Kumetolewa matamshi kadha kutoka kwa wanasiasa na hasa wasomi wa vyuo vikuu mara tu baada ya Rais wa Jamhuri kuteua wakuu wa mikoa wapya.

Baadhi ya wanasiasa wazoefu hapa nchini, ama kwa kukusudia (deliberately), au kwa kutokujua kwao (sheer ignorance), wametoa matamshi -mimi ningesema ni hatarishi au hasa potovu.

Mwanasiasa maarufu, tena msomi – profesa ametoa matamshi nadhani yanaweza kueleweka visivyo na baadhi ya wananchi. Matamshi namna ile mie nayaita potovu. Hayalengi kujenga, hayasisimui, ila yanahofisha wasomaji na kubaki kujiuliza hivi Serikali inatupeleka wapi sasa.

Tumesoma katika Gazeti la Mtanzania Toleo Na. 8124 la Jumanne, Machi 15, 2016 uk. 2 kuna kichwa cha habari: Profesa Baregu: “Ni utawala wa Kijeshi”.

Mtu akisoma hayo tu hupatwa na hisia kuwa nchi hii sasa inatawaliwa kijeshi. Tujuavyo tawala za kijeshi zinatokea baada ya mapinduzi. Wale wanajeshi walioshika madaraka, kwanza kabisa wanasimamisha Katiba ya nchi, wanalifuta Bunge la nchi husika, wanafuta vyama vyote vya siasa na ndipo wanaweka huo utawala wao wa kijeshi.

Mimi nikajiuliza kule kutaja majina ya majenerali wanne wastaafu ndiko profesa ameita utawala wa kijeshi? Labda kwa mtazamo wake kila penye wanajeshi wachache katika Serikali, basi hapo pana utawala wa kijeshi! Sijui kati ya dhana hizi mbili sahihi ni ipi. Inafaa kukumbushana kidogo hapa. Kwanza niulize, ni lini au wakati gani nchi inastahili kutajwa ina utawala wa kijeshi? Ni lini au wakati gani Serikali inakuwa ya kidemokrasia?

Kwenye uteuzi huo wa wakuu wa mikoa, Rais Magufuli hakufanya cha ajabu hata profesa aite ni utawala wa kijeshi.  Profesa ametumia maneno namna hii eti kwamba wanajeshi huwa hawana hulka ya kidemokrasia. Akasema hivi: “Kitu kimoja kinachojitokeza kwenye uteuzi huu ni kuwepo kwa wanajeshi wastaafu, na mimi ninavyoelewa wanajeshi huwa hawana hulka za kidemokrasia. Hii inaonyesha wazi kwamba utawala huu ni wa kijeshi”. Maneno  haya ni ya kupotosha dhana nzima ya utawala wa kijeshi.

Tuangalie kihistoria namna wanajeshi walivyoshiriki katika utawala. Katika nchi mbalimbali- kule Marekani mara tu baada ya Vita Kuu ya II mwaka 1945 ulifuata uchaguzi wa Rais wa Marekani baada ya Rais Harry Truman mwaka 1952. Marekani ni nchi tunayoiamini yenye demokrasia halisi. Katika uchaguzi ule wa mwaka 1952 alijitokeza Jenerali mashuhuri wa Vita ya Korea akiitwa Jenerali Dwight David Eisenhower. Huyu kutoka Korea alipelekwa kuongoza vikosi vya majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Ulaya (NATO) akawa Mkuu wa kile kilichoitwa SHAPE (Supreme Headquarters of the Allied Powers of Europe). Huo sasa ulikuwa ni Umoja wa Majeshi wa nchi rafiki zilizoshiriki Vita Kuu ya II kule Ulaya. Jenerali Eisenhower akastaafu na akarudi Marekani kugombea kiti cha urais kwa tiketi ya Republicans, akashinda. Basi, akaja kuwa Rais wa 34 wa Marekani.

Si huyo tu, bali hata alipomaliza mihula yake yote miwili ya urais, alifuatwa na mwanajeshi mwingine. Huyu alikuwa kijana John F. Kennedy aliyegombea urais kwa tiketi ya Democrats mwaka 1960 na akashinda akawa Rais wa 35 wa Marekani. Kennedy alikuwa Kapteni mstaafu wa Jeshi la Majini wakati wa Vita Kuu akiongoza meli ya Torpedo iliyoitwa PT – 109 ambayo kwa bahati mbaya mwaka 1943 Wajapani waliipiga na Kapt. Kennedy alipata kuumizwa.

Nako Ufaransa, shujaa wa Vita Kuu ya II akiitwa Jenerali Charles De Gaulle. Alitawala Ufaransa wakati hali ya uchumi wa nchi ile ilikuwa mbaya sana. Wafaransa walimchagua kwa kura nyingi mno na akawa Rais wa utawala wa Jamhuri ya Tano (President of the Fifth Republic) tangu Mei 1958 hadi mwaka 1963.

Nimetaja mifano hii ya nchi za wakubwa kule Magharibi kwenye demokrasia tunavyoamini sisi Waafrika kuwa ni kamili, walivyotumia majenerali wao wa Jeshi kuimarisha (stabilize) utawala wao huo wa demokrasia. Sijasikia mwanasiasa yeyote kutamka eti zile nazo zilikuwa ni Serikali za kijeshi! Hapo sijui profesa wangu anaweza kunijulisha kama demokrasia huko kwa wakubwa ilifinyangwa?

Labda niongeze hapa kwa nia ya kupanua mawazo ili nieleweke vizuri zaidi. Mwaka 1973 – 1974, Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alimteua Luteni Kanali Abdallah Twalipo (baadaye akaja kuwa Jenerali na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi – CDF – 1974 – 1980, na ndiye aliyepiganisha vita ile ya Kagera kwa jina la Kamanda Chakaza) kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera (RC). Siku hizo Iddi Amin aliwachachafya sana wananchi wa Kagera.

Si huyo peke yake. Kagera wamepelekwa wanajeshi kadha kuwa ma-RC (yupo Lt. Jenerali Tumainieli Kiwelu, Kanali Mfuruki, Kanali Massawe na leo hii Jenerali Kijuu). Hapo kwa faida tu ya profesa na wasomaji wangu tuelewe tu kuwa kumekuwapo utaratibu au utamaduni katika Serikali za nchini mwetu, kuwa na mtindo wa kuwashirikisha wanajeshi kuongoza mikoa na hata wilaya.

Hapakuwahi kusikika kauli kutoka kwa wanasiasa eti hii sasa ni Serikali ya kijeshi. Kwa vipi profesa msomi aje leo ataharuki na kutamka vile – kweli Tanzania inatawaliwa kijeshi? Ni matamko potovu tu. Labda kumekuwa na msukumo wa kisiasa kutoka chama chake – sijui.

Imekuwaje leo katika uteuzi wa Rais Magufuli kutokea tamko tena  kwa mwanasiasa mzoefu na msomi “eti kuna Serikali ya kijeshi sasa”. Huko ni kutumia maneno vibaya. Ni upotoshwaji wa makusudi kabisa. Katika wakuu 26 wa mikoa, wapo wanajeshi watano tu -kumbe wale 21 si wanajeshi. Hapo tunaona ni asilimia 16.7 ndio wanajeshi  wakati asilimia 83.3 si wanajeshi. Unawezaje kusema ni Serikali ya kijeshi au utawala wa kijeshi (how do you justify such au assumption?).

Kama ilivyokuwa kule Marekani, wanajeshi waligombea urais wakashinda kwa itikadi ya vyama vyao, nasi hapa nchini Rais wetu wa Awamu ya Nne alikuwa Luteni Kanali (wa JWTZ) Jakaya Kikwete. Akagombea urais na akashinda. Hapakuwa na Serikali ya kijeshi hata kidogo wala profesa hakuwahi kulitamka hilo. Hii hofu aliyonayo profesa hadi atamke wazi wazi hivi inatoka wapi? Mimi sielewi hata kidogo. Kila mwananchi awe mkulima, mtaalamu wa fani fulani, au mlinzi wa Taifa akiwa tu na sifa zinazohitajika, rais anaweza kumteua kumsaidia katika kazi yoyote ile na mahali popote pale. Ni “prerogative” ya kila Rais kufanya uteuzi wake.

Ubaguzi wa eti huyu mwanajeshi umeanza lini? Kwani mwanajeshi siyo mwananchi au siyo mzalendo au mkereketwa wa maendeleo ya Taifa lake la Tanzania? Maendeleo ya nchi yanaletwa na wananchi wenyewe.

Basi, Profesa Baregu, kwa kukusaidia uelewa zaidi ni kuwa Serikali za kijeshi zinatokana na mapinduzi na zinatawaliwa na kikundi cha wanajeshi kinachojulikana duniani kote kama “Military Junta”. Sijui kama umewahi kusikia jina hilo.

Kwa wasomi wa vyuo vikuu wanajua sana historia za nchi zenye utawala huo wa kijeshi ulimwenguni. Mara nyingi wanasiasa hasa wasomi wamekuwa wanashauriwa kuwa waangalifu katika kutoa maoni yao wasibwatuke tu kwa hisia za itikadi za imani zao za vyama vya siasa.

“Military Junta” Waingereza wanaelezea vizuri sana namna hii: “A Military Junta is a clique of junior army officers who seize power from a democratically elected government”. Kwa maelezo namna hiyo sisi tujiulize kwa maoni na matamshi ya Profesa Baregu, ndivyo ilivyotokea nchini mwetu hali namna hiyo? Mbona hawa walioteuliwa na Rais wote ni Senior Army Officers kama akina Eisenhower na De Gaulle? Ni dhahiri msomi wetu hajui mambo ya kijeshi wala aina ya vyeo vyao. Hapo angejinyamazia tu.

Huko nyuma enzi za utawala wa Warumi kulikuwa na angalizo kwa wasomi kuchunga ulimi wao wasije wakatamka yasiyofaa kwa wenzao. Warumi wakisema “SIC TARCIS PRUDENTERE VIDISES” yaani ukimya au ukinyamaza bila kusema neno utafikiriwa una busara. Ukimya unafikiriwa kuwa ni dalili za hekima, lakini kuropoka ropoka unaweza ukateleza ulimi na wasikilizaji (hapa wasomaji) wako wakakuhukumu vinginevyo.

Sisi wazee tuna imani na nyie wasomi maprofesa wetu. Lakini kwa matamshi namna hii ya upotoshaji tunaona hayastahili kutolewa na mtu msomi kama profesa hivi.

Laiti maoni kama yale ya wasomi wengine kuwa wanaoteuliwa ni watu mchanganyiko au kwa kusema kila mkuu ana haki ya kupanga timu yake anayoona itamsaidia kuendana nayo katika malengo yake, hapo ni sahihi kabisa. Ni kutoa maoni chanya na hapo maoni yako yatasaidia kujenga utawala uliopo.

Naamini kila kiongozi ana haki ya kuteua watakaomsaidia. Juzi juzi Mwenyekiti wa CHADEMA amemteua Dk. Vicent Mashinji kumsaidia uongozi kama Katibu Mkuu wa Chama hicho. Hiyo tunasema ni “prerogative” yake kufanya vile. Kama mtu mwingine anakubaliana naye au hakubaliani naye, hilo ni shauri jingine. Mtu anaweza kutoa maoni yake tofauti lakini kutoa maoni yake binafsi hii ni haki ya kila mtu kikatiba.

Laiti wanajeshi wangeweza kushauri, profesa asingetumia tamko namna ile eti kuna utawala wa kijeshi. Huko ni kutokujua maana halisi ya aina hiyo ya utawala.

Naomba nijiridhishe kwa swali hili: Profesa uliwahi kuhenya katika kambi la JKT? Huko hakuna ubabaishaji wala maneno maneno. Kuna KAZI TU. Basi, acha wateuliwa wa Rais wakatekeleze yale majukumu waliyopewa wasikatishwe tamaa kwa maneno kama yale uliyotoa. Hayajengi nchi.

Nashauri wanasiasa jitahidini kutoa maoni chanya kulingana na usomi wenu. Vionjo hasi vizuieni katika mioyo yenu. Tunasema mezeeni msitapike kwa umma- haifurahishi. Demokrasia haina FOMULA hapa duniani. Basi tusichanganye maana halisi ya utawala wa kijeshi hapa nchini. Tusiwachanganye wananchi. Wanasiasa mjue na mpime mnayotuambia. Hapa pana KAZI TU hapana Serikali ya Kijeshi.

1503 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!