwamba hata kama Nyalandu ataendelea kukumbatiwa licha ya kashfa nyingi dhidi yake, basi kama si leo, kesho historia itatuweka huru.

1094 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!