Mfuko wa vyombo vya habari nchini (TMF), kwa mara nyingine, umetoa ruzuku ya Sh. bilion 1.7 kwa vyombo vya habari 16.

Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura, alisema wakati wa kukabidhi ruzuku hiyo kwa vyombo vya habari mwisho mwa wiki kuwa mfuko wake umekuwa ukitoa ruzuku kwa nia ya kuendeleza habari za uchunguzi nchini.

Juzi mfuko huo, ulitiliana saini mkataba wa mwisho wa kutekeleza makubaliano ya kufanya habari za uchunguzi nchini na Watendaji 16 wa vyombo hivyo.

Sungura alisema ruzuku iliyotolewa inatakiwa kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba wamewaweka wakaguzi wao wa ndani watakaokagua mara kwa mara matumizi ya fedha zilizotolewa kwa nia ya kuhakikisha fedha zinasaidia wananchi.

Amesema wananchi kutoka nchi wafadhili wanatoa fedha hizo wakitaraji kuwa vyombo vya habari vitashiriki kikamilifu kuboresha utawala wa sheria serikalini na hatimaye huduma kwa jamii yenye uhitaji mkubwa.

“Ruzuku hiyo imetokana na msaada wa kodi za wananchi kutoka nchi za Denmark, Switzerland, Norway na Uingereza kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo (Tanzania) hivyo inatakiwa kuzithamini na kuweka nidhamu kubwa ya matumizi yake,” alisema Sungura.

Sungura alisema, kwa atakayefuja au kutumia vibaya ruzuku hiyo atakuwa anajitafutia ubaya na kwamba hatapata tena nafasi ya kupata ruzuku hiyo ambayo hutolewa kila mwaka.

Amesema jamii inazo dchangamoto nyingid hali ambayo inachangia maisha ya watu kuendelea kuwa duni, hivyo vyombo vya habari vinatakiwa kuangalia suala hilo katika kuibua mambo mbalimbali yenye kuzaa mabadiliko.

Amesema kwa sasa mahitaji muhimu ya binadamu hayapatikani katika jamii ikiwamo huduma za afya, shule na vitu vingine vya muhimu kutokana na changamoto za tabia za ubadhirifu.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vinahesabiwa kuwa ni muhimili ambao si rasmi ila ni muhimili muhimu unaofanya kazi kubwa ya kuibua mambo mbalimbali yakiwamo ya ufisadi.

Sungura amesema mkakati wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ni kuendelea kuviwezesha vyombo vya habari kuibua maovu ndani ya jamii, ili changamoto zilizopo zifafanyiwe kazi.

Ruzuku hiyo imegawanywa katika makundi mbalimbali na kwamba chombo cha habari kilichopata ruzuku kubwa ni Sh. milioni 185 na cha mwisho kimepata Sh. milioni 50.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, aliushukuru uongozi wa TMF kwa kuwa sehemu ya vyombo vya habari vilivyosaini mkataba wa kupata ruzuku hiyo juzi.

“Kama alivyosema Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, ndugu yangu Ernest Sungura chombo cha habari kina wajibu wa kurejesha matumaini yaliyopotea kwa jamii. Kwa mfano, Gazeto Jamhuri likiandika habari itakayookoa uhai wa wanyamapori zaidi 700 na wasiuawe, litakuwa limefanya kazi kubwa. Vyombo vya habari vina nguvu, vina nafasi ya kubadili maisha inayoishi jamii yetu,” amesema Balile na kuongeza:

“Chini ya mradi huu wa kuangalia matumizi ya mashine za elektroniki (EFD) kwa kila aina ya biashara kukusanya mapato halali ambayo ni kodi iliyokuwa inatafunwa na wafanyabiashara Gazeti la Jamhuri sasa tutafanya kazi kubwa na tunaomba wadau watuunge mkono kuhakikisha mashine hizi zinatumika kukusanya mapato ya serikali.

“Kodi ikikusanywa na kutosha, huduma za jamii zitaboreshwa. Miradi ya maendeleo ambayo kwa sasa inagharimiwa na wafadhili kwa asilimia 100 tutaanza kuigharamia sisi kama wafanyavyo Kenya. Nasema ahsante TMF, tuungeni mkono wananchi, serikali na wafanyabiashara kufanikisha mradi huu muhimu kwa taifa letu,” amesema Balile.

1150 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!