Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanajipanga kukutana wiki hii kutafuta ufumbuzi wa mgogoro mkubwa unaoendelea kufukuta katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera. Imeshadhihirika wazi kuwa mgogoro huo ni baina ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na Meya Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.

Inaelezwa pia kwamba kila upande unaungwa mkono na kundi la viongozi wa chama na serikali hali ambayo inaweza kutoa mwanya mkubwa wa kudhoofisha maendeleo ya wananchi wasio na hatia katika Manispaa hiyo kama si Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa jumla.

 

Tayari mgogoro huo umesababisha kutimuliwa kwa madiwani wanane kupitia Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kagera, ingawa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imetangaza kusitisha uamuzi huo.

 

Ni dhahiri kwamba mgogoro huo imeaathiri kwa kiasi fulani maendeleo ya wananchi wa Bukoba kutokana na ukweli kwamba viongozi wanaovutana wamebeba dhamana kubwa ya kuhamasisha na kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi.

 

Uchunguzi umebaini kwamba mgogoro huo kwa upande mwingine, umeghubikwa na maslahi binafsi, yakilenga zaidi nafasi ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao.  Viongozi kadhaa wa ngazi za juu CCM na serikalini wamejaribu kuingilia kati kwa nyakati tofauti lakini juhudi zao hazijaa matunda.

 

Matumaini ya wengi ni kwamba Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kitajadili na hatimaye kuibuka na uamuzi sahihi utakaosuluhisha mgogoro huo kunusuru kudhoofisha maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba na Mkoa wa Kagera.

 

Kikubwa zaidi kinachotarajiwa ni kwamba uwazi na haki vitatawala katika kusaka ufumbuzi wa mvutano huo. Upendeleo wa aina yoyote usipewe nafasi katika kikao hicho ili kuwafanya wananchi wasipoteze imani na kamati hiyo.

 

Sisi JAMHURI tungependa kuona umoja, upendo na mshikamano unakuwa ngao ya viongozi wote wa vyama na serikali katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa jumla, kwa kuwa hizo ndizo nyenzo kuu za kufikia mafanikio ya kisekta.

 

Kamati Kuu ya CCM isisite kuwakumbusha viongozi wanaovutana kwamba mgogoro wanaouendeleza mwisho wa siku utageuka mwiba kwao kiasi cha kutofikia malengo ya maslahi binafsi wanayotafuta.

 

Uamuzi utakaotolewa na Kamati Kuu ya CCM uwe wa hekima, busara na haki, lakini pia utekelezwe kwa vitendo na uwe fundisho kwa viongozi wengine wenye nia mbaya ya kuzusha migogoro kwa maslahi yao binafsi.

 

Hatutarajii kuona kikao hicho cha Kamati Kuu ya CCM ambacho kitagharimu fedha nyingi kinamalizika bila kupata ufumbuzi thabiti wa mgogoro huo. Kufanya hivyo kitakuwa kimetumia vibaya madaraka na fedha za chama.

 

Masikio na macho ya Watanzania sasa yanaelekezwa katika kikao hicho cha Kamati Kuu ya CCM wiki hii wakitarajia uamuzi mgumu na wa haki utakaoleta ufumbuzi na kuufanya mgogoro huo kubaki historia. Wahenga walisema  Penye nia pana njia.

By Jamhuri