Wezi wa fedha za Smart Partnership washitakiwe

Kwa wiki kadhaa gazeti la JAMHURI tumeandika habari za ufisadi wa mamilioni ya shilingi kwenye Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue).

Mkutano huo uligharimu Sh zaidi ya bilioni nane, lakini sehemu ya fedha hizo zilitafunwa na wezi ambao hawana hofu yoyote, si kwa Serikali bali hata kwa Mungu.

 

Baada ya kuandika habari hizo, Mhariri Mtendaji na Mhariri wa JAMHURI walihojiwa Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam. Walihojiwa si kwa sababu habari zilizoandikwa zilikuwa za uongo, la hasha! Kilichowakasirisha wakubwa ni matumizi ya barua yenye mhuri wenye neno “Secret” kutoka Ikulu.

 

Kwa maelezo ya wakubwa hao, uchapaji neno hilo ulikuwa ni ukiukwaji wa Sheria ya Usalama wa Taifa! Kwao, hilo neno ni hatari sana kuliko fedha za umma zilizotafunwa.  Kinachosikitisha ni kuwa hadi sasa kinachojulikana kwa umma ni kuhojiwa kwa waandishi wa habari, lakini si kwa hao waliotajwa.

 

JAMHURI tulidiriki hata kutaja kampuni hewa tatu ambazo wahusika waliziunda kiujanja-ujanja na kupewa zabuni kinyume kabisa na Sheria ya Ununuzi.

 

Uhuni uliofanywa kwenye ulaji fedha hizi za umma unajulikana vema. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.

 

Kwenye kikao cha mwisho, Sefue alisema ingawa yeye ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.

 

Akasema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya shilingi yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.

 

Msimamo wa viongozi wa Serikali umekuwa kwamba vyombo vya habari na raia wema wajitokeze kushiriki kupambana na wala rushwa na watu wanaotumia vibaya madaraka na ofisi za umma.

 

Sisi ni miongoni mwa tuliojitokeza kwa moyo wa dhati kabisa kutekeleza wito huu. Lakini tunapoona Serikali inakaa kimya, si tu kwamba hali hiyo inasikitisha, bali pia inawakatisha tamaa wananchi wanaochukizwa na matukio ya wizi wa fedha na mali za umma.

 

Tunatoa wito kwa wanaohusika kujitokeza kwa umma na kuueleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika wote. Tunaomba jambo hili lipewe msukumo kwa sababu bila hivyo Tanzania itakuwa nchi ya watu kuiba na kuachwa watambe.

 

Fedha zilizoibwa ni za umma. Wenye kampuni hewa wamekwepa kodi ambazo kama zingelipwa, bila shaka zingetumika kuboresha maisha ya wananchi. Adhabu itolewe kwa wenye kampuni hizo na maofisa wa Serikali waliowasaidia kufanikisha wizi huo.

 

Kama maofisa wa Ikulu na Polisi walikuwa wepesi kuwahoji waandishi kwa sababu tu ya neno ‘secret”, wawe wepesi pia kuwahoji na kuwatangaza hadharani washukiwa wote wa fedha za Smart Partnership, na kuwafikisha mahakamani. Watanzania wamechoka kila siku kuona wezi wakienziwa katika Taifa letu.