Wiki iliyopita Taifa limetikiswa na habari za waziri wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Juma Kapuya, kutuhumiwa kumbaka binti mwenye umri wa miaka 16.

Habari hizi ziliandikwa kwa mara ya kwanza na Gazeti la Tanzania Daima. Tumefuatilia kwa makini mwenendo wa matukio, na makataa waliyopewa Tanzania Daima ya kumwomba radhi Kapuya ndani ya siku saba.Kapuya ametoa makataa hiyo kupitia kwa wakili wake, Yassin Memba. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amekaririwa na vyombo vya habari akisema hawezi kumwita Kapuya kumhoji, kwani anaona mambo hayo yalikuwa binafsi, na hivyo wanapaswa kumalizana. Binti huyu anadai amekwishakwenda hadi bungeni na kote huko hapati msaada.

Kova ameripotiwa kuwaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa hawawezi kumwita Kapuya kwa sababu haya ni mambo yake binafsi na hakuna mtu yeyote ambaye amefika polisi kulalamika kutendewa vibaya na Kapuya.

“Hata hivyo kama kuna ushahidi wowote wa kueleweka si kusingizia mtu vituo vya polisi viko wazi masaa 24,” amesema Kova.

Kwa habari zilizoandikwa binti huyu amekwishatoa taarifa hizi kituo cha Polisi Oysterbay, lakini hakupata msaada wowote zaidi ya kutakiwa wasuluhishane, na tangu wakati huo inadaiwa kuwa Kapuya amekuwa akimlipa fedha kila mwezi.

Sisi hatuwezi kumhukumu Kapuya kuwa alitenda kosa hili au la, na wala hatutilii shaka maelezo ya wakili Memba. Tulielekea kushtushwa na kauli ya Kova kuwa “hayo ni mambo yao binafsi” lakini tukafurahishwa na maelezo ya Kova kuwa vituo vya polisi vipo wazi saa 24. Huu ni wakati wa Polisi Oysterbay kujitokeza hadharani kusema kama binti huyo aliwahi kufungua jalada pale au la.

Tunasema kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kifungu cha 130 kinafafanua mazingira ya kubaka ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu, ulaghai, udanganyifu, kurubuni, na kifungu cha 131 kinasema bayana kuwa mtu anayekutwa na kosa la ubakaji anastahili kupata kifungo cha maisha jela, ikibidi pamoja na viboko.

Kosa hili kwa kuwa chini ya Kanuni ya Adhabu kwa yeyote anayelitenda anatenda kosa dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa upande mwingine, Kova hawezi kuanzisha uchunguzi ikiwa hakuna mtu aliyejitokeza kulalamika.

Sisi tunasema nyadhifa alizopata kushika Kapuya ni kubwa na zenye heshima kubwa katika Taifa hili. Si vyema mtu mkubwa kiasi hiki kutuhumiwa, tena na binti wa miaka 16, kisha Serikali ikaziacha zipite hivi hivi. Ikiwa Serikali imeshindwa kuzichunguza, basi tunaomba mashirika ya kutetea haki za binadamu yamsaidie binti huyu.

Hatumwombei mabaya Kapuya, tunataka uchunguzi ufanyike ili ikithibitika kuwa kweli Kapuya amembaka binti huyu, basi aadhibiwe kwa kiwango ambacho itakuwa fundisho kwa jamii, ila ikithibitika kuwa Kapuya hakumbaka, basi Mahakama imsafishe na kulinda heshima ya Serikali alizopata kuzitumikia, kisha binti huyu afunguliwe mashitaka (counter claim) achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria iwe fundisho kwake na wengine wakome kusingizia watu mabaya.

Hili lisifumbiwe macho, tulinde heshima ya Tanzania.

 

1111 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!