Wiki iliyopita makala hii iliishia kwa kusema wawili hao (Ruto na Waigui) wanahaha kusafisha majina yao, huku Rais Kenyatta akiwa kimya. Jambo jingine linalomtia tumbo joto (Ruto) ni kitendo cha Odinga kujipenyeza kwenye Mkoa wa Bonde la Ufa, ambao ni ngome kubwa ya Ruto anayeungwa mkono na kabila lake la Wakalenjini. Endelea…

Odinga kwa sasa amejenga uswahiba na Seneta wa Baringo, Gideon  Moi, mwana wa kiume wa mtu aliyeongoza Kenya kwa muda mrefu, Rais mstaafu Daniel arap Moi, na anataka kumtumia kama chambo.

Seneta Moi ni Mkalenjini kama alivyo Ruto, na wawili hao wakikutana kwenye uchaguzi, watazigawa kura za Mkoa wa Bonde la Ufa, ngome kubwa ya Wakalee.

Habari ambazo si rasmi zinasema Rais Kenyatta yuko nyuma ya mpango huo, kuhakikisha uongozi wa nchi unaendelea kushikiliwa na familia kubwa.

Ruto ambaye ameibuka kutoka kusikojulikana na kuwa tajiri na kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Ukanda wa Bonde la Ufa, ni mtoto kutoka familia fukara isiyo na jina lolote.

Lakini hawezi kufua dafu litakapokuja suala la shujaa na mfalme wao, mzee Daniel arap Moi. Tayari jitihada hizo zimezaa matunda na kufanya maisha ya Ruto kuning’inia kwenye uzi mwembamba.

Wakati tukijadili mbio za Odinga kuelekeo Ikulu mwaka 2022, hivi karibuni Umoja wa Afrika (AU) ulimwona na kumpa wadhifa mzito. AU imemteua Odinga kuwa Balozi Maalumu anayesimamia miundombinu katika Bara la Afrika. Kazi yake kubwa atakuwa msimamizi mkuu wa ujenzi wa barabara zinazoliunganisha Bara la Afrika.

Moja ya barabara atakazozisimamia ni ile inayoanzia Cairo, Misri hadi Cape Town, Afrika Kusini. Kwa wadhifa wake mpya, Odinga atakuwa na ofisi katika miji ya Nairobi, Kenya; Johnesburg, Afrika Kusini; Abuja, Nigeria; Cairo, Misri na Adis Abba, Ethiopia yalipo makao makuu ya AU.

Wakati akikubali uteuzi huo, Odinga aliweka bayana kuwa ataanza na barabara hiyo ya Cairo hadi Afrika Kusini, kwa alichoeleza kuwa mipango yake ilikwisha kukamilika ila ilitupwa kwenye makabati bila kutekelezwa.

Uteuzi huu umeziongeza kasi mbilio za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye atamaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kikatiba mwaka 2022. Mbio hizi zimeibua mgawanyiko wa waziwazi ndani na nje ya Ikulu, zikiibuka kambi mbili hasimu ndani ya serikali moja ya Jubilee.

Naibu Rais, William Ruto na wapambe wake wanaamini kuwa sasa Odinga yuko kwenye ‘levo’ ya kimataifa, hatakuwa na muda wa kuhangaika na siasa za ndani ya Kenya, na wakati wowote atatangaza kung’atuka na kuacha milango wazi kwa Ruto.

Ruto ambaye amekuwa akizunguka sehemu mbalimbali za nchi hiyo ‘akiwajaza watu mapesa’ kupitia ‘harambee’ mbalimbali, anaona Odinga kama ndiye mtu pekee anayemnyima usingizi.

Hata hivyo ndani ya Jubilee kuna kundi jingine la wapambe wa Uhuru ambao wanawapinga wenzao waziwazi, wakiwa na imani kuwa bado Odinga ana mchango kwa taifa lao. Wanaungana na wapinzani wanaobeza maoni ya wapambe wa Ruto na kuyaita ndoto za mchana. Wanasema ‘baba yao’ amelamba dume na siyo tena saizi ya Ruto.

Odinga mwenyewe amekaa kimya na ameacha kabisa kuchangia hoja hiyo inayohusu mustakabali wake kisiasa. Zifuatazo ni nukuu mbalimbali za wapambe hao kutoka kwenye mitandao na vyanzo vingine. “Hatutarajii kumwona (Odinga) akihangaika na siasa za ndani. Huyu atakuwa ‘busy’ na majukumu yake mapya ya kimataifa yenye lengo la kuliletea maendeleo bara letu,” anasema Kimani Ichungwa, Mbunge wa Kikuyu na mfuasi sugu wa Ruto.

“Mkakati wake kuitisha kura za maoni kubadilisha Katiba nadhani umefikia tamati. Asante Rais kwa kutia mkono wako katika uteuzi wa Odinga na kumshawishi akaukubali,” anasema Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.

Je, unajua kuwa Odinga alipata kuukataa Ubalozi? Usikose JAMHURI toleo la wiki ijayo.

By Jamhuri