Profesa Ibrahim LipumbaAliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amekuwa sehemu ya makundi ya watu wa kada mbalimbali nchini anayepinga kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

“Zanzibar inaumbiwa hatari kubwa, na mtu wa kuokoa hatari hiyo si mwingine. Ni Rais Dk. John Pombe Magufuli. Nina imani na Rais Magufuli anaweza kulitatua hili kwa matokeo kutangazwa badala ya kurudia uchaguzi,” anasema.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani utakaofanyika Machi 20, mwaka huu.

Taarifa ya ZEC imesema uchaguzi utahusisha vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi wa awali na hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wala mikutano ya kampeni.

Imesema wapigakura watakwenda kwenye vituo siku ya kupiga kura na kuondoka kama ilivyo katika sheria ya uchaguzi. Uchaguzi wa Zanzibar ulifutwa Oktoba 28, mwaka jana, baada ya kudai kuwa kulikuwa na dosari zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huo.

Katika mahojiano na JAMHURI, Profesa Lipumba anasema: “Zanzibar kinaandaliwa kitu cha hatari. Na ni hatari kwelikweli kwenye uso wa dunia unaoamini katika demokrasia ya kweli.”

Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa JAMHURI kuwa Jecha anafanya kazi kwa mashinikizo makubwa kutoka chama kinachotawala sasa – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema mwaka 2010 Zanzibar iliifanyia marekebisho Katiba yake ya mwaka 1984 ambako pamoja na mambo mengine, iliweka utawala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo Rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein alishinda na mgombea wa CUF, Maalim Seif akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwa msingi huo, Profesa Lipumba anahoji: “Mbona aliposhindwa Maalim Seif 2010 alikubali kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, inakuwaje CCM inapinga sasa? Nadhani ni zamu ya Dk. Shein naye akubali.”

Anasema uchaguzi wa mwaka 2010 ulikuwa katika mfumo wa kuficha matokeo, lakini utaratibu wa uchaguzi uliopita wa mwaka jana, wa kubandika matokeo vituoni, umefumua mambo mengi yaliyokuwa kwenye ufichoni.

“Mbona baadhi ya wana-CCM walitangaza kwamba wanaongoza katika matokeo ambako walifikia majimbo 27, ikawaje tena matokeo yakafutwa, Jecha ni tatizo Zanzibar,” anasema.

Anadai Jecha alichukua madaraka ya kufuta matokeo bila ya baraka kutoka kwa makamishna kwani hata Makamu Mwenyekia wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa hakuwapo baada ya kuchukuliwa na polisi saa chache kabla ya kutangazwa kufutwa kwa matokeo.

Profesa Lipumba anasema, njia pekee anayoweza kuitumia Rais Dk. Magufuli ni kutangazwa kwa matokeo na ikitokea Maalim Seif ameshinda “Hakuna ubaya wowote.”

“Maana ninachojua moja ya hofu ya CCM ni ibara ya 54 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini sioni kama kuna ubaya wowote,” anasema Profesa Lipumba hasa akirejea historia ya uongozi wa Maalim Seif.

“Kwa sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Huko anahudhuria vikao vyote vya kiserikali anavyohitajika. Kuna tatizo gani limetokea?” anahoji.

“Maalim Seif amepata kuwa waziri katika serikali ya SMZ ya zamani hadi kufikia kipindi kuwa Waziri Kiongozi wa SMZ yaani ni kama Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano, aliharibu wapi?” anahoji tena.

Anasema miaka mitano iliyopita kwa nafasi yake kama Makamu wa Kwanza wa Rais akimsaidia Dk. Shein, hakuna machafuko wala dalili za machafuko zilizojitokeza.

Kabla ya kushika madaraka hayo, kiongozi mwenye hadhi ya Maalim Seif anapaswa kula kiapo – jambo ambalo amelifanya na nchi zote mbili zinazounda Tanzania zimekuwa salama,” anasema.

Profesa Lipumba anasema, CCM wanakuwa woga kutokana na ibara ya 54 inayosema: “Kutakuwa na Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake watakuwa ni Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na mawaziri wote.”

Anasema: “Sasa hiyo nafasi ya Rais wa Zanzibar wanaona ni hatari. Mimi sioni kama hatari na hakuna ubaya wowote kwa Maalim kuwa Rais Zanzibar na kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri.”

Alipohojiwa juu ya alichozungumza na Rais Dk. Magufuli baada ya kushinda, kutangazwa na kuapa kuwa Rais walipokutana, Profesa Lipumba anasema: “Mazungumzo yetu na Rais yataendelea kuwa siri…”

Alipotakiwa kueleza sababu ya kuwa siri ilihali kwa sasa anatoa maoni akitaka Rais Dk. Magufuli aingilie kati, Profesa Lipumba anasema: “Yalikuwa ni mazungumzo ya watu wawili.”

Alipoelezwa kwamba pengine kulikuwa na mpango wa kuteuliwa angalau nafasi moja ya uwaziri kati ya zile nne zilizokuwa kiporo kabla ya kujazwa, akajibu haraka: “Nimesema mazungumzo yangu na Rais yataendelea kuwa siri. Maana tulikuwa wawili tu.”

Alipohojiwa haoni kama anaingia kwenye mgogoro na Serikali kupinga uchaguzi wakati huo huo akibashiri hali ya hatari, jambo ambalo liliponza ‘maisha ya gazeti la Mawio’, Profesa Lipumba akajibu: “Hata mabalozi wanajua. Hivyo Jumuiya za kimataifa na nchi wadau wa maendeleo wanajua. Siogopi kusema ukweli.

“Itoshe kusema tu kwamba CCM inaturejesha mambo ya 2001. Nilikuwako. Mgogoro ule kisiasa ulikuwa mkubwa. Chanzo chake kilikuwa ni kukataa matokeo. Mambo yake bado yanasikitisha, sio mimi tu ninayesema hayo hata mabalozi wanasema.”

Profesa Lipumba anasema kwa kawaida uvumilivu una ukomo na ikitokea misingi ya demokrasia ikawekwa kapuni, njia nyingine inaweza kufuatwa na wananchi katika kutafuta ambacho wanakitaka.

Mbali ya Lipumba, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe naye mwishoni mwa wiki lililopita alijitokeza kupinga uamuzi wa kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar akisema dunia inashangaa.

Membe amefanya mahojiano na gazeti la Mwananchi ambako amependekeza CCM na Serikali isiwaachie watu wawili tu, Rais wa SMZ Dk. Shein na Maalim kutafuta njia za kutatua mgogoro huo.

Kadhalika yuko Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye muda wote anashinikiza matokeo kutangazwa akiungana na Maalim Seif na msimamo wa CUF wanaopanga kususia uchaguzi huo.

Taarifa kwamba kuna harakati za chini kwa chini kumshawishi Lipumba agombee tena uenyekiti wa CUF, alisema hajazisikia na kwamba hakuna mwanachama yeyote aliyezifikisha kwake rasmi.

By Jamhuri