*Kila kikao mbunge analipwa Sh laki 9

 

Posho ya Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ni Sh. 940,000 kwa siku. Malipo hayo ni kwa kila mbunge hata kama hakudhuria vikao vya Bunge.

Kutokana na utoro wa wabunge ambao umefikia kiwango cha kukwamisha vikao, juhudi za chini kwa chini zimeanza kufanywa na baadhi ya wabunge ili kubadili kanuni.

Mmoja wa wabunge hao ameiambia JAMHURI kuwa juhudi hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa mbunge ambaye hahudhurii kikao, anakosa posho.

Bunge la EALA linaundwa na wabunge kutoka nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Kila nchi inawakilishwa na wabunge kenda; hiyo ikiwa na maana idadi yote ya wabunge ni 45.

Hiyo ina maana kwamba kwa kila kikao, Sh milioni 42.3 zinatumika kuwalipa posho tu. Malipo hayo ni mbali na yale yanayofanywa kwa watumishi na wataalamu wengine katika Bunge hilo.

Aidha, malipo hayo ni tofauti na mshahara wa mbunge ambao ni zaidi ya Sh milioni 15 kwa mwezi. Malipo hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa mizigo mizito waliotwishwa walipa kodi wa nchi wanachama wa EAC; huku tija ya vikao vya wabunge hao ikiwa haionekani moja kwa moja kwa wananchi.

Utoro unatajwa kuwa moja ya mambo yaliyokithiri miongoni mwa wabunge, huku kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akitajwa kuwa miongoni mwa wanaoonekana kwa nadra mno kwenye vikao vya EALA.

Hivi karibuni vikao vya Bunge la Afrika Mashariki vilifikia tamati katika vikao vyake jijini Dar es Salaam, kwa kuahirishwa kabla ya muda wake kutokana na akidi kutotimia kwa vile wabunge wa Burundi na Rwanda kutoka nje na wengine kutokuwapo.

Sheria inataka ili kikao kiendelee lazima bungeni kuwe na nusu ya wabunge wa kuchaguliwa na angalau wabunge watatu kutoka kila nchi mwanachama.

Kikao kiliahirishwa baada ya Rwanda kuwa na mbunge mmoja na Burundi wawili. Hii ilikuwa mara ya pili baada Bunge hilo kuahirishwa kwa sababu kama hizo wiki iliyopita.

Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa Bunge hilo, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Abdulla Juma Sadalla, amesema Serikali imesikitishwa na vitendo hivyo vya wabunge kwa kuwa wanatumia kodi kubwa ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Bunge hilo lilianza Agosti 25 na lilitarajiwa kuahirishwa jioni lakini liliahirishwa mchana.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki aliahirisha kikao cha Bunge hilo baada ya akidi kutotimia kutokana na wabunge wa Rwanda na Burundi kutoka nje na wengine kutokuwapo kabisa katika siku ya mwisho ya Bunge hilo Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam Septemba 4, 2014.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera, alijibu hoja zilizoulizwa na wabunge wakati wa kikao cha Bunge hilo Karimjee Dar es Salaam Septemba 4, 2014 kabla hakijaahirishwa kutokana na wabunge wa Rwanda na Burundi kutotimiza akidi.

2154 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!