Ni matumaini yangu kuwa Watanzania wenzangu hamjambo hasa wale Watanganyika walalahoi kama mimi, sizungumzii wale wanaoishi kama wapo paradiso.

Nimesoma magazeti kadhaa, karibu wiki nzima yanazungumzia habari ya ‘mtoto wa mkulima’ Mizengo Pinda eti anataka urais na wengine kuanza kumpigia debe kwamba anafaa eti kwa vile ni muadilifu, pia hana tuhuma za ufisadi.

Si vibaya mtu kutoa maoni yake kwa mtazamo wake, ndiyo maana na mimi nimeona bora nitumie haki yangu ya kikatiba niseme lile ninaloliona linanifaa, na niwakumbushe wengine ambao wamesahau, au wanafanya hivyo kwa mapenzi tu.

Mwanzo nilikuwa najiuliza ni Pinda gani? Nilipoiona picha yake nikakumbuka kumbe ni yule yule Waziri Mkuu wangu aliyesimama mbele ya Bunge la Jamhuri ya Tanzania na kutoa amri kwa askari, kwamba watu wakijifanya wana nguvu wapigwe tu, hakuna jinsi na kwamba wamechoka. Hivi kweli huu ni uadilifu?

Baada ya kutoa amri ile kweli askari walipiga watu kule Mtwara wengine walipoteza maisha, wengine walichomewa nyumba zao, na ukatili wa aina mbalimbali, hivi huu ni uadilifu kweli? Hali hii waziri mkuu, akiwa rais wetu je? Watamchora katuni kama wanavyochorwa akina Jakaya Kikwete, si ataamuru waliochora hiyo katuni wafungwe kifungo cha maisha?

Kingine alichofanya kule Mtwara baada ya vurugu, alikwenda kutembelea eneo la kituo na alipita kwenye maeneo ya viongozi wa Serikali tu lakini kwa wananchi hakwenda kuwapa pole wala kuwajulia hali, huo ni uadilifu? Namuuliza yeyote anayejua maana ya uadilifu maana mimi naona sivyo.

Kuhusu ufisadi, hilo silijui lakini ninachofahamu kule Mikwambe huyo mzee anazo hekari kibao, sina uhakika ni ngapi, uongo kwangu mwiko. Wewe ukifika hata Kongowe ukimuuliza mtu kwa Pinda anakujua, kabla hujafika huko kwake utakutana na mtaa uliojaa fremu nyingi pameandikwa Katavi.

Kwa kusema kweli tu sitaki nimfurahishe mtu yeyote — awe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwenzangu au mtu yeyote asiye na chama — Pinda hafai kuwa Rais. Siyo yeye tu wapo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Steven Wassira, Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi; hawa ndiyo waliotufikisha hapa tulipo, ni wavurugaji wa Rasimu ya Katiba mpya.

Huu si wakati wa kuogopa kusema kweli, tukiogopa watatuwekea rais garasa waendelee kulinda maslahi yao. Kwa mtazamo wangu kwa upande wa CCM tukikosa kupata rais kwa upande wa vyama vingine, basi Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ni bora zaidi kuliko yeyote na ndiyo maana anafanyiwa mizengwe. Wanamwogopa, ni mtu mwenye msimamo, anajua jema na baya.

Alitolewa kafara kwa chuki, hakuwa na kosa, hata Bwana Yesu pia alisalitiwa bila kosa, hili wenye akili tunalijua. Mimi nina miaka 39 kwenye chama tangu  mwaka 1975 sijahama TANU na sihami, lakini kwa sasa japo nimebaki lakini sitampigia kura mtu wa CCM mwenye mlengo wa kulia asiyejali binadamu wenzake, ubinafsi na uroho wa madaraka.

Kama si Lowassa basi wa upinzani ni bora zaidi. Tunataka rasilimali zetu zirudishwe kutoka kwa wageni zibaki kuwa zetu kama zamani, huo ndiyo mtazamo wa walio wengi wenye ufahamu.

Hii ni nchi yetu sote mambo ya ukoloni yalishazikwa zamani. Tunataka Tanganyika yetu, tunataka rasilimali zetu, hatutaki kutawaliwa kiujanjaujanja. Mwalimu Julius Nyerere alishautokomeza ukoloni.

Mungu ibariki Tanganyika, Mungu ibariki Tanzania.

 

0773 – 402133

By Jamhuri