Wiki iliyopita makala hii iliishia katika aya iliyosema; (Raila) Odinga mwenyewe na Najib Balala (Waziri wa sasa wa Utalii), waliwakilisha masilahi ya Mkoa wa Pwani, huku Kalonzo na Charity Ngilu wakiwakilisha masilahi ya Ukambani. (William) Ruto (kabla hawajafarakana), aliyekuwa ameuacha Ukatibu Mkuu wa KANU, aliuwakilisha vema Mkoa wa Bonde la Ufa katika chombo hicho na kuzoa kura nyingi za kabila la Kalenjini. Endelea…

Rais Mwai Kibaki aliamua kuupiga chini mchakato wa kuundwa Katiba mpya na baada ya Odinga kugundua kwamba amewashtukia,  aliungana  na baadhi ya mawaziri wakafanya ‘uasi’ dhidi ya rais wao na  kuanzisha harakati za kuandikwa kwa Katiba mpya kwa nguvu. Walimshinikiza mpaka akasalimu amri na kuitisha kura ya maoni.

Odinga akiungwa mkono zaidi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kalonzo Musyoka, waliunda ngome yao imara ambayo ilitumia kaulimbiu ya ‘Chungwa’  kudai Katiba mpya na upande wa kina Kibaki wakatumia kaulimbiu ya ‘Ndizi’ kupinga kuandikwa Katiba mpya.

Kambi ya Chungwa iliibuka kidedea na kumbwaga bosi wao Kibaki katika matokeo ya kura hiyo ya maoni. Ndipo ikazaliwa Katiba ya mwaka 2010.  Uvulimu ulimshinda Kibaki na akaamua kuwafuta kazi Odinga na kundi lake ambao baada ya hapo waliingia ‘msituni’ na kuanzisha vuguvugu jipya la kisiasa la Orange Democratic Movement (ODM), ambalo mpaka sasa kinara wake ni Odinga.

Aliipanga vilivyo ODM na kumpa wakati mgumu sana Kibaki wakati akitetea kiti chake mwaka 2007 katika uchaguzi uliokwisha kwa vurugu vilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 na maelfu kadhaa kuyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani.

Odinga alitengeneza chombo cha juu cha uamuzi ndani ya ODM, kikienda sawasawa na siasa za kikabila, huku kikiwakilisha karibu mikoa na jamii zote zenye nguvu. Chombo hicho kilichoitwa ‘Pentagon’ kilimsaidia kupata kura nyingi na viti vya kutosha katika bunge la taifa.

Watu wenye ushawishi kutoka jamii mbalimbali walikuwa ndani ya chombo hicho. Yeye na Najibu Balala (Waziri wa sasa wa Utalii ) waliwakilisha masilahi ya eneo la Pwani lenye kaunti nyingi zilizozolewa na ODM.

Ukambani waliwakilishwa na Kalonzo Msyoka, pamoja na Waziri wa Maji aliyekuwa mbia wa Kibaki awali wakati wa kampeni mwaka 2007, mama wa chuma, Charity Ngilu. Nilibahatika kuona kwa macho kampeni hizo na nilishuhudia tukio la Mama Ngilu kujiunga na ODM na kupewa nafasi kwenye Pentagon.

Jioni siku hiyo Ngilu alitoka kwenye ofisi za Wizara ya Maji pale karibu na viwanja vya Uhuru (Uhuru Park), katikati ya Jiji la Nairobi na kuingia uwanja wa kampeni akiwa kwenye gari la serikali. Hata hivyo aliacha gari hilo baada ya kampeni siku hiyo.

Kwa jinsi walivyokuwa wamejipamba na staili yao ya kuongea jukwaani, ilikuwa ni kivutio kuwatazama. Ruto aliuwakilisha Mkoa wa Bonde la Ufa, hasa watu wa kabila lake la Kalenjini. Mkoa wa Magharibi na viunga vyake viliwakilishwa na aliyepata kuwa Makamu wa Rais, Musalia Mudavadi.

Kesi  mbili za uhalifu wa kivita ambazo moja ilimhusu Kenyatta na wapambe wake na nyingine ya Ruto na wapambe wake, baadaye zilizua mpasuko mkubwa ndani ya Pentagon, uliosababisha Ruto kujiengua na kuunda chama chake cha URP ambacho baadaye kiliungana na cha Uhuru kuunda ushirikiano wa Jubilee.

Kabla ya  Jubilee, Uhuru Kenyatta alikuwa ameachana na wadhifa wake wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni na Kiongozi Mkuu wa KANU na kuungana na Mwai Kibaki, katika Chama kipya cha PNU, kilichotumiwa na Kibaki kutetea kiti chake. Vuguguvugu la NARC baadaye ilibadilishwa na kuwa chama na kubaki mikononi mwa Waziri wa zamani wa Sheria,  Martha Karua.

Tofauti na hapa kwetu Tanzania, Katiba ya Kenya inaruhusu mtu kugombea urais kupitia muungano maalumu, kama ilivyokuwa NARC, ODM, Jubilee n.k. Hapa kwetu Edward Lowassa alishindwa kugombea kwa tiketi ya UKAWA na badala yake akafanya hivyo kupitia Chama mshirika cha Chadema. Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, alilazimika kujivua uanachana wa CUF ili aweze kupata nafasi hiyo.

By Jamhuri