Mabadiliko Bandari

DSC01990Baada ya Bandari ya Dar es Salaam kulalamikiwa kwa muda mrefu kuwa haina ulinzi mzuri wa mali za mateja, hatimaye uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) umechukua hatua za dhati kwa kuimarisha mfumo wa ulinzi. Kati ya mambo waliyofanya, ni pamoja na kuanza kufunga kamera za usalama (CCTV) zipatazo 486 ambazo sasa zinamulika Bandari ya Dar es Salaam mchana na usiku.

Si kamera tu, katika kinachoonyesha kuwa wameshituka na kuamua kudhibiti wizi na biashara haramu kupitia Bandari ya Dar es Salaam, Jumapili iliyopita walipokea mbwa wanne wenye utaalamu wa kunusa dawa za kulevya na pembe za ndovu hata kama zitakuwa kwenye kontena.

Si hayo tu, wizi wa mafuta unaolalamikiwa kwa muda mrefu nao sasa unaelekea kupata muarobaini, baada ya kufunga flow meter ya dizeli kwa gharama ya dola milioni 6.5 (karibu Sh bilioni 14).

Katika ulinzi, kupitia mradi wa Integrated Security System uliogharimiwa na Bandari wenyewe, ambao nao umegharimu dola milioni 6.5 (Sh bilioni 14), kuanzia wiki iliyopita wameanza kufunga kamera za usalama na wamefanikiwa ndani ya wiki moja kufunga kamera za 226 kati ya 486, zinazopaswa kufungwa kabla ya mwezi huu. “Hapa wala si utani. Ni lazima kuendana na kasi ya Rais [John] Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa [Kassim]. Maelekezo waliyoyatoa yako wazi, ni ama tunafanya kazi au tunawapisha wengine wanazifanya,” alisema mtoa habari aliyeshangaa kasi ya kufungwa kamera na kuongeza idadi ya vifaa vya usalama bandarini.

Chini ya mradi huo wa ISS Bandari ya Dar es Salaam imezungushiwa waya wa umeme yote, hivyo mtu akithubutu kuruka ukuta atanaswa, kamera zinaona kila malango ya kuingilia (gates) yamefungwa vifaa maalum vya kufunga na kufungua.

“Huyu mtaalam aliyeko katika chumba cha CCTV anaweza kufunga au kufungua gate lolote akiona kuna gari analolitia shaka au kitu chochote. Pia wameweka speaker (vipaza sauti) kila kona ya bandari hivyo anaweza kutokea hapa akatoa tangazo lolote au kumwambia mtu wa kitengo chochote kuwa jambo fulani linatokea na hatua zikachukuliwa,” anasema.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wataalam ndani ya Bandari, kamera zilizofungwa ni za kisasa kwa kiwango ambacho kama kuna tukio la wizi au lisilo la kawaida, kamera mbali na kurekodi tukio hilo inatoa ishara kwa mtu aliyeko control room anaivuta na kuangalia mara moja kinachoendelea kisha hatua zinachukuliwa.

“Zote kwa pamoja zinapiga picha na kuleta taarifa wakati wote na kwa maeneo yote ya bandari na nchi kavu kwani kila kitu kinaonekana kwenye control station. Hata ikitokea gari inaondolewa, mtu wa chumba maalumu ana uwezo wa kuzuia kutokana na miundombinu ya kielektroniki iliyofungwa bandarini kwa sasa,” anasema mtoa habari na JAMHURI lilishuhudia mfumo huo wa kisasa. Anasema kwa mfano, “Hata mtu mwenye nia ovu akishika gari, kamera humnasa na kutoa taarifa na hatua zikachukuliwa mara moja. Hii itatusaidia sana si tu kupunguza, bali ni kufuta kabisa wizi na Bandari zetu zikabaki kuwa salama wakati wote.

Anasema kamera hizo zinaweka kumbukumbu ambazo pia uhifadhiwa angalau kwa mwaka kabla ya wataalamu kuchuja taarifa za kubaki nazo na nyingine kuziondoa.

Sambamba na kamera mamlaka hiyo imenunua radio mpya za mawasiliano zinazowahamisha kutoka mfumo wa VHF (Very High Frequency) kwenda UHF (Ultra High Frequency) zenye ufanisi wa hali ya juu.

Tofauti na zamani, wamenunua mashine za

Pia wameboresha mfumo wa ukaguzi kwa kununua mashine za kubaini mionzi (radiation detectors) na vyuma (metal detectors), ambapo katika mageti yote tofauti na zamani kwa sasa kila anayeingia atakaguliwa kwa mashine maalum.

Katika vita ya kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya na nyara za serikali kama pembe za ndovu, Serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake hapa nchini imetoa msaada wa mbwa wanne wenye uwezo mkubwa wa kunusa na kutambua dawa za kulevya na pembe za ndovu hata kama zipo kwenye kontena.

Tanzania inaelezwa kama njia ya kusafirisha dawa za kulevya na pembe za ndovu kwenda Amerika na Ulaya, huku vipusa vingi vikielekezwa Asia, hivyo mbwa hao waliotarajiwa kuwasili Jumapili usiku kutoka Marekani wanatajwa kuwa ufumbuzi wa tatizo.

TPA wametoa eneo la mita za mraba 20 kujenga nyumba maalumu kwa ajili ya mbwa hao. “Mbwa hao wana uwezo wa kunusa na kutoa taarifa na kuonesha kontena lenye dawa za kulevya au pembe za ndovu hata kama wamefunika kwa kiasi gani,” anasema mtaalam aliyezungumza na JAMHURI. Marekani inatoa msaada huu chini ya idara ya usalama wa mipaka (Customs and Border Protection). “Hata kama kontena limebeba meno ya tembo, mbwa hawa wana uwezo wa kulitambulisha. Hii ni hatua nzuri ambayo kwa kweli ni njia mojawapo ya namna ya kudhibiti maliasili za nchi na kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia bandari zetu”.

Pia Bandari imeboresha miundombinu ya barabara ndani ya Bandari kwa kupiga lami chini ya msaada wa Kampuni ya Trade Mark East Africa na kuifanya sura ya bandari na kuipa mwonekano mpya.

Kwa upande wa mgogoro wa wizi wa mafuta uliotokana na kusitishwa kwa matumizi ya flow meter, ufumbuzi umeanza kupatikana ambapo sasa tayari mita ya dizeli na mafuta ghafi (crude oil) imefungwa eneo la Mji Mwema, Kigamboni kwa gharama ya dola milioni 6.5 (karibu Sh bilioni 14).

Watendaji TPA wameliambia Jamhuri kuwa mita nyingine kwa ajili ya petrol, vilainishi, mafuta mazito, mafuta ya kula na nyingine itafungwa.

Baadhi ya wataalam ndani ya TPA wameliambia JAMHURI kuwa kuna haja ya kufanya uchunguzi upya juu ya ubora wa flow meter zilizopo eneo la KOJ, ambazo kwa ujumla wake ni 16, ambazo zilipofungwa ziliimarisha mapato kutoka wastani wa bilioni 4 hadi 60 kwa mwezi wakati zinatisishwa.

JAMHURI lilipowasiliana na Kaimu Meneja Mawasiliano, Janeth Ruzangi, alithibitisha maboresho hayo ya kamera, flow meter na ujio wa mbwa wa kunusa dawa za kulevya na pembe za ndovu.

“Mizigo ya wateja kuanzia sasa itakuwa salama zaidi na Bandari itakuwa tofauti na mwanzo ambapo tulikuwa tunatumia physical guarding (watu kuwapo kila mahala kulinda), sasa eneo kubwa zaidi linalindwa na mitambo ya kisasa, mizigo inakuwa scanned, nasema usalama umeongezeka,” amesema Ruzangi.

Amesema usalama ulioimarishwa bandarini ukichanganywa na mfumo wa kulipia mizigo kwa kutumia mtandao wa kompyuta (online clearance) ulioondosha mawasiliano na binadamu, basi ufanisi umeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Ruzangi aliongeza kuwa Bandari sasa inafanya kazi saa 24, hali iliyoondoa msongamano wa makontenda na mizigo ya wateja ya kila aina. Pia amesisitiza kuwa wizi wa makontena hautokei bandarini bali kwenye Bandari Kavu (ICD) baada ya kuwa yametolewa bandarini.

Anaamini jengo linalokamilishwa ujenzi la Bandari ambalo litamwezesha mteja kupata huduma zote katika jengo moja (one stop centre) nalo litaongeza ufanisi zaidi.

Katika jengo hilo kutakuwapo huduma zote kama za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mawakala wa forodha, viwango, vipimo, watu wa chakula na dawa na huduma nyingine.

Kabla ya miradi hii Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na msongamano mkubwa wa makontena huku wizi wa vifaa vya magari ukiwa umetamalaki, lakini baada ya vyombo vya habari, hasa gazeti la JAMHURI kuandika habari hizo kwa kina, uongozi wa Bandari umefanya mabadiliko makubwa kwa nia ya kuboresha huduma na kuondoa malalamiko.

Matunda ya kelele hizo za vyombo vya habari ni pamoja na kubainika kwa upotevu wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo hatimaye imebainika kuwa makontena zaidi ya 14,000 yamepotea yakiwa kwenye Bandari Kavu.

Baadhi ya wafanyabiashara kama Said Salim Bakhresa tayari melipa karibu Sh bilioni 5 kutokana na upotevu wa makontena yakiwa kwenye ICD zao, hali iliyoongeza mapato ya TRA na kuvunja rekodi yake kwa kukusanya Sh trilioni 1.3 mwezi Novemba na Sh trilioni 1.4, mwezi Desemba.