Wiki iliyopita Mwenyekiti wa Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), Robert Kisena alikutana na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam akazungumza nao kuhusiana na habari kuu tuliyoichapisha katiak toleo Na 225 la Gazeti la JAMHURI.

Katika maelezo yake, alikanusha habari tuliyoichapisha ukurasa wa kwanza iliyosema “Familia ya Kikwete inahusika UDA.” Katika habari hiyo, tulionyesha kuwa mtoto wa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete,  Khalfan Mrisho Kikwete nyaraka za kampuni ya Simon Group Ltd zinamtaja kama mmoja wa wakurugenzi.

Habari hii tuliichapisha baada ya kupata taarifa ya uchunguzi wa kina (due diligence report) iliyofanywa na Kampuni ya Philip and Co iliyochunguza Simon Group ni nani na ana uwezo kiasi gani katika kuendesha biashara ya usafirishaji wa abiria hadi apewe shirika kama UDA iliyowasilishwa kwa Jiji la Dar es Salaam, Novemba 2009.

Kati ya mambo yote yaliyomo kwenye ripoti hiyo tuliyoyachapisha, Kisena amekanusha suala la familia ya Kikwete kuhusika katika UDA pekee. Baada ya kukanusha huko, mjadala mkubwa umeendelea katika vyombo vya habari kwa maana ya magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii.

Kisena wakati anakanusha alisema kuna watu wanatumia waandishi kisiasa, hapana shaka akimaanisha kuwa waandishi wa JAMHURI wanatumika kisiasa. Kwa nia ya kulinda heshima ya gazeti hili linalothaminika katika jamii kwa habari za uchunguzi, tumeamua kuweka kumbukumbu sawa na wala si kuanzisha malumbano.

La kwanza tumekubali kitaaluma Kampuni ya Simon Group kutoa makala ya mtangazaji katika toleo letu la leo. Tumefanya hivyo kwa kuamini kuwa chombo cha habari ni uwanja huru unaopaswa kutoa fursa kwa yeyote mwenye jambo analotaka kulisema aliseme bila kunyimwa fursa hiyo kisha jamii ndiyo ipime uhalisia wa asemalo. Ni kwa msingi huo tumekubali kuchapisha toleo lake.

Pili tunapenda kuweka wazi kuwa hatuna shaka, wala wasiwasi na taarifa hii ya uchunguzi tuliyoipata na kuichapisha katika toleo Na 225. Tumeamua kutafsiri kifungu cha 2.1.2 kinachohusu umiliki wa hisa katika ripoti hiyo kinachosema:

Umikili wa hisa

“Kama kampuni nyingi za Tanzania ambazo zilianzishwa na watu binafsi au familia, kampuni hii haina leja ya hisa.

“Simon Group Ltd

“Mwaka 2008 hesabu zilizokaguliwa za Simon Group Ltd, wakurugenzi waliotajwa ni wawili tu: Ndugu Robert Kisena, na Ndugu Khalfan Mrisho [Kikwete]. Hata hivyo, hati ya mkopo iliyotiwa saini Mei 31, 2008 kwa ajili ya mkopo uliochukuliwa kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), mtia saini wa pili katika hati hiyo ni mtu aitwaye William Simon Kisena. Hivyo idadi ya wakurugenzi bila shaka ni zaidi ya wawili ikiwa nyaraka hizi zitaaminika. Idadi ya wamiliki wa hisa pia haiko wazi.

“Hesabu pekee zilizochapishwa, ambazo ni za Simon Group Ltd pekee, zinaonyesha kwamba hisa za mtaji zilizoidhinishwa ni Tsh bilioni 2, lakini mtaji uliolipiwa ni Tsh milioni 670.

“Kwa kutokuwapo mapato ya mwaka wa 2008, umiliki halisi na makazi ya wakurugenzi na mengine hayawezi kuthibitishwa.” Sehemu hii ya repoti ya ukaguzi wa kina ambayo ipo kwenye vitabu vya taasisi nyeti za kifedha nchini, tunaamini inaendelea kuwa sahihi hadi itakapofutwa na wakaguzi walioifanya.

Katika taarifa yake, Kisena amesema Kampuni ya Simon Group ilianzishwa mwaka 2007 na wanafamilia wa familia ya Mzee Simon na imepewa jina hilo kwa heshima ya Baba yao, Mzee Simon Kisena Maige.

Wakurugenzi wa Simon Group anasema ni Robert Simon Kisena, William Simon Kisena, Kulwa Simon Kisena, Gloria Robert Simon, Simon Robert Simon, George Robert Simon, Modesta Pole, na mwanahisa pekee kutoka nje ya familia, Juma Kapuya, anayemiliki asilimia 5.

 Alihitimisha kwa kusema inawezekana kuna watu wana ugomvi wa kisiasa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete hivyo wasitumie ugomvi wao kupitia kampuni ya Simon Group.

Tunachofahamu na kuamini ni kwamba habari za uchunguzi zinajikita katika ukweli, ukweli tupu bila uonevu, wala upendeleo. Tunaindesha kampuni ya Jamhuri Media Ltd na gazeti inalozalisha la uchunguzi la JAMHURI kitaaluma na kwa weledi wa hali ya juu.

Kama ambavyo mara zote tumechapisha habari zetu bila hiyana, woga, upendeleo au uonevu kwa kutaja mifano michache kama Bandari, maliasili, dawa za kulevya, watakatisha madini na nyingine nyingi tunaamini kote huko tulifanya kwa kusukumwa na uzalendo tukitanguliza masilahi ya taifa chini ya falsafa yetu ya “TUNAANZIA WANAPOISHIA WENGINE”, na hivyo ndivyo tulivyofanya kwa UDA. Taarifa ya Simon Group tumeichapisha ukurasa wa 19.

 

Mhariri

2565 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!