Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho hakina nguvu kama awali kutokana na kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Akizungumza leo Februari 24, 2018 katika mkutano wa ndani na wananchama wa CUF kwenye ukumbi wa Makonyo Chake Chake Pemba, Profesa Lipumba amesema uamuzi huo wa kutoshiriki uchaguzi uliobarikiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ndio tatizo la CUF kutokuwa na nguvu.

Amesema chama hicho kimekosa nguvu kwa kuwa hakimo tena katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar.

Wakati Lipumba akieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar upande unaomuunga mkono Maalim Seif, Nassor Ahmed Mazrui amesema hawatambui ziara hiyo kwa maelezo kuwa Profesa Lipumba si kiongozi wao.

“Chama kinawataka wanachama, viongozi na wapenzi wa CUF waliopo Pemba na Unguja kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao za maisha ya kawaida na kupuuza kabisa ujio huo wa Profesa Lipumba,” amesema Mazrui.

Katika maelezo yake Profesa Lipumba amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa ni fursa kubwa kwa CUF katika kupiga hatua za maendeleo kwa jamii na Taifa, kwamba kutokuwemo ni sawa na kuwakosesha haki wananchi wanaokiunga mkono chama hicho.

“Wawakilishi wangapi tumekosa kwa kugomea uchaguzi hili nataka lieleweke kuwa mtu akifanya jambo lazima aangalie maslahi ya mbali badala ya kuangalia maslahi ya karibu,” amesema.

Amesema kutokana na CUF kutokuwemo katika SUK, chama tawala kinaweza kubadili hata Katiba kwa urahisi.

Januari 28, 2016 Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilitangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC), likitoa hoja 12 zilizosababisha kufikia uamuzi huo.

Uchaguzi huo wa marudio wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani ulifanyika Machi 20, 2016.

Uamuzi wa CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo ulitokana na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 25, 2015 kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye kutangaza Machi 20, 2016 kuwa siku ya kupiga kura upya.

2229 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!