Katika gazeti hili kuna barua iliyoandikwa na mmoja wa Watanzania walio kwenye magereza Hong Kong, kutokana na usafirishaji mihadarati.

Barua hiyo ambayo ina vimelea vingi vya ukweli inajieleza wazi. Anachojaribu kufanya ni kuwaonya Watanzania wenzake kutojihusisha na biashara hiyo. Amefikia hatua hiyo kutokana na adha na mateso makubwa aliyoyapata kuanzia kumeza mihadarati hadi kukamatwa kwake.

 

Inakisiwa kwamba Watanzania zaidi ya 200 ama wamefungwa, au wapo mahabusu huko Hong Kong na China pekee. Julai 26, Watanzania wengine wawili wamekamatwa Hong Kong wakiwa na shehena kubwa ya mihadarati.

Hao ni tofauti kabisa na Watanzania wengine wawili – mabinti wadogo – waliokamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za mihadarati. Aidha, bado tuna kumbukumbu ya msichana mwingine wa Tanzania aliyekamatwa nchini Misri. Orodha ni ndefu sana.

 

Hizi ni habari mbaya kwa sifa ya Taifa letu. Jina la Tanzania sasa linanuka mbele ya jumuiya ya kimataifa. Inatuwia vigumu kuamini kama wote walio kwenye magereza na mahabusu hizo ni Watanzania kweli. Tunasema hivyo kwa sababu hati za kusafiria za Tanzania ni rahisi mno kupatikana. Hatua hiyo imewafanya matapeli wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani kuzipata.

 

Mtandao wa biashara ya dawa za kulevya ni mkubwa sana. Unawahusisha wanasiasa, wafanyabiashara na matajiri. Wanaoumizwa zaidi ya biashara hii ya kipuuzi ni vijana masikini wanaokuwa tayari kuhatarisha maisha yao kwa ujira mdogo.

 

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa hali ilivyo sasa umepoteza kabisa heshima ya mwasisi huyo wa Taifa. Umekuwa upenyo wa kusafirisha mihadarati. Si siri kuwa watumishi wa uwanja huo ndiyo wahusika wakuu wa upuuzi huu.

 

Tunashangaa kuona kuwa pamoja na kubainika mwanya unaopitisha mihadarati katika uwanja huo, hakuna hatua zozote kali zilizochukuliwa dhidi ya wahusika. Kuna ugumu gani kuwabaini wanaoruhusu mihadarati ipite?

 

Tunatoa wito kwa mamlaka zinazohusika kusimama kidete kupambana na biashara hii inayoliangamiza Taifa. Kama kiwango kinachokamatwa nje ya nchi ni kikubwa kiasi hicho, je, kile kinachosalia hapa nchini kwa soko la ndani si kweli kuwa ni kikubwa zaidi?

 

Sote sasa tunaziona athari za biashara hii. Vijana ambao ndiyo nguzo ya uchumi wa Taifa, wamekuwa mazezeta. Hospitali zimelemewa na waathiriwa wa mihadarati. Gharama za kuwatibu ni kubwa mno. Matukio ya uhalifu yanaongezeka.

 

Vita dhidi ya biashara hii, pamoja na ukweli kuwa ni wajibu wa vyombo vya dola, bado inahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwamo wananchi. Wauza mihadarati tunaishi nao. Tunawatambua. Hatuna budi kuwaweka hadharani tukiwaeleza wazi kuwa biashara yao ni mauti kwa kizazi chetu.

 

Tunapendekeza sheria zibadilishwe ili adhabu kali zitolewe kwa wahusika. Hii ya kuweka adhabu ya faini na kifungo kidogo inachochea na kuifanya biashara hii haramu ishamiri nchini. Muhimu zaidi ni kuanza kuwashughulikia mapapa wa biashara hii ambao wakati fulani Rais Jakaya Kikwete alisema ana orodha yao. Tunamuuliza, “Kasi hiyo ya kuwashughulikia hao mapapa wa mihadarati imezimwa na nini? Je, orodha aliyokuwa nayo Rais ni feki?”

 

1294 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!