Kuna mambo mengine mtu unaweza kupata sifa hata kama huna ujuzi nayo. Wakati wa mvutano wa Chama cha Wamiliki wa Malori na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, nilisema Waziri huyo hatafika mbali kwa uamuzi wake wa kusimamia sheria.

Siku moja baadaye, kama “nilivyotabiri”, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya kile kilichotabiriwa. Akatengua msimamo wa Dk. Magufuli ambao kimsingi ni msimamo wa kusimamia sheria za nchi. Ametupa sifa kwa kutufanya tuonekane tunauweza utabiri!

 

Baada ya hapo nikawa miongoni mwa wale tuliomshauri Dk. Magufuli ajiuzulu! Nikarejea namna Pinda alivyomsulubu jimboni kwake Chato kwa kumzuia kuendelea na bomoabomoa kwa waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara. Nikakumbuka namna Pinda alivyojaribu kumzuia asiongeze nauli kwenye vivuko; na sasa hili la malori.

 

Nikajaribu kutafakari agizo la Pinda kwa Dk. Magufuli na jingine baya la kuua uhifadhi alilolitoa dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, wiki mbili hivi zilizopita. Waziri huyo wa Maliasili, kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu, na kwa kurejea mapendekezo ya tume zaidi ya tatu kuhusu Loliondo, alitenga eneo kwa ajili ya ushoroba (mapitio) ya wanyamapori na jingine akawapa wananchi. Pinda akaona uamuzi huo wa Kagasheki haufai! Hapo siasa ikawa imeshinda utaalamu!

 

Nilipounganisha hilo la Kagasheki na hili la Dk. Magufuli, ndipo nilipofikia hitimisho la kuona kuwa mawaziri hao wawili hawana sababu za kujiuzulu, isipokuwa anayestahili kuachia madaraka ni Waziri Mkuu mwenyewe.

 

Waziri Mkuu amekuwa akiwavunja moyo walio chini yake. Wananchi tunahoji, hivi wakubwa hawa kabla ya kuamua mambo huwa wanaketi pamoja? Lakini, kuna sababu gani ya kumshirikisha Waziri Mkuu katika jambo ambalo linabainishwa kwa Sheria na kwa Kanuni?

 

Dk. Magufuli, kama walivyo binadamu wengine, ana upungufu wake. Huo lazima usemwe. Nilishampinga sana kwenye suala la uuzaji nyumba za Serikali. Na kwa kweli nitaendelea kumpinga kwa hilo. Lakini Waswahili husema “mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni”. Katika hili la malori, nilitangaza tangu mapema kabisa kumuunga mkono. Namuunga mkono kwa sababu kama ni ubaya si Magufuli, bali ni wa sheria iliyopo. Kwanini tumhukumu kiongozi anayesimamia sheria hata kama ni mbaya? Wanaomuona mbaya kwanini wasiende bungeni kuifuta au kuirekebisha? Aliapa kulinda au kuvunja sheria?

 

Dk. Magufuli alipozungumza na waandishi wa habari juu ya kuondolewa kwa nafuu ya kutolipa tozo kwa uzito wa magari unaozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria, aliwapa nakala za sheria na kanuni wanahabari hao.

 

Baada ya mvutano kati yake na wamiliki wa malori, nimelazimika kuzisoma sheria hizo ambazo ni Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973; Sheria ya Usalama Barabarani Sura Na. 168 ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001. Wanahabari wanazo sheria hizi.

 

Sheria hizo na kanuni zake ZILIFUTWA na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, katika barua yake ya Julai 19, 2006. Yeye ndiye aliyeamuru wenye malori na wasafirishaji wengine wasilipe faini kwa kuzidisha uzito huo wa asilimia tano! Hapa ikumbukwe kuwa Tanzania imeruhusu mizigo yenye uzito wa tani 56 isafirishwe katika barabara zake. Nimeingia kwenye mtandao na kuona kuwa hata huko Ulaya, uzito wa juu kabisa unaoruhusiwa ni tani 44. Hapa sisi ni tani 56, lakini ukiongeza na hizo asilimia tano, maana yake ni karibu tani 60! Huu ni mzaha.

 

Waziri Mkuu Pinda ni mwanasheria. Napata shida kuamini kuwa kwa weledi wake kama mwanasheria, anashindwa kutambua kuwa Waziri hana mamlaka ya kufuta kwa “waraka au mwongozo” sheria iliyotungwa na Bunge. Alichofanya Mramba ni kuvunja sheria iliyo wazi kabisa. Mramba hakuwa na kamwe hatakuwa na mamlaka ya kufuta sheria kwa kutoa mwongozo!

 

Kosa hilo hilo la Mramba limerejewa tena na Waziri Mkuu Pinda. Mramba tunaweza kumsamehe kwa sababu, kwanza yeye si mwanasheria, na pili inawezekana alishauriwa na wanasheria wasiotaka kusoma sheria. Pinda ni mwanasheria, anashindwaje kuliona hili?

Serikali inaendeshwa kwa taratibu zinazotawaliwa na sheria. Bila shaka linapokuja jambo kama hili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anapaswa kusaidia kupatikana kwa suluhu. Je, ina maana hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshindwa kumshauri Waziri Mkuu kwamba Mramba mwongozo wake ulikuwa batili? Je, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishindwa kumweleza Waziri Mkuu kwamba sheria haibadilishwi kwa barua ya waziri, bali kwa kuandaa amendment na kuiwasilisha bungeni?

 

Waziri Mkuu amesema itaundwa tume kwa ajili ya kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Kwanini ahangaike na tume wakati mahali pekee pa kumaliza kadhia hii ni bungeni kwa kupeleka marekebisho ya sheria? Hizi tume ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

 

Juzi amejitokeza Azim Dewji, na kudai kwamba Serikali imepata hasara ya Sh bilioni 20 kwa mgomo bandia walioufanya. Hizi ni porojo. Dewji amepata nguvu za kumsema Magufuli kwa sababu bado anaugulia maumivu ya kufuata sheria aliyoyapata baada ya Magufuli kuzuia maboti yake mabovu kusafirishwa kwa barabara hadi Mwanza. Maboti yenyewe yalikuwa mabovu na sasa yanafaa kuwa vyuma chakavu. Huhitaji akili za ziada kutambua kuwa huyu hata kuwa mbele kumsema Magufuli kunatokana na maumivu hayo ya kuzuiwa kwa maboti yake mabovu!

 

Pili, watu kama kina Hans Pope kushangilia malori yabebe uzito wa tani zaidi ya 56 si jambo la ajabu. Huyu anataka barabara zife. Wengine walidiriki kumuua Rais wa nchi, bila shaka wao kuziua barabara si kazi ya kuwatoa jasho. Hili nalo halihitaji kusumbua vichwa.

 

Mfanyabiashara Pope anatamba kuwa mwaka jana alilipa serikalini Sh milioni 200 kutokana na biashara yake ya malori! Sawa, Sh milioni 200 ni kitu gani kwa malori yanayoua barabara? Kilometa moja ya barabara ya lami inajengwa kwa wastani wa Sh milioni 700 hadi Sh milioni 1,000. Kwa hiyo Pope anataka aharibu barabara kwa sababu analipa fedha ambazo hazitoshi kujenga hata robo kilometa.

 

Waziri Mkuu Pinda anatambua kuwa wenye malori hawa ni matajiri. Wana fedha nyingi, na kwa sababu hiyo wana ushawishi wa hali ya juu. Anatambua kuwa wanasiasa wengi wana malori, na kwa sababu hiyo wasingependa kuona reli zikifanya kazi.

 

Wala hili si la kustaajabisha kwa sababu unaona hata Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, badala ya kusaidia kuboresha reli na bandari ili zitumiwe kusafirisha mizigo mizito, amekuwa sehemu ya wanaolalamikia mgomo wa malori kwamba umesababisha mlundikano bandarini! Dk. Magufuli ambacho hakijui ni kwamba ameamua kupambana na wenye fedha, na kwa bahati mbaya umma nao umeshindwa kupewa elimu stahiki juu ya ulaghai huu wa kina Dewji na Pope.

 

Wakati wakubwa hawa wakiendeleza mapambano, zipo kampuni ambazo nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba kwa miaka mingi malori na mabasi yao hayazidishi uzito. Kampuni hizo ni kama Dar Express, Cargo Star, Hood, Coca Cola, BM Bus, Bakhresa, TBL, Golden Coach, Kanji Lalji, Tawaqal, Condolidated Logistic, Ramada Transport na BP ambayo kwa sasa ni Puma.

 

Kwanini hawa wafaulu, lakini kina Dewji washindwe? Hawa hawa watetezi wa uzito bila shaka ndiyo wanaosali usiku na mchana reli zisifanye kazi. Leo ni kwa Dk. Magufuli, lakini ikitokea Dk. Mwakyembe akaanza kujenga reli, na yeye watamshughulikia tu! Hawa wapo kimaslahi zaidi.

 

Hizi barabara si mali za wafanyabiashara wamiliki wa malori na mabasi. Barabara za Tanzania zinajengwa kwa kodi za wananchi wote. Mikopo ya barabara hizi italipwa hadi na vitukuu vyetu. Kama hivyo ndivyo, hatuna sababu ya kushabikia wanaozidisha uzito.

 

Lakini kubwa zaidi ni kwamba nchi inaongozwa kwa sheria. Bila kuheshimu sheria, nchi hii itakuwa kituko. Hali inakuwa mbaya zaidi pale Waziri Mkuu, kiongozi mkubwa kabisa, anapoamua kubariki barua ya waziri wa zamani ifute au ipindishe sheria zilizotungwa na Bunge. Kuna maana gani ya kuwa na Bunge? Kuna maana gani ya mawaziri, akiwamo Waziri Mkuu kula viapo vya utii wa sheria za nchi?

 

Kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Usalama Barabarani, inasema hivi kwa kimombo, “Any Person aggrieved by the decision  of the authorized officer or the Road Authority refusing to grant a weighbridge report or any permit required to be granted under these Regulations may appeal against that decision to the Minister.

(2) Where a person is not satisfied by the decision of the Minister he may appeal to the High Court and the provisions of the Criminal procedure Act, shall apply.”

Hapa kinachoelezwa ni kwamba kama mtu hakuridhishwa na uamuzi wa Waziri, anachopaswa kufanya ni kwenda kufungua kesi katika Mahakama Kuu.

 

Wenye malori wanaijua kanuni hii, na Waziri Mkuu anaijua pia. Wanatambua kuwa wakienda mahakamani watashindwa. Njia ya mkato waliyoamua kuitumia ni ya kwenda kwa Waziri Mkuu ambaye hatajwi kwenye sheria hii. Kwa hiyo kilichofanywa na Pinda ni ubabe tu kwa sababu ni Waziri Mkuu. Amefanya hivyo akijua Magufuli hawezi kumpinga. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka. Huu ndiyo ukweli ambao wanahabari hawataki kuusema, na jamii imefungwa isiujue.

 

Sioni ni kwa namna gani Pinda ataumaliza mgogoro huu kwa staili aliyoamua kuitumia ya kuvunja sheria. Sioni ni kwanini Mwanasheria Mkuu wa Serikali asiwe sehemu ya lawama kwa kushindwa kumwongoza au kumshauri Waziri Mkuu kwenye jambo hili lisilohitaji mhitimu wa cheti cha sheria.

 

Moja ya matatizo makubwa katika nchi yetu ni viongozi kukosa misimamo. Viongozi kama Mheshimiwa Pinda wapo radhi kuvunja sheria alimradi tu waridhishe kundi la watu wachache. Ndiyo maana narejea tena na tena kwamba hata hiyo Katiba tunayoililia ikija, kwa uongozi wa aina hii ya kina Mheshimiwa Pinda, haitasaidia chochote.

 

Itakuwa nzuri, lakini uamuzi utatolewa kwa utashi wa kisiasa na hofu zinazojengwa na watu, hasa matajiri. Katika hili, anayestahili kujiuzulu ni Waziri Mkuu kwa kubariki uvunjifu wa wazi wa sheria za nchi.

1472 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!