DAR ES SALAAM

Na Zitto Kabwe

Miaka 10 iliyopita nikiwa nimekaa kwenye jukwaa la wageni waalikwa katika sherehe za uhuru wa Sudan Kusini, nilimwona mzee mmoja akitembea taratibu akiwa amepinda mgongo na kitambaa cheupe mkononi.

Alikuwa akitembea uwanjani kuelekea jukwaani siku hiyo ambayo Jamhuri ya Sudan Kusini ilitangazwa kuwa huru. 

Shughuli za uhuru zilikuwa zimeanza na uwanja ulikuwa umejaa pomoni, kukiwa na wakuu wa nchi na serikali kutoka Bara zima la Afrika.

Uwanja ulikuwa kimya, ninadhani kwa bumbuwazi, kwani kila mtu alikuwa amekaa lakini mzee huyu alikuwa akiendelea kutembea kuelekea jukwaani. 

Kulikuwa na kitambo. Mwendesha shughuli alitangaza kwa umma kuwa huyo anayetembea si mwingine bali ni Kenneth David Kaunda.

Uwanja ulilipuka kwa shangwe, nderemo na vifijo. Jukwaa kuu la marais na mawaziri wakuu wote walisimama kupiga makofi mpaka mzee Kaunda alipoketi.

Ilikuwaje aingie uwanjani wakati marais wote, akiwamo Rais mwenyeji, wameshaingia? Lilibaki swali kwa wengi pale jukwaani nilipokuwa nimekaa. 

Baadaye nilifahamishwa na maofisa wa Mambo ya Nje wa Tanzania kuwa mzee Kaunda alikuwa amefika muda ule ule kwa kuwa ndege yake ilichelewa.

Mapokezi yake pale uwanjani yalionyesha jinsi ambavyo wazee hawa walioanzisha na kuendesha vita ya ukombozi walivyobaki na heshima zao hata katika maisha yao ya ustaafu. 

Kwa Jamhuri ya Sudan Kusini, Rais mstaafu wa Zambia na Mwenyekiti wa Pili wa Nchi za Mstari wa Mbele kuhudhuria siku yao ya kuwa taifa huru, ilikuwa ni heshima kubwa.

Miezi michache baadaye, Machi 2012, nilibahatika kuonana na mzee Kaunda. Nilikuwa Lusaka kwa shughuli za kibunge na nililiomba Bunge la Zambia kuniombea nafasi ya kwenda kumsalimu. 

Alinipokea vizuri ofisini kwake na tukazungumza mambo kadhaa ya Afrika. Kwa hakika mazungumzo hasa yalikuwa ni maswali na majibu kuhusu maisha yake ya kupigania uhuru.

Ninakumbuka unapoingia tu ofisini kwake unakutana na picha ya yeye Kaunda, Mwalimu Julius Nyerere na mzee Jomo Kenyatta wakiwa Uwanja wa Ndege wa Nairobi, Kenya wakisubiri kuunganisha ndege kwenda Uingereza. 

Kaunda na Kenyatta walikuwa mawaziri wakuu wakati ule kabla ya nchi zao kuwa na mamlaka kamili, maana zilikuwa bado zina utawala wa ndani na hazijawa huru. Tanganyika tayari chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilikuwa imepata uhuru.

Nilimuuliza mzee Kaunda kama anakumbuka picha ile ilipigwa lini; akaniambia ilikuwa Januari 1964. Walikuwa vijana watanashati wakiwa wanajiamini sana. Aliniambia kuwa muda ule Afrika ilikuwa ina matumaini makubwa sana.

Akanieleza namna alivyokuwa na ukaribu wa kindugu na Mwalimu Nyerere na hata mzee Kenyatta japo siasa zao hazikuwa zinashabihiana sana. Wote watatu sasa wametangulia mbele ya haki. Mzee Kenneth David Kaunda hivi karibuni, jijini Lusaka.

Kenneth Kaunda, maarufu KK, alikuwa ni mwasisi pekee wa Nchi Huru za Afrika aliyekuwa hai. Kuna makosa yanayotokana na mazoea tu kusema kuwa Kaunda alikuwa mwanzilishi wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Zambia haikuwa nchi huru wakati OAU inaanzishwa Mei 25, 1963, hivyo si Kaunda wala Jomo Kenyatta waliokuwa miongoni mwa viongozi waliotia saini mkataba wa OAU. Zambia ilijunga na OAU Februari 26, 1965.

Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa KK alikuwa mstari wa mbele katika harakati za uhuru wa Bara la Afrika na kwamba uhuru wa Zambia ulipatikana muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa OAU, ni rahisi sana kufanya kosa hilo.

KK pia alikuwa ni muumini mkubwa wa Umoja wa Afrika. Alishiriki karibu mikutano yote ya OAU na kuwa Mwenyekiti wake mwaka 1970, kufuatia Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi uliofanyikia Addis Ababa, Ethiopia.

Zambia ilipata uhuru nyakati ambazo nchi za kusini mwa Bara la Afrika zilikuwa zimeanza harakati za ukombozi dhidi ya utawala mkongwe wa Ureno katika nchi za Msumbiji na Angola, vilevile utawala dhalimu wa kibaguzi wa makaburu huko Afrika Kusini na Namibia. 

Licha ya kwamba Zambia ilizungukwa na nchi nyingine zilizokuwa huru kama Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC) na Malawi; ni nchi mbili tu zilizopakana na Zambia ndizo zilikuwa na utawala ambao ni rafiki. Hizo ni Tanzania na Botswana.

Malawi, chini ya Dk. Hastings Kamuzu Banda, ilikuwa karibu na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini na Zaire ilikuwa inatumiwa na nchi za Magharibi dhidi ya juhudi za ukombozi. 

Zambia ilikuwa katika wakati mgumu sana kwa kuwa ni nchi isiyo na bahari. Ilitegemea mizigo yake kupitia bandari za Beira au Nacala nchini Msumbiji iliyokuwa chini ya Ureno na kusafirishwa kupita Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) ambayo ilikuwa imekaliwa na mlowezi, Ian Smith. 

Hapa ndipo uongozi wa Rais Kaunda ulikuwa na majaribu makubwa – kulinda masilahi ya nchi yake kwa kushirikiana na tawala dhalimu au kusaidia vyama vya ukombozi na kuondoa ukoloni barani Afrika. Alichagua la pili, kwa gharama kubwa sana.

Katika moja ya vikao vya Kaunda na Nyerere walimwalika Rais Seretse Khama wa Botswana na hapo ndipo kwa mara ya kwanza jina ‘Nchi za Mstari wa Mbele’ lilianza kusikika, yaani ‘Frontline States’.

Kikao cha kwanza kilifanyika Lusaka na Mwalimu Nyerere akawa Mwenyekiti wa Kwanza wa Frontline States kinyume kabisa cha utamaduni wa rais wa nchi mwenyeji kuwa mwenyekiti. 

Mark Chona, msaidizi maalumu wa Rais Kaunda katika masuala ya ukombozi ananukuu namna Rais Nyerere alivyokuwa mwenyekiti:

“Ilikuwa ni suala la kuwatoa jela wapigania uhuru wa Zimbabwe, mkutano wa kwanza ulikuwa mwezi Oktoba, nikiwa nimetumwa Cape Town na KK alitaka kuwapa mrejesho wenzake; Rais Nyerere na Rais Khama.

“Walipokaa, Mwalimu akasema: ‘Oh! Kenneth, wewe ni mwenyeji. Naomba uwe mwenyekiti.’ KK akajibu: ‘Hapana, Mwalimu; ongoza kikao, mimi ni mwenyeji tu.’ Kikao cha pili kilipofika, Mwalimu alimtaka tena Kaunda awe mwenyekiti na Kaunda akasema: ‘hapana, hapana, kikao cha kwanza uliongoza vizuri sana, endelea tu kuongoza vikao’.”

Kumbukumbu ya Rais Kaunda hasa ni ukombozi wa Afrika. Wakati wake Zambia ilihudumia vyama vya ukombozi, kutatua migogoro ya vyama hivyo, kuvisaidia kifedha na kuwaandaa kwa ajili ya kutawala nchi zao. Kutokana na haya, Zambia ilishambuliwa na Ian Smith na ndege za Afrika Kusini na hata wakati mmoja kulikuwa na tishio la Zambia kumalizwa kwa bomu la nyuklia ambalo inasemekana lilikuwa linatengenezwa na Afrika Kusini.

Katika kukabiliana na kuifanya Zambia kutotegemea bandari za Msumbiji na Afrika Kusini, ndipo Rais Kaunda na Rais Nyerere waliamua kuomba msaada China kujenga Reli ya TAZARA [Tanzania-Zambia Railway]. 

Reli hiyo pia inajulikana kama Uhuru Railway (Reli ya Uhuru). Vilevile inasemekana kuna wakati Zambia nayo ilianza matayarisho ya kuunda bomu la nyuklia ili kupambana na Afrika Kusini.

Nchi za Mstari wa Mbele ziliendelea kuongezeka kila uhuru ulipopatikana. Kwanza Angola na Msumbiji mwaka 1975 kisha Zimbabwe mwaka 1980, hivyo kufikia nchi sita. 

Kazi kubwa ilikuwa ni kukamilisha ukombozi wa Afrika Kusini na Namibia ambazo zilikombolewa mwaka 1991 kwa Namibia na mwaka 1994 kwa Afrika Kusini. 

Mzee Kenneth Kaunda alikuwa mbele kabisa katika kukamilisha kazi hii kubwa ambayo iligharimu damu nyingi za wananchi wa nchi yake.

Rais Kaunda pia alifanya uamuzi ulioleta sintofahamu kati yake na viongozi wenzake katika Nchi za Mstari wa Mbele au kushawishi wenzake kufanya uamuzi kinyume cha OAU. 

Mambo matatu yanakumbukwa zaidi. Moja ni kuhusu kuitambua Biafra kama nchi huru kutoka katika Shirikisho la Nigeria. Uamuzi huu ambao ulifanywa na nchi nne tu za Afrika; Zambia, Gabon, Ivory Coast na Tanzania, ulileta zogo kubwa katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika.

Tanzania iliitambua Jamhuri ya Biafra Aprili 13, 1968 na Zambia ilifanya hivyo mwezi mmoja baadaye, Mei 20, 1968. 

Nimepata kuhadithiwa na kiongozi mmoja mstaafu wa Tanzania ambaye wakati huo alikuwa balozi na alihudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa OAU jijini Algiers, Algeria, Septemba, 1968 ambao ulijadili suala la Biafra. 

Rais Kaunda alitukanwa na kushambuliwa na marais wenzake kiasi cha kuukimbia mkutano ule. Rafiki yake, Mwalimu Nyerere, hakuhudhuria na badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Rashidi Mfaume Kawawa. 

KK aliendelea kuamini katika Biafra kwa muda mrefu kiasi cha kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Kiongozi wa Biafra, Kanali Chukwuemeka Odumegwu Ojukwu, Novemba, 2011.

Jambo la pili ni kuhusu kutambuliwa kwa uhuru wa Angola kupitia MPLA [Movimento Popular de Libertação de Angola]. Uhuru huo ilioupata mwaka 1975 kutoka kwa Ureno ulitokana na vita ya ukombozi ambapo kulikuwa na vyama vitatu vya ukombozi – MPLA cha Augustino Neto, UNITA [National Union for the Total Independence of Angola] cha Jonas Savimbi na NFLA [National Liberation Front of Angola] cha Holden Roberto. 

Kwa kuwa uhuru wa Angola ulitokana pia na mazungumzo baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Ureno (na mazungumzo haya yaliendeshwa na Zambia), hapakuwa na chama cha ukombozi ambacho kilikuwa kimelishika Jiji la Luanda. Hivyo, Umoja wa Afrika uliingilia kati kwamba chama gani kikabidhiwe uhuru.

Umoja wa Afrika uligawanyika mapande bila upande wowote kuwa na kura nyingi. Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika jijini Addis Ababa mabishano yalikuwa makubwa na Rais Kaunda alitoa hotuba ya kuonyesha mwelekeo wa kuunga mkono UNITA ya Savimbi, jambo ambalo lilimkasirisha sana Mwalimu Nyerere na ujumbe wa Tanzania.

Hivyo, Mwalimu Nyerere hakutoa hotuba yake isipokuwa maneno machache kumjibu Rais wa Senegal, Léopold Sédar Senghor kuhusu UNITA na MPLA.

Mwandishi wa habari mbobezi na mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, alikuwapo Addis Ababa akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Afrika na alipata kunihadithia kuwa hali ilikuwa mbaya sana. 

MPLA waliamua kuingia Luanda na kutangaza uhuru baada ya Ureno kuacha ombwe kwa kubwaga ‘instruments of power’ [hati za madaraka].

Jenerali ambaye alikuwapo Luanda siku ya uhuru hawezi kuisahau siku hiyo kutokana na Tanzania kuonekana haina msimamo licha ya kumtuma Makamu wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi, katika sherehe zile. 

Mpaka mauti yanamkuta mzee Kaunda, suala la yeye na Jonas Savimbi na UNITA bado ni jambo ambalo halikueleweka kabisa.

Jambo la tatu ni suala linalohusu nchi yake. Rais Kaunda aliadhibiwa vikali na serikali ya walowezi wa Rhodesia na makaburu wa Afrika Kusini kiasi kwamba uchumi wa Zambia ulianguka kabisa.

Alikuwa amefunga mpaka wa kusini lakini TAZARA haikuweza kusafirisha mbolea na bidhaa nyingine kuingia Zambia. Wananchi walianza kumlaumu kwa siasa zake za kusaidia ukombozi bila kuangalia masilahi ya nchi yao.

Kinyume cha makubaliano na viongozi wenzake, pia kinyume cha ahadi yake kuwa “hatafungua mpaka hadi Zimbabwe ipate uhuru” KK aliamua kufungua mpaka wake na Zimbabwe. 

Katika kikao cha Nchi za Mstari wa Mbele, ugomvi mkubwa ulitokea kati ya marais Samora Machel wa Msumbiji, Agostinho Neto wa Angola, Kenneth Kaunda wa Zambia na Julius Nyerere wa Tanzania. 

Mzee Joseph Butiku, Katibu wa Rais wakati wa Mwalimu Nyerere, amerekodiwa akisema mkutano ule ulikuwa ni moja ya mikutano migumu kabisa kuhudhuria akiwa na Rais Nyerere.

Butiku anasema: “Katikati ya kikao viongozi walianza kulia. Sisi wasaidizi kazi yetu ni kuchukua kumbukumbu za maongezi. Mimi niliandika tu, ‘marais wanalia’!”

Hata hivyo, mzee Kaunda alimaliza ngwe yake ya uongozi  kwa somo kubwa kwa demokrasia ya Afrika pale alipokubali kushindwa uchaguzi na kukabidhi madaraka ya urais kwa Frederick Chiluba mwaka 1991.

Kaunda alikuwa kiongozi asiye na makuu kiasi kwamba alipomaliza urais hakuwa na mahala pa kuishi. Rais aliyeingia madarakani baada yake alimsumbua hadi akamsweka ndani kwa kosa la uhaini.

Akiwa jela, aligoma kula hadi ikabidi Mwalimu Julius Nyerere kwenda kumwona. Ndipo akaacha mgomo wake. Rais wa tatu wa Jamhuri ya Zambia, hayati Dk. Levy Patrick Mwanawasa, ndiye aliyerudisha hadhi ya Baba wa Taifa kwa Rais Kaunda.

Pia akampa stahiki zake zote kama Rais mstaafu, ambapo ameendelea kuzipata mpaka mauti yalipomkuta.

By Jamhuri