Klabu ya Manchester United ya Uingereza iko mbioni kumuuza mchezaji wake Henrikh Mkhitaryan ili kupata pesa za kumsajili kiungo wa klabu ya Arsenal, Mjerumani Mesut Ozil.

Mchezaji huyo anatarajiwa kumaliza mkataba wake ndani ya klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu hali inayoilazimu klabu yake kumuuza katika dirisha dogo la mwezi Januari au aondoke bure mwishoni mwa msimu.

Katika siku za karibuni mchezaji huyo ameingia katika mkwaruzano na klabu yake baada ya kugoma kusain mkataba mpya akishinikiza kuongezewa mshahara.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ozil upande wa Henrik Mkhitaryan  ndani ya klabu ya Manchester United siyo nzuri kiasi cha kujikuta akiwekwa nje katika michezo saba iliyopita.

Mchezsaji huyo amejikuta katika wakati mgumu baada ya kocha wake Jose Mourinho kudai kuwa mchezaji huyo ameshuka kiwango kiasi cha kumuondoa miongoni mwa wachezaji wanaoanza siku za karibuni.

Kutokana na hali hiyo tayari kocha Mourinho  amenza kumuamini Jesse Lingard pamoja na Juan Mata katika nafasi ya namba 10 huku Mkhitaryan akiendelea kusota benchi.

Kutokana na kutokuelewa hatima yake ndani ya klabu hiyo tayari mchezaji huyo ameomba kukutana na meneja wake kutaka kujua hatima ya maisha yake ya kisoka ndani ya klabu hiyo.

Taarifa toka Old Traford zinadai Mourinho ameamua kuanzisha jitihada za kumsajili Ozil baada ya kuona Mkhitaryan akishindwa kufikia malengo ya klabu katika siku za hivi karibuni.

Hali ya Ozil ndani ya klabu ya Arsenal imekuwa haieleweki kiasi cha mchezaji huyo kukataa kubaki Gunners pamoja na kupewa dili jipya lenye mshahara wa pauni 235,000 kwa wiki yeye anataka  pauni 300,000 kwa wiki.

United wanaamini wana nguvu ya pesa ya kuweza kumlipa Ozil kile kiasi chochote cha fedha anacho hitaji na kwa sasa kinachosubiriwa ni klabu kutuma ofa rasmi kwenda Arsenal.

Kutokana na jitihada zinazofanywa na klabu ya Man United kumpata Ozil kuna uwezekano mkubwa kwa mchezaji huyo kupishana na Mkhitaryan ndani ya klabu hiyo ya Old Traford siku za karibuni.

By Jamhuri