Staika mkongwe wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Amissi Tambwe ameanza kuingiwa na hofu ya kumuona Emmanuel Okwi wa Simba akivunja rekodi zake katika Ligi Kuu Bara huku akisema jamaa ni balaa.

Tambwe, raia wa Burundi, ana rekodi nyingi katika ligi kuu ikiwemo ile ya ufungaji bora mara mbili katika msimu wa 2013/14 akifunga mabao 19 na msimu wa 2015/16 alipofunga mabao 21.

Tambwe amekumbwa na hofu hiyo baada ya kumshuhudia Okwi akivunja rekodi ya msimu wa 2014/15 ya Simon Msuva ambaye alikuwa mfungaji bora akifunga mabao 17.

Juzi Jumatano, Okwi alifikisha mabao 18 akibakisha bao moja kumfikia Tambwe ambaye msimu wa 2013/14 alifunga mabao 19 wakati huo akiichezea Simba.

Okwi anahitaji bao moja tu ili aweze kuivunja rekodi hiyo ya Tambwe ambaye msimu huu hana bao hata moja katika ligi kuu akiwa amecheza mechi mbili tu za ligi hiyo, muda mwingi yupo nje ya uwanja akiuguza jeraha la goti.

Tambwe amesema kasi aliyonayo Okwi kwa sasa siyo ya mchezo na kama ataendelea hivyo basi anaweza kuzivunja rekodi zake zote za msimu wa 2013/14 na 2015/16.

“Nampongeza kwa kasi yake hiyo pia kwa kuvunja rekodi ya Msuva na sasa ameanza kuzinyemelea za kwangu ambapo amebakiza bao moja tu aivunje ile ya mabao 19 ambayo niliiweka msimu wa 2013/14.

“Anaweza kuivunja ile ya msimu wa 2015/16 ya mabao 21 kama ataendelea na kasi hiyo kwani mechi bado zipo nyingi, kwa hiyo ngoja tuone itakavyokuwa,” alisema Tambwe.

Kwa upande wake, Okwi alisema: “Kwa sasa siangalii ishu ya kuvunja rekodi ya mtu yeyote yule bali ninachoangalia ni kuhakikisha naisaidia timu yangu kushinda katika mechi zake zote ili tuwe mabingwa.”

 

By Jamhuri