Wiki iliyopita Bunge limetoa maelekezo kwa Kamati ya Maliasili na Utalii kuchunguzia utekelezaji na mwenendo wa Operesheni Tokomeza. Operesheni hii imeendeshwa kwa makusudi kudhibiti majangili waliokuwa wakiua tembo kwa kasi ya ajabu na kutishia uwepo wa tembo nchini. Wabunge wamelalamika kuwa askari walioendesha operesheni hii walikosa uaminifu.

Hata sisi tumeyapata malalamiko haya. Yametokea Tabora, Mara, Kagera, Arusha na sehemu nyingi za nchi hii. Baadhi ya askari wasio waaminifu wametumia fursa hiyo kuwanyanyasa wananchi, kuua na kupora mali zao. Kila aliyekuwa na chuki dhidi ya mtu mwenye ukwasi, basi operesheni hii na ile ya Kimbunga alizitumia kunyanyasa watu.

Tumeripoti matukio ya watu kuawa, ng’ombe kupigwa risasi au kuporwa, askari kupora mbao na milango kwenye nyumba za watu waliowatuhumu ama kuwa majangili au kuwa wahamiaji haramu. Sisi tunasema hali hii imetusikitisha. Imetusikitisha kwa maana lengo la Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, halikuwa hilo.

Viongozi hawa wakuu walilenga kuwatia mbaroni majangili wenye uchu wa utajiri bila kujali vyeo vyao, madaraka au nasaba zao. Na kweli katika msako huu, Gazeti JAMHURI toleo Na. 106 limechapisha orodha ya majangili 20. Katika orodha hii wamo maafisa wanyamapori. Askari wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili, wengi wao wamekamatwa katika operesheni hii.

Imethibitika kuwa askari hawa wengi wao ni majangili namba moja. Maafisa wanyamapori wengi wamefikishwa mahakamani. Wamekutwa na pembe za ndovu ama ofisini au nyumbani kwao. Imebainika pia kuwa hata bunduki za ofisi zimekuwa zikilazwa nyumbani kwa askari wa wanyamapori kinyume cha sheria na taratibu za kazi.

Tunazo taarifa na tulizichapisha kuwa baadhi ya wanasiasa wanashiriki ujangili. Wabunge wawili wamehojiwa kwa ujangili. Ni kwa mantiki hiyo, tunapenda kumuasa Spika wa Bunge, Anne Makinda, na Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Utalii, James Lembeli, kuwa macho wanapofanya uchunguzi. Kipindi chote cha operesheni viongozi wa wizara walikuwa hawalali.

Mawaziri walikuwa wanampigia simu Kagasheki kama mvua. Walipokamatwa, hasa wafanyabiashara wenye ukwasi usioelezeka katika mikoa mbalimbali, simu zilizidi kumiminika. Ukali wa wabunge unapaswa kuchunguzwa kwa kina iwapo unatokana na uchungu wa kweli juu ya wananchi kuumizwa au wamejipanga kutetea majangili wanaowapa michango wakati wa uchaguzi.

Tunasisitiza kuwa ikiwa kuna askari aliyetenda kinyume na maelekezo halali ya operesheni hizo, basi huyo ashughulikiwe bila huruma, ila tunapata shida sehemu moja tu. Wapo askari waliokamatwa kwa mfano wilayani Songea, ambao wananchi wengi wana ushuhuda kuwa wanashiriki ujangili, lakini baada ya muda wakaachiwa. Hii inatoa picha gani?

Wapo watu waliotajwa bungeni, akiwamo huyo aliyetajwa na Mbunge Ester Bulaya kuwa aliwekwa ndani, akafanya mbinu akatoka kwa msamaha wa Rais. Rais Kikwete akaagiza awekwe tena ndani, bado zikafanywa mbinu akatolewa. Unaweza kujiuliza watu wa namna hii nguvu wanaipata wapi? Huu ni ujumbe kuwa Kagasheki amepata wakati mgumu na ameonesha ujasiri wa hali ya juu kuendesha operesheni hii.

Tunasisitiza kuwa kwa maslahi ya Taifa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza ziendelee, ila askari watakaozitumia kwa manufaa binafsi au kunyanyasa wananchi washughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Tusipofanya hivyo tukasikiliza mihemuko wa wabunge, ujambazi utashamiri na tembo watateketea wote hapa nchini. Spika Makinda kuwa makini katika hili, usiruhusu fedha zikayumbisha nchi.


By Jamhuri