Mtendaji wa Kijiji cha Vuchama Ndambwe, Jeremiah Daniel, amepigwa na kujeruhiwa kwa mkuki akiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali na mkazi wa kijiji hicho anayetambulika kwa jina la Rashid Juma.

Tukio hilo limetokea wiki iliyopita nyumbani kwa mtuhumiwa wakati mtendaji huyo akiwa ameambatana na watu sita, alipokwenda kumtoza faini ya kutohudhuria katika ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho. 

Wanakijiji walikubaliana awali kuwa kila Jumatatu watu wote wanapaswa kushiriki katika kazi za ujenzi wa zanahati hiyo na atakayeshindwa kufanya hivyo atapaswa kulipa faini.

“Hapa tumeweka sheria ndogo kwamba iwapo mtu hatafika katika shughuli za maendeleo atachukuliwa hatua ambazo ni ama alipe faini ya shilingi elfu kumi au kutoa kitu chochote chenye thamani ya pesa hiyo. Siku hiyo kulikuwa kuna zoezi la ujenzi wa zahanati ya kijiji, kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa hawajahudhuria, tuliamua kwenda ‘kumpambua’ (kumtoza faini au kuchukua kitu) ndipo yaliyonikuta haya,” anasema mtendaji huyo.

Anasema baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa walimkuta binti yake anayesoma kidato cha pili na kujitambulisha kwake ambapo binti huyo alikiri kuwafahamu na kusema kuwa baba yake hakuwapo nyumbani wakati huo.

“Kwa kuwa alikiri kutufahamu, tulimweleza nia yetu ya kuwa pale, kwamba baba yake hajafika zahanati, hivyo anatakiwa kulipa faini, na kwa kuwa hayupo tunachukua kitu chenye thamani ya hiyo fedha, tukaamua kuchukua kuku, wakati tunataka kumkamata, kumbe baba yake alikuwa ndani, akatoka na mkuki na kuanza kunishambulia huku wenzangu wakikimbia,” anasimulia Daniel na kuongeza:

“Niliona nikikimbia anaweza kunidhuru zaidi kwani anaweza kunirushia kitu chochote kwa nyuma, kwa hiyo nilisimama, alivyofika alitaka kunipiga kichwani nikawa ninajizuia kwa mkono, ndipo akauumiza, kwani mfupa wa mkono umedhurika vibaya. Kwa mujibu wa picha ya X-ray kuna mfupa umemeguka.”

Anasema wakati anamshambulia mtuhumiwa alikuwa akisema: “Mnaacha kutuletea vitambulisho vya NIDA badala yake mnakuja kutusumbua na kazi zenu.”

Mtendaji huyo anasema alipata fomu namba 3 katika Kituo cha Polisi Mwanga na kupatiwa matibabu ya awali katika Kituo cha Afya Mwerange na hatimaye akapatiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Wilaya Usangi ambapo alipatiwa matibabu na kuruhusiwa.

By Jamhuri