Profesa MwamilaMakamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Profesa Burton Mwamila, amejiuzulu kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi, JAMHURI linaripoti.

Kujizulu kwa Profesa Mwamila, kumekuja siku chache baada ya vyombo vya ukaguzi vya Serikali kumaliza kazi ya kuchunguza tuhuma dhidi ya uongozi wa chuo ambazo zimeandikwa na JAMHURI kwa wiki nane.

Licha ya kutumia fedha za umma nyingi kujisafisha, na hata kulishitaki Gazeti la JAMHURI katika Baraza la Habari Tanzania (MCT), hatimaye imetbibitika kuwa yaliyoandikwa na JAMHURI yalikuwa sahihi.

Amejizulu mapema wakati ripoti ya uchunguzi ikiwa bado haijawekwa hadharani, lakini ikitajwa kuwa imesheheni matukio mengi na makubwa yanayohusu ufisafi wa mabilioni ya fedha za Serikali na matumizi mabaya ya ofisi.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amethibitisha kujiuzulu kwa Profesa Mwamila.

Pamoja naye, watumishi wengine wako kwenye orodha ya, ama kusimamishwa, au kufukuzwa kazi kutokana na kujihusisha kwenye matukio ya ufisadi.

Vyanzo vya habari kutoka NM-AIST vinasema miongoni mwa watakaokumbwa na fagio hilo ni wahasibu na watumishi walio kwenye kitengo cha rasilimali watu.

“Mipango ya kuwaondoa inaendelea, na wengine wataishia mahakamani kwa sababu ushahidi wa matukio ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka uko wazi kabisa,” kimethibitisha chanzo chetu.

JAMHURI limethibitishiwa kuwa nafasi ya Profesa Mwamila, kwa sasa inakaimiwa na Profesa Osmund Kaunde, ambaye kabla ya kupelekwa hapo alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya.

“Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la NM-AIST, Profesa David Mwakyusa, napenda kuwafahamisha kwamba Mkuu wa Chuo cha NM-AIST amepokea ombi la Profesa Burton Mwamila, la kujizulu nafasi yake ya Makamu Mkuu wa Chuo…Mkuu wa Chuo amemteua Profesa Osmond Kaundekuwa Kaimu Mkuu wa Chuo kuanzia Agosti 1, 2016. Hadi hapo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo atakaporipoti, Profesa Karoli Njau, atakaimu nafasi hiyo,” ilisema taarifa iliyotolewa na Dk. Martin Kimanya.

Baadhi yahabari zilizoandikwa na JAMHURI kuhusu hicho hicho ni “Jipu Chuo cha Mandela Arusha”.

Habari hiyo ilisema: “Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikisisitiza ubanaji matumizi, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ya jijini Arusha, imebainika kukodisha nyumba na kulipa mamilioni ya shilingi kila mwaka bila kuitumia.

“Nyumba hiyo ipo Kitalu C eneo la Njiro jijini humo. Imekodiwa kwa malipo ya Sh 1,500,000 kwa mwezi kwa maelekezo ya Makamu Mkuu wa Chuo, licha ya kuwapo ukinzani kutoka kwa Baraza la Chuo. 

“Huu (2016) ni mwaka wa tatu malipo hayo yakifanywa kila mwezi. Uchunguzi umebaini kuwa Sh milioni 43 zimeshatumika kumlipa mmiliki wa nyumba na mlinzi kwa upangaji huo ‘hewa’.

“JAMHURI inaendelea kufanya utafiti kumjua mmiliki wa nyumba hiyo ingawa kwenye ankara ya maji jina la mmiliki linasomeka la Mina Said Mohamed, lakini kwenye ankara ya LUKU jina ni la Saum Ally Said.

“Kwanza hakuna umuhimu wa nyumba hiyo kwani tuna nyumba nyingi sana na za kisasa zilizo tupu ndani ya chuo, tuna researchers village- nyumba zake ziko tupu ndani ya chuo, na tuna rest house ndani ya chuo. Pamoja na kupiga sana kelele katika Baraza la Uongozi la Chuo, Mkuu wa Chuo hajakubali kuiachia nyumba hiyo. 

“Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila, anajibu tuhuma hizo kwa kukiri kukodiwa kwa nyumba hiyo.”

Habari nyingine ilikuwa na kichwa cha habari cha: “Chuo cha Mandela kinavyotafunwa”.

Ilisema kuwa ufisadi wa kutisha na matumizi mabaya ya madaraka vimebainika kuwapo katika Taasisi NM-AIST ya jijini Arusha, JAMHURI linathibitishia wasomaji.

“Pamoja na kununuliwa kwa vifaa vya mabilioni ya shilingi ambavyo, ama havitumiki, au vipo chini ya kiwango, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila anadaiwa kutumia muda mrefu kusafari ndani na nje ya nchi.

“Nyaraka zinaonesha kuwa kuanzia Novemba 27,2014 hadi Januari 18, mwaka huu alisafiri safari 40, ikiwa ni wastani wa safari tatu kila mwezi.

“Katika kipindi hicho safari za nje ya nchi zilikuwa 13, na za ndani zilikuwa 27. 

“Amesababisha hata wasaidizi wake nao wawe watu wa kusafiri tu. Safari hizo zimegharimu fedha nyingi mno. Katika kipindi cha mwanzo cha zuio la Rais kwa safari za nje, alisafiri safari mbili za Ethiopia-hatuna hakika kama alikuwa na kibali. Nusu ya mwezi huwa hayupo ofisini,” kimesema chanzo chetu.

 

Ununuzi wa vifaa 

“Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Chuo kilinunua vifaa vyenye thamani ya dola 120,000 za Marekani Sh milioni 240) kupitia kampuni ya Dar Worth ya Dar es Salaam bila kuwashirikisha wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano.

“Ununuzi wa Smart Board:  Hizi zinazotumika kufundishia, na zimetengenezwa kwa teknolojia ya Kimarekani. Imebainika kuwa hazitumiki licha ya kufungwa katika vyumba vya madarasa.”

 

Habari nyingine ilisema: “Mamilioni yaliwa Chuo cha Nelson Mandela”

Katika habari hiyo, tuliandika kuwa uongozi wa NM-AIST unazidi kuandamwa na kashfa mbalimbali, na safari hii imebainika kuwapo matumizi makubwa ya fedha kwenye ujenzi, utoaji zabuni na ununizi wa vifaa.

“JAMHURI limethibitishiwa kuwa ujenzi wa karakana ni miongoni mwa maeneo ambayo yametafuna fedha nyingi, huku ujenzi ukiendelea bila kuwapo bango linaloonesha ujenzi huo kama sheria inavyotaka.

“Lengo ni kukwepa isijulikane na kuzuia mamlaka husika kama TBA kuja kukagua,” amesema mtoa habari wetu.

“Sh milioni 300 zilitengwa awali kwa kazi hiyo, na mkandarasi akalipwa lakini baadaye akaondoka kazi ikiwa haijakamilika.

“Aliombwa kuendelea na kazi bila ya mafanikio. Baada ya muda mrefu akaonekana kama amerudi kufanya kazi, lakini kimsingi anayefanya kazi si yeye, ni mtu mwingine nyuma ya pazia. 

“Gharama zimepanda hadi Sh milioni 602 na bado zinaongezeka. Gharama hizo zimekuwa zikipanda bila ya idhini ya Baraza la Uongozi wa Chuo.

“Makamu Mkuu wa Chuo amekuwa na kawaida ya kuomba Baraza libariki matumizi ya fedha kwa kazi hiyo,” kimesema chanzo chetu.

 

Kulipa riba ya Karangai

“Uchunguzi umebaini matumizi ya Sh milioni 500 zilizotumika kulipa riba kwa eneo lililonunuliwa la Karangai; kitu ambacho hakikuwemo kwenye mkataba wa ununuzi wa eneo hilo. Mkaguzi wa nje kwenye ripoti yake amebaini kuwapo kwa ufujaji huo wa fedha za umma.

“Aidha, mashine mbili za “Kora System” na “Sensor” zilinunuliwa nchini Kenya kwa ajili ya maktaba bila kufuata kanuni za ununuzi, licha ya vifaa hivyo kupatikana hapa nchini.”

Makala nyingine ilikuwa na kichwa cha habari: “Fedha zatafunwa  Chuo chaMandela”

*Uongozi waandaa majibu kuidanganya Serikali

Tuliandika kuwa uongozi wa Taasisi NM-AIST unajitahidi kufanya kila linalowezekana kuficha vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika chuo hicho.

“Hivi karibuni uongozi huo umewasilisha serikalini kile kinachoonekana kuwa ni utetezi dhidi ya sehemu ndogo kati ya yale yaliyoandikwa na yanayokusudiwa kuandikwa na Gazeti la JAMHURI.

“Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Burton Mwamila, amekwenda Baraza la Habari Tanzania, ikiwa ni juhudi zake binafsi na wasaidizi wake katika kuficha ukweli wa yale yanayoendelea katika NM-AIST.

 

Fedha za utafiti za wanafunzi

“Fedha za utafiti za wanafunzi ni miongoni mwa fedha zinazodaiwa kutumika vibaya. Kuna udanganyifu kwenye bajeti zinazowasilishwa kwenye vikao vya Chuo na fedha halisi wanazopewa wanafunzi.

“Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu wanapewa malazi (accommodation) ya hali ya chini tofauti na kiwango kilichotolewa na mfadhili.

“Kuna udanganyifu na kupandisha bei kwenye ununuzi wa vifaa vya utafiti wa wanafunzi. 

“Wanafunzi wajawazito walikuwa wakiondolewa kwenye hosteli za Chuo kwa lazima pasipo kurudishiwa fedha zao licha ya kuwa zimelipwa na mfadhili.

“Wanafunzi wanalazimishwa kuzalisha vitabu vya utafiti kwa fedha zao licha ya kua chuo kimechukua fedha hizo kutoka kwenye ada na chuo kilipaswa kuzalisha. Wanafunzi waliohitimu mwaka 2013 vitabu vyao havipo kwenye kumbukumbu za maktaba kwa sababu fedha za kuzalisha zilizolipwa kwenye ada zilitumika kwa mambo mengine.

“Chuo hakirejeshi fedha za tahadhari za wanafunzi hata kama wamefanya uhakiki wa kutokudaiwa au kuharibu mali yoyote.”

2258 Total Views 1 Views Today
||||| 3 I Like It! |||||
Sambaza!