ASKARI MAGEREZA: ‘Wafungwa huru’ wanaoifia nchi 

DODOMA

Na Javius Byarushengo 

Ukikutana nao mitaani au kwenye usafiri wa daladala wakiwa wamevaa magwanda yao yenye rangi ya ugoro, unaweza ukahisi ni watu wenye majukumu laini kama ambayo wakati mwingine hayahitaji kuumiza kichwa, lakini watembelee katika maeneo yao ya kazi uone!

Ebu jifanye unatembelea magereza makubwa kama Butimba lililoko jijini Mwanza, Ukonga la  Dar es Salaam, Isanga la Dodoma na mengineyo ujionee kibarua cha hawa jamaa na mazingira wanayofanyia kazi.

Asubuhi na mapema ukifika katika maeneo hayo utakutana na makarandinga yanayoingia na kutoka huku yakiwa yamewabeba watu wenye sura tofauti, wakiwa chini ya ulinzi mkali wa wabeba mitutu.

Watu hao wanaopelekwa kule si wagonjwa wanaokwenda kwenye matibabu, wala si wanafunzi wanaosaka elimu; bali ni watu waliokataliwa na jamii kutokana na matendo yao.

Wapo wanaopelekwa huko kwa kutuhumiwa kuikosea sheria; jina lao maarufu ni mahabusu. Watu hawa hupelekwa kuhifadhiwa huko huku wakiendelea kuhudhuria mahakamani na mwishowe ‘Pilato’ akiwatia hatiani, huhukumiwa faini, kifungo au vyote kwa pamoja au wakikutwa hawana hatia huachiwa huru.

Watu wengine ambao hupelekwa huko ni wafungwa ambao wamehukumiwa kutumikia adhabu zao kwa mujibu wa sheria.

Kimsingi wafungwa na mahabusu wote hawa ambao huletwa magerezani na kukaa huko kwa nyakati tofauti, muda wote huo wa kukaa ndani huwa wako chini ya askari magereza.

Ni askari magereza ambao huingia ndani ya magereza asubuhi, mchana na usiku kwa ajili ya kuhakikisha watu hawa hawatoroki na kurudi mitaani kuhatarisha usalama wa nchi.

Ni askari magereza wanaotumia muda wao mwingi magerezani kwa ajili ya kuwadhibiti mahabusu na wafungwa wenye kesi za  unyang’anyi wa kutumia silaha wasitoroke, mwishowe raia wema walale usingizi fofofo majumbani mwao.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani huku wakidunguliwa na mbu kwa lengo la kuwadhibiti wafungwa na mahabusu wenye kesi za wizi na ujambazi wasitoroke na kurudi mitaani kuwadhuru raia wema wanaoendelea na shuguli za uzalishaji mali.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani huku wakipigwa baridi kali kwa lengo la kuwadhibiti wafungwa na mahabusu wenye kesi za ugaidi ili wasije wakabomoa magereza wakatoroka na hatimaye kuangamiza raia wema wasio na hatia.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani huko kwa lengo la kuwadhibiti wafungwa na mahabusu wenye kesi za mauaji wasitoroke na kurudi mitaani kuendeleza maovu yale yale.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani kwa lengo la kuwazuia wafungwa na mahabusu wenye kesi za ubakaji wasije wakatoroka na kurudi mitaani kuendelea kuwadhuru watoto wetu wa kike, wasichana na wanawake kwa ujumla.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani kwa lengo la kuwachunga wafungwa na mahabusu wenye kesi za dawa za kulevya, uhamiaji haramu, uvuvi haramu na ujangiri.

Ni askari magereza wanaoshinda na kulala magerezani kwa ajili ya kuwachunga wafungwa na mahabusu wenye kesi za rushwa, ufisadi na ubadhirifu mwingine.

Ajabu siku hizi wazazi wamefikia hatua ya kuwaleta watoto wao magerezani ili warekebishwe tabia baada ya wao kushindwa kuwarekebisha huko majumbani, hivyo watoto hao kujikuta mikononi mwa askari magereza.

Si tu wazazi peke yao wanaowapeleka watoto wao magerezani, bali pia hata wengine wamekuwa wakiwapeleka magerezani watu wanaowadai vitu vyao, hivyo wadaiwa hao kujikuta mikononi mwa askari magereza.

Hata hivyo, licha ya majukumu yote haya yanayofanywa na wafunga buti hawa, kuna hali fulani ya upweke inayosababisha nyuso zao ziendelee kuonekana kuwa na mikunjo.

Mikunjo hiyo si ya uajuza! Bali ni ya ukosefu wa  nyuso za bashasha kutokana na ughali wa maisha.

Mikunjo hiyo si ya kimaumbile, bali ni ya ukosefu wa neno la faraja, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakichukuliwa kuwa si chochote ilhali magereza yamekuwapo tangu ukoloni.

Watu hawa watakosaje mikunjo usoni ilhali kwao hakuna vitu vya kuwatia hamasa, mfano kupandishwa vyeo kwa wakati?

Watu hawa watakosaje mikunjo nyusoni wakati wakistaafu wanaendelea kubaki makambini wakisubiri mafao yao ambayo huchukua muda mrefu kulipwa?

Watu hawa watakosaje mikunjo usoni katika mazingira yanayowapa msongo wa mawazo, wakiwaza namna watakavyoishi baada ya kustaafu kutokana na kutumia muda mwingi kazini huku wakilipwa pensheni kiduchu?

Watu hawa watakosaje mikunjo usoni ikiwa mfungwa akitoroka kwa bahati mbaya sheria zilizopo ambazo kimsingi zilirithiwa kutoka kwa wakoloni husababisha mhusika/wahusika kuadhibiwa kwa kukatwa robo mshahara, kutopandishwa cheo kwa muda wa miaka miwili na wakati mwingine kunyimwa kibali cha kujiendeleza kimasomo?

Watu hawa watakosaje mikunjo usoni ilhali hata bungeni michango mingi ya wabunge huwa ni kuwatetea waliofungwa na kusahau wanaosimamia magereza?

Watu hawa watakosaje mikunjo usoni kwa kuzingatia kuwa wanafanyia kazi katika mazingira hatarishi yanayoweza kuhatarisha usalama wao?

Ni ukweli usiopingika kuna askari walishawahi kudhurika kutokana na kupigwa na wafungwa au mahabusu.

Wapo askari walishawahi kumwagiwa kinyesi na mkojo kutoka kwa wafungwa ambao walifanya hivyo kupinga kulazimishwa kwenda  kufanya kazi.

Wapo askari ambao wakati mwingine hujikuta wakiambukizwa magonjwa, mfano kifua kikuu, kutokana na kuwachunga wafungwa au mahabusu wanaoletwa magerezani wakiwa na magonjwa.

Kimsingi watu hawa hawana budi kuangaliwa kwa jicho la huruma na la kipekee, vinginevyo ni giza nene.

Kanuni ya 74 ya Nelson Mandela inaeleza kuhusu mishahara, kwamba inapaswa kuwa minono, mafao ya ajira yanatakiwa kuwa mazuri na mazingira ya kufanyia kazi yanapaswa kuwa mazuri kulingana na mahitaji yao ili kuwavutia wafanyakazi wa magereza.

Ni dhahiri kwamba ulinzi na usalama wa nchi hauna mbadala wake na ndiyo maana mataifa makubwa; mfano Marekani, hujikuta yakitumia bajeti kubwa katika masuala ya ulinzi na usalama.

Ni kweli hali ya uchumi wa nchi si nzuri kutokana na changamoto mbalimbali, lakini suala la ulinzi na usalama ni moyo ambao unatakiwa kuchungwa sana.

Wananchi na watu wote kwa ujumla ili wafanye shughuli zao za maendeleo kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi ni lazima wawe katika mazingira ya usalama, vinginevyo itakuwa ni shida.

Wananchi ili waweze kumuabudu Mungu wao vizuri makanisani na misikitini ni lazima wahakikishiwe usalama wao kwanza.

Wanafunzi ili waweze kusoma vizuri shuleni na vyuoni ni lazima pawepo na hali ya usalama wa kutosha.

Madaktari na wahudumu wote wa afya ili waweze kuwahudumia watu vizuri ni lazima wawe katika mazingira yenye usalama.

Wanasiasa na viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi ya chini mpaka juu ili waweze kuongoza/kutawala vizuri ni lazima pawepo na hali ya kutosha ya usalama.

Unapozungumzia ulinzi na usalama huu, kamwe hauwezi kuwasahau wasimamizi wa magereza.

Na hili linadhihirishwa pindi wafungwa wanapotoka magereza aidha kwa kumaliza vifungo vyao au kwa misamaha mbalimbali ikiwamo ile ya Rais. Ni katika mazingira hayo utasikia usalama wa nchi umeanza kuyumba baada ya wafungwa kupata msamaha.

Juzi juzi tu Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amesema kuwa miongoni mwa watuhumiwa ambao wamekamatwa katika matukio ya ujambazi wamo wafungwa waliotolewa magerezani kutokana na msamaha.

Si tu wafungwa kumaliza vifungo vyao au kupewa msamaha hugeuka tishio, lakini pia historia na mazingira ya sasa duniani yanatuonyesha kuwa kuna baadhi ya mataifa magereza yake yamekuwa yakivamiwa kwa lengo la kuwatorosha wahusika kwa nguvu.

Wakati umewadia serikali kuwaangalia kwa jicho la tatu wasimamizi wa magereza ambao kimsingi ni miongoni mwa watu muhimu wanaosababisha viongozi na watawala walale usingizi mzuri.

Aidha, wabunge mnapojipangia mishahara ya uhakika, posho nzuri na marupurupu kibao, msiwasahau kuwatetea watumishi wa umma, watumishi wa sekta binafsi, wakulima na wafugaji bila kuwasahau wafungwa huru.

[email protected], 0756521119