Ofisa KCMC atuhumiwa kuajiri Warundi

Ofisa Utumishi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Kilimanjaro, inayomilikiwa na Shirika la Msamaria Mwema (GSF), Alpha Chabakanga (57), anatuhumiwa kuwaajiri raia wanne wa Burundi katika shughuli za ujenzi wa nyumba yake.

Pia anatuhumiwa kuvunja haki za binadamu kwa kumtumikisha kwenye shughuli za uyaya, mtoto mwenye umri wa miaka 15 ambaye pia ni raia wa Burundi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa raia hao wa kigeni ni miongoni mwa mamia ya Warundi wanaoikimbia nchi yao kutokana na machafuko ya kisiasa. Wageni hao walikamatwa Januari 20, mwaka huu eneo la Shah Tours mjini Moshi.

Waliotiwa mbaroni ni Ndaishimie Baranizigie (22), Daudi Ndai (30), Fredy Bukuru (24) na Nabalushima Njanini ambaye ni yaya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kilimanjaro, (ACP) Ramadhan Mungi, Warundi hao walikamatwa nyumbani kwa Chabakanga. Kukamatwa kwao kulitokana na taarifa za siri kutoka kwa raia wema, na kwamba wamekabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro.

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Mwanguku Embrossy, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema chanzo cha kukamatwa kwao ni ugomvi baina yao na mwenyeji wao, Chabakanga.

Amedai kwamba Chabakanga aliwafungulia Warundi hao malalamiko katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi baada ya kutofautiana.

“Sisi tunafurahia ugomvi wao maana umetupa fursa ya kuwakamata na kama si ugomvi wao tusingewakamata kwa sababu kuna watu wengi wanaishi na raia wa kigeni bila kufuata taratibu za Uhamiaji,” amesema.

Maeneo yanayotajwa kuwa na raia wengi wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi kinyemela ni kwenye shule binafsi za msingi na sekondari hasa Himo na Njia Panda ambako kuna shule nyingi za mchepuo wa Kiingereza.

Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wapo watumishi wa Uhamiaji wasio waaminifu ambao huwapa taarifa waajiri wa wageni hao na kuwaficha.

Idara ya Uhamiaji imesema Warundi hao wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuishi na kufanya kazi hapa nchini bila vibali kwa mujibu wa sheria.

Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Henry Ng’webeya, amedai kuwa Chabakanga anakabiliwa na mashitaka matatu.

Shauri hilo lilifikishwa mbele ya Hakimu Pamela Meena wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro. Chabakanga alikana mashitaka na aliachiwa kwa dhamana. Masharti ya dhamana yalikuwa kuwa na mdhamini mmoja na ambaye atasaini hati ya dhamana ya Sh 1,000,000.

Kwa mujibu wa hati mashitaka ambayo nakala yake gazeti hili inayo, Chabakanga ameshitakiwa chini ya kifungu cha 16(1) na 31(1) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji sura ya 54 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2015 kinachokataza kuajiri mtu asiye raia wa Tanzania bila kibali.

Shitaka la pili na la tatu liliwahusu raia hao wa Burundi ambako katika shitaka la kwanza ni la washitakiwa hao kukamatwa wakiwa hawana pasi za kusafiria wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Katika shitaka la tatu, wanashitakiwa kwa kujihusisha na ujenzi wa nyumba ya Chabakanga bila kuwa na kibali kinachowaruhusu kufanya kazi hiyo.

Washitakiwa Baranizigie na Ndai walikiri kosa la kukutwa katika ardhi ya Tanzania bila vibali, lakini wakakana shitaka la tatu. Walipelekwa mahabusu ya Gereza la Mkoa la Karanga.

Upande wa mashitaka umeiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 8, mwaka huu.