Polisi wamtapeli kachero mstaafu

Maofisa wa Jeshi la Polisi nchini wasio waaminifu wamekula njama na kumwingiza matatani kachero mstaafu, Thomas Njama, ambaye kwa michezo yao ameshindwa kulipwa mafao yake Sh 47,162,559 tangu mwaka 2015, JAMHURI linathibitisha.

Njama anapigwa danadana kama ‘kibaka’ wakati amelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 37 na amekuwa mwanachama wa uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) tangu mwaka 1999, huku namba ya uanachama wake ikiwa CN 4894928. Njama alianza kazi mwaka 1978.

Mwaka 2001 akiwa na askari mwenzake anasema walipata tuhuma za kusababisha kifo cha mahabusu Mamula Mramba, wilayani Moshi, Kilimanjaro, hivyo yeye na wenzake wakakamatwa, wakashitakiwa na kuwekwa mahabusu.

Kutokana na tuhuma hizo, Jeshi la Polisi lilimshitaki katika mahakama ya kijeshi na kumfukuza kazi akiwa mahabusu, hivyo michango yake ikasitishwa kupelekwa PSPF tangu mwaka 2003. Aliwekwa mahabusu kwa miaka miatano hadi mwaka 2007 alipotolewa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya kuonekana hana hatia.

Njama amesema mahabusu Mramba alikamatwa kwa wizi wa kutumia silaha. Alimfanyia mahojiano kisha akamuweka ndani. 

“Mimi nilimwambia hii ni kesi ndogo kwani hujaua, wala hujapiga hata risasi moja, hii ni kesi ndogo. Yeye hakuwa na uzoefu wa kutumia bunduki, hivyo alikoki mara mbili, risasi zikapandana. Hivyo bunduki ikashindwa kufyatua risasi.

“Sasa huyu ndugu alikiri kila kitu nikamrekodi vizuri. Sasa askari aliyeingia akamkuta lock-up (mahabusu), akasoma jalada lote, kisha akaenda akauliza Mramba ndiye nani? Pengine alifanya hivyo kwa nia ya kumtisha ili ampatie hela kidogo. Yule Bwana Mramba akasema ‘ni mimi’. Yule askari akamwambia, kesi yako ni kubwa sana. Kama si kunyongwa unafungwa maisha au miaka si chini ya 30.

“Yule mtuhumiwa akasema ‘kweli’, akamwambia unatafuta ukweli gani wakati umekiri kila kitu hapa na kila kitu kimeandikwa? Hauna pa kutokea. Baada ya kuambiwa hivyo, yule mtuhumiwa Mramba akaanguka chini akazimia. Alibebwa akapelekwa hospitalini, akakaa huko miezi saba,  baadaye akafa. Alipokufa wakatukamata, wakatushitaki kwa mauaji.

“Nilikaa ndani kwa miaka saba, lakini wakati wote nilieleza kuwa mimi nikiwa askari kanzu hapo Moshi, nilimkamata huyu mtuhumiwa na kumfanyia mahojiano. Nilimwacha kwenye mahabusu akiwa salama, hivyo sihusiki na kifo chake. DPP alipitia maelezo yangu akaiondoa kesi mahakamani… huku nyuma niliishafukuzwa kazi, mshahara wangu ukakatwa, michango ikasitishwa kupelekwa PSPF… lakini baadaye nikarejeshwa kazini, nikalipwa mishahara yote, madeni ya nyuma yote yakalipwa yakiwamo ya PSPF,” amesema Njama.

Hata hivyo, baada ya kurudi kazini alibaini kuwa ana uanachama katika mifuko miwili; yaani PSPF na mfuko wa GEPF anaosema alibambikiziwa. Njama, ambaye amestaafu Juni, 2015 akiwa na cheo cha S/SGT, C. 8350, amesema wakati akiwa gerezani polisi walifanya njama wakamsajili katika mfuko wa GEPF bila yeye kuwapo. Amesema mpaka sasa kuna mtu (jina linahifadhiwa) anayepokea pensheni kupitia Acc. No. 40310007113 ambayo si yake, ambayo ipo Benki ya NMB na inaendelea kupokea mafao ya uzeeni kila mwezi hadi sasa.

GEPF walimwambia kwa miaka 16 aliyotumikia anastahili kulipwa mafao Sh milioni sita, kwani kwa miezi hiyo 192 aliyochangia alikuwa akichangia kama mwanachama wa hiyari, hivyo akachukua Sh milioni sita, lakini kwa mshangao mafao ya uzeeni wanayotoa yanaingia kwenye akaunti ya mtu mwingine anayemfahamu.

Anafahamu mchezo ulivyochezwa makao makuu ya Jeshi la Polisi na walioshiriki kufungua akaunti hiyo ya GEPF akiwa mahabusu wakidhani kwa kuwa alikuwa na kesi ya mauaji, basi ama angenyongwa au angefungwa maisha, hivyo kurudi uraiani ilikuwa haiwezekani, hivyo wakafungua akaunti feki ya michango na uanachama.

“Mchezo huu haujafanywa kwangu pekee. PSSSF wakague. Kuna askari na watumishi wengi waliostaafu wana akaunti mbili za mafao ya ustaafu. Kwa wanaofanikiwa, akaunti moja wanalipwa wao walio wastaafu wa ukweli, na hiyo nyingine wakubwa ndani ya Jeshi la Polisi wananeemeka kwa kutumia akaunti feki kama hii ya kwangu iliyopo NMB mtu anaendelea kupata pensheni kwa jina langu, wakati mimi sijapata haki yangu,” amesema Njama.

Baada ya Njama na wenzake kutuhumiwa Januari, 2001, hivyo kuondolewa kazini Februari 2001, mwezi Machi 2001 baadhi ya maofisa wa polisi waliokuwa kwenye Idara ya Fedha na Utawala walighushi na kufungua akaunti feki GEPF kuonyesha kuwa kuna mwanachama mpya aitwaye Njama, wakati yeye alikuwa gerezani.

Katika kufanikisha mchezo huo, walijaza mkataba wa kuonyesha kuwa Njama kwa hiyari yake aliamua kujiunga na mfumo wa malipo ya bakishshi (Gratuity), badala ya kiinua mgongo (pension). Ila katika harakati za kufoji wakakosea, kwani walionyesha kuwa Njama alijaza mkataba huo mwaka 1993, kumbe wakati huo mifuko ya jamii ukiwamo PSPF ilikuwa haijaanzishwa. PSPF ilianzishwa mwaka 1999, hivyo Njama asingeweza kuchagua kujiunga PSPF au GEPF kabla mifuko hii haijaanzishwa.

Baada ya kustaafu, alikwenda PSPF waliompigia hesabu kuwa amechangia miezi 446 sawa na miaka 37 na nusu, akaenda GEPF kuuliza imekuwaje akawa na akaunti mbili na mwajiri akawa anachangia kote, wakamwambia huko ilikuwa hiyari na amechangia miezi 192 sawa na miaka 16. Alipohoji iweje GEPF alipwe Sh milioni 6.8 kupitia hundi Na. 543 ya Desemba 28, mwaka 2015, wakasema: “Sisi wewe hukuwa mwanachama wetu, isipokuwa ulikuwa umechangia kama mwanachama wa hiyari.”

Barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa GEPF Januari 2016 yenye kumbukumbu namba GEPF. 1179/4894928/15 kwenda kwa Njama inaeleza kuwa ataendelea kupata pensheni ya kila mwezi ya Sh 136,279 ambayo italipwa kupitia akaunti yake namba 40310007113 iliyoko Benki ya NMB. Hii ilimshangaza kwani akaunti hii si yake, kwani akaunti yake halisi ni 40310007118 aliyoisajili katika Benki ya NMB kwa majina ya Thomas Sebastian Njama.

PSPF kwa upande wao walimpigia hesabu kuwa anastahili kulipwa kiinua mgongo cha Sh 47,162,022 sawa na miezi 444 ya uanachama wake na pensheni ya kila mwezi ya Sh 253,559 kwa mujibu wa hesabu alizopatiwa. Lakini PSPF kwa miaka minne mfululizo unashindwa kumlipa mafao hayo kwa kigezo kwamba ni mwanachama wa mfuko mwingine wa GEPF.

Kutokana na serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuunda mifumo miwili tu, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), anasema kwa kuwa yeye alikuwa mtumishi wa umma, PSSSF ndio wanaostahili kumpatia mafao ya Sh milioni 47 alizoahidiwa na PSPF awali, lakini wanasema kuna kikwazo cha mkataba aliosaini mwaka 1993.

“Hivi kweli hii inaingia akilini, yaani wakati niko mahabusu ndiyo niandike barua ya kuridhia kujiondoa kwenye uanachama wa PSPF kwenda GEPF?” amehoji Njama.

Katika toleo Na. 399 JAMHURI liliripoti habari hizi za Njama, ambapo Mkurugenzi wa PSSSF, Hosea Kashimba, alisema ni suala la kawaida hutokea na mara nyingi linasababishwa na uelewa mdogo anaokuwa nao mwanachama katika kufuatilia haki yake.

“Hilo ni suala la uelewa tu, mwambie huyo askari mstaafu aende kwenye ofisi zetu PSSSF za Ilala (Dar es Salaam) akaonane na meneja akamweleze tatizo lake,” alisema Kashimba. Alisisitiza kuwa haiwezekani pesa yake kupotea kama ana uhakika na hoja zake awaombe kukagua faili lake kubaini ni wapi lilipo tatizo liweze kushughulikiwa.

Aliongeza kuwa huenda tatizo hilo likawepo kwani kipindi cha nyuma askari waliokuwa wakiingizwa katika mifuko hiyo walikuwa wakitazamwa katika madaraja na vyeo vyao.

“Sidhani kama kuna tatizo hapo, huenda suala hilo limetokana na makosa madogo yaliyojitokeza wakati wa kuwapanga kwa madaraja. Ili tatizo liweze kurekebishwa mwambie afuatilie ajue makosa hayo ni yapi na yanarekebishika, na mweleze hivi, nimekuagiza aende ofisini kwa meneja Ilala wakague faili lake.

“Kama ana uhakika na stahiki zake uhakiki utafanyika na atalipwa tu hakuna wasiwasi wowote,” alisema Kashimba. Hata hivyo, pamoja na malekezo hayo ya Mkurugenzi wa PSSSF bado suala la Njama halijapata ufumbuzi na badala yake amekuwa wa kuhangaishwa katika ofisi za PSSSF zilizoko Dar es Salaam.

Kwa mara ya mwisho amesema wamemwelekeza kwenda Dodoma yaliko makao makuu ya PSSSF kuchukua stakabadhi ya malipo ya mshahara (salary slip) wake wa mwisho na kwamba akiifikisha ndipo suala lake lishughulikiwe.

Stakabadhi hiyo ameifuata Dodoma na kuileta Dar es Salaam lakini tangu ameifikisha na kuikabidhi kwenye ofisi za PSSSF zilizoko Ilala haoni utekelezaji wowote wa madai yake.

“Ndugu mwandishi mimi naona kama ninazungushwa tu bila sababu, kama mkurugenzi mwenyewe anaagiza suala langu lishughulikiwe, lakini watendaji walioko chini yake hawatekelezi, wewe unahisi haki yangu itapatikana kweli?

“Natamani kupata nafasi ya kumuona Rais John Magufuli nimweleze jinsi wastaafu tunavyopata taabu kwa sababu ya watendaji aliowaamini na kuwapa nafasi ya kumsaidia kazi, lakini wanamwangusha makusudi.

“Haiwezekani jambo kama hili kuchukua muda mrefu kwa kiwango hiki wakati liko wazi, kama si hujuma ninafanyiwa basi kuna uzembe fulani kwa watu wanaotakiwa kunisaidia,” amesema Njama.

Wakati Njama anaeleza malalamiko hayo, JAMHURI limemtafuta Ofisa Mkuu wa Mahusiano wa PSSSF, Eunice Chiume, aliyesema Njama leo aende kwa meneja wa PSSSF ofisi za Ilala, Dar es Salaam, ambapo atapatiwa nauli na posho aende Dodoma kwenye kikao cha kutatua mgogoro wake.

“Sasa mawasiliano yote tutayaweka kwenye maandishi. Mwambie aende pale Ilala, akamwone meneja ambaye atampatia yeye na mwanasheria wake nauli na posho ya siku tatu waje Dodoma tukae tulijadili suala hili tulimalize moja kwa moja,” amesema Chiume.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ameshangaa kuwepo kwa jambo kama hilo. “Hicho unachoniambia hakiwezekani, yaani mtu kuwa mwanachama wa mifuko miwili? Na yote ameichangia kama kawaida?” amehoji Misime. Ameongeza kuwa kama lilitokea wakati wa kuhamisha askari mifuko, basi litashughulikiwa lakini si suala la kawaida.

Kwa upande wake, Njama amesema amekwisha kuwasilisha vielelezo kwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde kwa nyakati tofauti, ila pamoja na ahadi walizompta kulipatia ufumbuzi suala hili ili apate malipo yake, hadi sasa amegonga mwamba.