NA MWANDISHI WETU

SHINYANGA

Shinikizo linawekwa kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bukombe mkoani Shinyanga kumchukulia hatua za kisheria mwalimu anayetuhumiwa kumuua mkewe ambaye pia ni mwalimu, kisha ‘kuigiza’ kuwa amejinyonga.

Katika kibali cha mazishi, inathibitishwa kuwa chanzo cha kifo cha Mwalimu Georgina Kizanye, ni kutokwa damu nyingi baada ya bandama kupasuka.

Kwa upande mwingine, taarifa ya kitabibu ambayo Polisi wamegoma kuitoa kwa ndugu wa marehemu inathibitisha kuwa Kizanye alipigwa ubavuni na kitu kizito, akapasuliwa bandama na hatimaye alivuja damu nyingi tumboni zilizosababisha afariki dunia. Miongoni mwa watuhumiwa ni mumewe, Mwalimu Christian Msonde.  

Lakini Polisi kwa upande wao wamefungua jalada la uchunguzi BKE/RB/1262/2021 kuonyesha kuwa kifo cha Kizanye kilichotokea Agosti 30, mwaka huu kilisababishwa na yeye mwenyewe kujinyonga kwa khanga bafuni nyumbani kwake.

Tofauti na matukio mengine ya aina hiyo, hadi mwishoni mwa wiki iliyopita Polisi walikuwa hawajamkamata mtuhumiwa, huku Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Bukombe, Mokiri Mkenye, akidai kwamba hakuna tukio la aina hiyo wilayani kwake.

Danadana juu ya tukio hilo zimewafanya ndugu wa marehemu Kizanye walalamike hadi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya (DC) ya Bukombe, Said Nkumba. DC huyo amewatuliza kwa kusema kuwa haki itatendeka.

Mmoja wa ndugu aliyezungumza na JAMHURI anasema: “Ilikuwa ni siku ya Agosti 30, 2021 saa nne usiku ndipo tulipokea taarifa ya kifo cha dada yetu kutoka kwa askari polisi aliyedai kuwa ndugu yetu amejinyonga ndani ya bafu au choo cha ndani ya chumba chao – mke na mume.

“Polisi huyo alikuwa amejionea mwenyewe kwamba marehemu Georgina Kizanye hakujinyonga, bali ameuawa na mwili wake kupelekwa bafuni kwake na baadaye kufungwa kitenge shingoni na kuunganishwa kwenye nondo ya chini kati ya nondo tatu zilizopo kwenye ki-dirisha kidogo cha urefu wa kama futi 5.5 hivi kutoka sakafuni katika master bedroom ya nyumba waliyojenga na mumewe. Wote waliishi pamoja.

“Kitenge hicho kilifungwa kwa namna ya kuzuia mwili usianguke chini ili ubakie kama mtu aliyepiga magoti akielekea ukuta wa bafu. Siku iliyofuata, yaani Agosti 31 kaka wa mume wa marehemu (shemeji yake marehemu), alimpigia simu kaka yangu na kudai wanataka kuzika. Hapo ndipo tulijua lazima kuna kitu wanataka kuficha.

“Tulitafuta namba ya simu ya Ofisa Elimu na akatuhakikishia kuwa hawatazika hadi tufike. Tulianza safari siku hiyo hiyo na kufika Ushirombo saa tatu usiku wa Septemba Mosi. Wapo waliotoka Dar es Salaam na wengine walitoka Kigoma, na wengine Sumbawanga.

“Septemba 2 tulifika eneo la tukio tukisindikizwa na polisi. Tuliona eneo na kulipiga picha. Hata kabla ya kuona picha za tukio tuliridhika kuwa hata ule mpango wa wao kutaka wazike haraka haraka ulikuwa ni wa kuficha ukweli wa chanzo halisi cha mauaji ya ndugu yetu.

“Baadaye askari walitupeleka ofisini kwao na kutuonyesha picha walizopiga eneo la tukio. Tukauona mwili ulivyokuwa, na namna ulivyokuwa ‘umepiga magoti’ na kuonekana kushikiliwa na kitenge ili usianguke! Askari wale walitupa ushirikiano stahiki. Walituonyesha picha zote na kiji-karatasi ikisemekana eti kimeandikwa na dada yetu! Mwandiko wa dada tunaujua, lakini huu ulikuwa wa kiume. Maandishi yalisomeka: ‘Sina thamani’, na kisha ikawekwa tarehe na namba yake ya simu (marehemu).

“Baada ya kuona picha tulipelekwa mochwari kwa ajili ya post-mortem, hapo walikuwapo watu kama 15 hivi. Askari polisi wa upelelezi watatu – wanawake wawili, na wa kiume mmoja. Alikuwapo OC-CID, madaktari wawili, wahudumu wawili wa mochwari, ndugu watatu wa marehemu, ndugu wawili wa mume na watumishi wengine watatu wa serikali.

“Mwili ulipoangaliwa kwa nje ulikuwa na michubuko kwenye mguu wa kushoto. Shingo haikuvunjika kama ilivyotarajiwa kwa mtu aliyejinyonga. Alikuwa pia na malengelenge (blisters) kwenye mbavu za kulia eneo la mgongo wa chini na eneo la shingoni. Alitokwa damu nyingi puani.

“Mwili ulipopasuliwa tuliona damu nyingi iliyovujia ndani upande wa kulia. Daktari akasema tuone…viungo vyote vilikuwa sawa. Walipofungua upande wa kushoto tulikuta bandama ikiwa imeharibika na kuvuja damu nyingi. Daktari akasema hiyo imesababishwa na kupigwa na kitu butu kilichopasua bandama na kusababisha kuvuja damu nyingi, hivyo kusababisha kifo chake. Baada ya hapo tulikwenda kuandika maelezo.”

Sintofahamu

Ndugu wa marehemu wanasema wakati wote wa uchunguzi wa mwili, mume wa marehemu hakushiriki, na sababu za kutoshiriki kwake hazikuwekwa bayana.

“Alikuwa nje ya ofisi ya OCD. Tulipomaliza kuandika maelezo ya kile tulichokiona tuliambiwa tukamuone OCD ili tupewe taarifa ya daktari, alikuwapo Ofisa Utumishi wa Wilaya ya Bukombe, Leah Kibaki na Ofisa Elimu Wilaya ya Bukombe, Shadrack Kabanga. Lakini OCD, alikataa kutoa taarifa hiyo akidai ni nyaraka ya kipolisi hatupaswi kuiona. Akasema kama hatumuamini daktari aliyesimamia, basi atauhifadhi mwili tukatafute daktari popote aje arudie post-mortem, lakini yeye hatatusomea kilichoandikwa.

“Alipokataa nilikumbuka lazima watuandikie kibali cha mazishi, hivyo tukaambiwa twende tena hospitali tukakichukue. Ofisa Elimu na Ofisa Utumishi wote pia walishangaa, hivyo tulilazimika kurudi hospitalini ambako daktari aliandika kibali cha mazishi ambacho ndiyo nyaraka pekee tuliyoondoka nayo iliyoonyesha chanzo cha kifo cha dada yetu – ambacho ni kupigwa ubavuni na kupasua bandama,” anasema ndugu wa marehemu.

Baadaye kukawapo mjadala wa mahali anakostahili kuzikwa marehemu Kizanye, lakini viongozi wa utumishi na elimu wakawa wako tayari kuwasikiliza ndugu na mume wa marehemu, maana hadi anafariki dunia alikuwa katika ndoa halali.

“Tukakaa wote – ndugu wa mume na sisi ndugu wa marehemu, tukawaambia kulingana na tulichokiona tutazika kwao marehemu – Nyarubanda, Wilaya ya Kigoma Vijijini, Mkoa wa Kigoma. Ndugu wa mume hawakubisha na huo ukawa ndiyo uamuzi.

“Awali, tukiwa bado eneo la mochwari kama saa 10 jioni, Mkuu wa Wilaya, Said Nkumba, alifika akiwa na viongozi wa usalama. Alimuita pembeni daktari, akampa taarifa ya kilichotokea. Baada ya hapo alikwenda nyumbani walipokuwa wakiishi marehemu na mumewe, kulikuwa na waombolezaji wengi.

“Tulimkuta mume wa marehemu ameshafika, akakaa kiti cha mbele kabisa karibu na jeneza. Mkuu wa Wilaya alipewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi, hakutaja lolote kuhusu chanzo cha kifo, wala hakusema lolote kuhusu uchunguzi wa kilichotokea. Alitoa pole kwa waombolezaji, akaongea tu kwamba maisha ni mafupi na kifo kipo, basi,” anasema ndugu wa marehemu.

Baada ya salamu za DC, waombolezaji waliaga mwili kisha safari ya kwenda Kigoma ilianza. Mwili ulisafirishwa kwa gari la halmashauri.

Mmoja wa ndugu wa marehemu anasema: “Licha ya ushahidi wa daktari na ule wa mazingira, mume wa marehemu aliondoka akiwa na msafara wa gari la marehemu na gari lake binafsi. Aliwapakia ndugu zake wote na kuondoka, akaenda zake kwao Ulyankuru, Urambo mkoani Tabora.”

Ndugu hao wanasema kabla na muda mfupi baada ya mazishi walipewa ushirikiano na askari wa upelelezi, lakini baada ya siku kadhaa walishangaa kuona hata simu zao hazipokewi.

“Kila tukimpigia simu mpelelezi akawa hawezi kuzungumza na sisi, mwishowe alisema tuzungumze na OC-CID kwa sababu yeye hakuwa na majibu kwa sababu ni mtu mdogo.

“OC-CID naye tumekuwa tukimpigia lakini hataki kupokea. Septemba 8 baada ya kutoka Kigoma kwenye mazishi tulimpigia simu mkuu wa wilaya, alipokea akasema hayuko ofisini, akaomba tumpigie Ijumaa saa 1:30 asubuhi. Ilipofika Ijumaa Septemba 10 tulimpigia, baada ya kujitambulisha na kumweleza shida akasema amekwenda nyumbani kwake Tabora, hivyo atanipigia Jumatatu Septemba 13 baada tu ya kikao.

“Akasema siku hiyo asubuhi kabla ya lolote, atakuwa na kikao na wahusika wote wakiwamo OC-CID na OCD, akaahidi atatueleza nini kinaendelea. Ilipofika Jumatatu, Septemba 13 tulisubiri simu yake bila mafanikio. Ilipofika saa nane mchana tulimpigia, alijibu kwa ufupi sana kwamba yuko na ugeni, nimpigie tena kesho yake saa mbili. Ilikatisha tamaa,” anasema mmoja wa ndugu wa marehemu.

Hata hivyo, JAMHURI limepata taarifa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo, Mwalimu Msonde, alikamatwa mwishoni mwa wiki na kuwekwa rumande kwa amri ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga. Hata hivyo, juhudi za chini kwa chini zilikuwa zikifanywa na uongozi wa polisi wilaya ili atolewe.

“Hili suala tatizo kubwa liko kwa OCD wa Bukombe, tunadiriki kusema itakuwa vizuri uongozi wa juu wamchunguze, maana anaonekana ana mpango wake tofauti. Swali letu, ana masilahi gani kwenye hili jambo? Hata kama mtuhumiwa ana ndugu yake mkubwa sana serikalini, bado tunaomba ndugu yetu atendewe haki,” anasema ndugu wa marehemu.

 Msonde azungumza

Kumekuwapo taarifa kutoka kwa watu walio karibu na familia ya Msonde kuwa yeye na mkewe walikuwa na migogoro ya ndoa ya mara kwa mara. Madai hayo yanathibitishwa na mmoja wa ndugu wa marehemu: “Dada hakuzaa, hali hiyo tunaichukulia kama kigezo kikuu cha ugomvi wao. Lakini dada mwenyewe aliamini kuwa licha ya umri wake (alizaliwa mwaka 1974) kuna siku atazaa. Sasa inaelekea hiyo ilikuwa sababu ya ugomvi wao.”

Mwalimu Msonde amezungumza na JAMHURI kwa simu mwishoni mwa wiki kuhusu kifo cha mkewe, na haya yalikuwa majibu yake: “Ni kweli nimefiwa na mke wangu, sahihi kabisa. Siwezi kuzungumza maneno mengi kwa sababu kwanza sikujui, lakini pia inawezekana nikawa ninazungumza na mtu ambaye si mwandishi wa habari.”

Licha ya mwandishi kujitambulisha na kujieleza kwa kila namna, Msonde aliendelea kugoma kutoa maelezo zaidi. “Hili suala la kifo cha mke wangu wasiliana na polisi, pia kama unataka kuzungumza na mimi lazima polisi wawepo, bila hivyo siko tayari kuzungumza.”

Ofisa Michezo na Utamaduni Wilaya ya Bukombe, ambaye alikuwa mkuu wa msafara wa mazishi yaliyofanyika mkoani Kigoma, Jennifer Kisusi, amezungumza na JAMHURI, na amegoma kuingia kwenye undani wa sakata hilo kwa kigezo kuwa yeye si msemaji.

“Serikali ina itifaki zake, mimi si msemaji, wasemaji ni Idara ya Mkurugenzi wa Halmashauri, mazingira unayajua. Nashauri mtafute Ofisa Elimu Wilaya. Ninachojua haya mambo yapo kwenye vyombo vya usalama, bado wanaendelea na uchunguzi, hao ndio watakupa majibu sahihi. Hii ni kesi ya jinai, ninashauri utafute maofisa wa halmashauri au wapelelezi wanaoshughulikia hili suala,” anasema Kisusi.

Ofisa Elimu Wilaya ya Bukombe, Kabanga, ameulizwa na JAMHURI kuhusu tukio hili, na mara moja akajibu kuwa Mwalimu Kizanye alijinyonga. “Alijinyonga nyumbani kwake Katete, hiyo ni kwa mujibu wa madaktari.”

Alipoulizwa kama taarifa ya madaktari inathibitisha kuwa amekufa kwa sababu ya kupigwa, Kabanga akasisitiza kuwa mwalimu huyo alijinyonga. Hata alipoulizwa kuhusu ujumbe wa maandishi unaodaiwa kuandikwa na Kizanye, akajibu: “Hakuna ujumbe alioacha. Vyombo vya uchunguzi vinaendelea na uchunguzi wa hili tukio, hadi sasa wanafuatilia, bado hata mwezi haujaisha. Hayo ya kwamba amepigwa sijayapata, nayasikia kwako. Hili ni suala la kipolisi. Wote hawa – marehemu na mume wa marehemu ni walimu wangu, kuhusu mirathi, ninaamini taratibu zitazingatiwa kutokana na kwamba aliandika nani arithi.”

Kwa upande wake, OCD wa Bukombe, Mkenye, ameulizwa na JAMHURI kuhusu tukio hilo na kujibu kuwa hana taarifa zozote juu ya tukio hilo.

“Mimi ni OCD ndiyo, lakini sina taarifa zozote za tukio hilo. Hata kama ningekuwa nazo mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi. Wewe ni mwandishi wa habari kweli? Umesomea kazi yako? Basi, mtafute RPC, maana mimi kwanza silijui hilo tukio, pia mimi si msemaji. Kila kitu kina taratibu zake,” anasema OCD Mkenye.

Hadi tunawenda mitamboni, Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Shinyanga hakupatikana kuzungumzia tukio hili.

Hata hivyo, DC wa Bukombe, Nkumba, amelithibitishia JAMHURI kuwapo kwa tukio hilo.

“Tukio hilo lipo, mwalimu amefariki dunia. Kama unavyosema, kumekuwapo maneno tofauti, sasa mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama nimeshatoa maagizo lishughulikiwe kwa mujibu wa taratibu za kiuchunguzi.

“Aliyekufa ni mtumishi wetu, mimi kama DC wajibu wangu mmojawapo ni kulinda maisha ya wananchi, siwezi kukurupuka kutoa kauli bila kwanza uchunguzi wa vyombo vya usalama. Nakuhakikishia kuwa uchunguzi unaendelea, na hatua zinachukuliwa. Kwa muda huu tuviache vyombo vifanye kazi zake. Naomba familia ya marehemu iwe na utulivu, suala hili litakwisha katika utaratibu wa haki,” amesema Nkumba.

By Jamhuri