Wiki iliyopita, Rais John Magufuli, alitangaza utaratibu mpya wa uingizaji sukari nchini. Uamuzi huu unalenga kulinda viwanda na ajira kwa Watanzania. Ni uamuzi mzuri kabisa.

Baada ya kumsikiliza, na kwa kuwa lengo ni kuwalinda wakulima wetu, ajira kwa vijana na soko la bidhaa zinazozalishwa nchini, nimeonelea vema nigusie bidhaa ambayo kwa namna fulani uingizwaji wake nchini una athari kubwa kwa wakulima, viwanda na ajira kwa Watanzania.

Uingizaji mafuta ya kula ya mawese kutoka Malaysia na Indonesia, tena bila kuyalipia ushuru, ni kifo kwa wakulima wetu hapa nchini. Kibaya zaidi, wakulima wa huko wanapata ruzuku kutoka serikali zao kwa hiyo kuruhusu mafuta hayo bila kodi ni kutangaza kifo kwa wakulima wetu.

Kampuni zinazoingiza mafuta ya mawese zinaihadaa Serikali yetu kwa kusema zinaingiza mafuta ghafi! Hii si kweli hata kidogo. Mafuta hayo huwa yameshasafishwa kwa asilimia zaidi ya 90. Bahati nzuri wapo viongozi wetu kama Dk. Chrisant Mzindakaya, Dk. Zainabu Gama na Dk. Kilontsi Mpologomyi ambao walifuatilia vema hadaa hii na kubaini uongo mwingi.

Wakati fulani ushuru kwa mafuta hayo ulikuwa asilimia 10, lakini katika namna isiyoashiria uadilifu, Waziri wa Fedha wa wakati huo, Dk. Mustafa Mkulo, mwaka 2009 alifuta ushuru huo na kuwa sifuri!

Mawese, mbali ya kutoa mafuta, ni malighafi kwa utengezaji sabuni na vyombo mbalimbali kama viti, meza, sahani, ndoo, na kadhalika.

Hawa waagizaji wakishapata mafuta, malighafi inayobaki huitumia kutengeneza bidhaa hizo. Wale wenye viwanda vidogo wanapohitaji malighafi, njia pekee ya kuwanyima ni kuwauzia kwa bei ghali. Matokeo yake ni kufa kwa viwanda vingi vya aina hiyo hapa nchini. Hatua hiyo imewafanya ‘wababe’ wa uagizaji mafuta waendelee kutamba wao wenyewe kwenye mafuta, sabuni na utengenezaji bidhaa kama viti, meza, sahani na kadhalika.

Kufutwa kwa ushuru kwenye mafuta ya mawese ni mkakati madhubuti uliosukwa na wafanyabiashara wakubwa na kufanikiwa kuwarubuni ‘mabwana mipango’ wa serikali yetu. Kuna dalili zote zinazoashiria kuwapo kwa ushawishi fulani ulio juu ya ushawishi wa maneno matupu!

Wastani wa mafuta ya mawese yanayoingizwa nchini ni tani 300,000 kwa mwaka. Kiwango hiki kingeweza kuipatia serikali mabilioni ya shilingi kama kodi na ushuru. Kwa kuwa Serikali ipo kwenye maandalizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, litakuwa jambo la maana mno endapo ushuru kwenye mafuta ya mawese yanayongizwa nchini utarejeshwa. Mwaka 2009 ushuru ulipofutwa ulikuwa asililimia 10; Serikali sasa ione busara ya kuongeza kiwango hicho walau hadi asilimia 20. Hiyo itasaidia kulinda viwanda vyetu vya ndani na ajira kwa Watanzania.

Hatuwezi kujenga viwanda vipya vya mafuta ya kula endapo hakutakuwapo malighafi ya kutosha. Malighafi inazalishwa na wakulima. Kilimo hakiwezi kustawi endapo soko la bidhaa, ama halipo, au kama lipo, basi ni kwa bei ndogo mno.

Hoja ya kwamba nchi yetu ina uhaba wa mafuta ya kula; na kwa sababu hiyo lazima tuagize kutoka nje, kwa maneno mengine ni kukidumaza kilimo chetu. Mahitaji ya soko ndiyo njia pekee ya kuwahamasisha vijana wengi kukipenda kilimo. Rais Magufuli ameanza kwenye sukari, sasa tumwombe atoe tamko kwenye mafuta ya kula. Akimaliza huko, afanye hivyo kwenye maziwa na bidhaa nyingine nyingi ambazo Watanzania tuna uwezo wa kuzizalisha nchini mwetu.

Juni 2009, niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Kuna jambo tumemkosea Mungu!”

Niliiandika baada ya Serikali kufuta ushuru kwenye mafuta ya mawese. Kwa muktadha wa hali ya mambo ilivyo, nimeona nirejee makala hiyo- neno kwa neno- kama njia ya kuonyesha namna nilivyolishupalia suala hili kwa miaka mingi.

Makala hiyo ilisomeka hivi: Wakulima makabwela wa Tanzania wameumizwa. Nguvu za fedha zimewashinda. Bunge, chombo kilichoundwa kwa ajili ya kuwatetea, limelemewa kwa hoja fifi za viongozi wa Wizara ya Fedha na Uchumi.

Uamuzi hatari wa kuruhusu kuingizwa nchini mafuta ya kula, yanayoitwa mafuta ghafi, umebarikiwa na Bunge letu. Sasa kinachosubiriwa ni maumivu na majuto kwa wakulima makabwela wa nchi yetu.

Serikali yetu imeona ni busara sana kuwapa misamaha “maaskofu na masheikh” wanaotokana na makanisa na misikiti vinavyoibuka kila siku kama uyoga. Busara hiyo hiyo kwa wakulima imepindishwa.

Wakulima wa nafaka zinazotumika kuzalisha mafuta ya kula, wamekosa mkombozi, ingawa watetezi walikuwapo. Kilimo cha ufuta, mawese, pamba, alizeti na aina hiyo ya mimea, kimepata pigo.

Juzi jioni Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria wa Fedha wa mwaka 2009 kwa kubariki mafuta ya kula yanayoitwa ghafi, kuondolewa ushuru wa asilimia 10. Sasa ushuru ni sifuri!

Kwa uamuzi huo, wakulima wa Malaysia, Indonesia na kwingineko barani Asia na Ulaya, sasa ni kicheko. Haitashangaza kuwasikia wakiandaa tuzo maalumu kwa viongozi wetu kutokana na kituko hiki walichofanya. Wala haitashangaza kusikia viongozi na maofisa wa Wizara ya Fedha na Uchumi wakipata mialiko kwenda kupongezwa!

Wiki iliyopita nilieleza hisia zangu kuhusu uamuzi wa Serikali. Nikaeleza namna watangulizi wa Mustafa Mkulo walivyokataa kubariki udhalimu huu wa kuwaumiza wakulima. Lakini wapo wasomaji walionikosoa. Wakati mimi nikisema suala hilo lilianza katika mwaka wa fedha wa 2006/2007; wasomaji wanasema lilianza mwaka 1996.

Mmoja wa wasomaji hao ambaye alikuwa mmoja wa viongozi waandamizi serikalini, anasema walishafuatwa na mifuko ya fedha, lakini mapenzi yao kwa wakulima na nchi yao Tanzania, vikawasuta. Wakakwamisha jambo hilo.

Mwaka 2001 suala hilo likaibuka tena kwa nguvu zote, lakini mawaziri watangulizi wa Mkulo walikataa kata kata. Akaja Zakia Meghji, naye akakataa kata kata suala hilo.

Juzi, Mbunge wa Kibaha Mjini, Dk. Zainab Gama, akilengwa lengwa machoni bungeni, alihoji: “Imekuwaje mawaziri wote waliotangulia walikataa suala hili (kufuta ushuru kwenye mafuta hayo), lakini Mkulo amekubali?”

Serikali kuona hivyo ikaandaa majibu. Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha na Uchumi wakaandaa majibu ya kutupumbaza sisi tuliozaliwa na kusomeshwa kwa nguvu za jembe la mkono-sisi ambao tumetibiwa na kupewa huduma nyingine muhimu kutokana na alizeti, mbegu za pamba, mawese, ufuta, mahindi na kadhalika.

Viongozi hao wakatoa takwimu ndefu ambazo kwa mwenye akili njema hawezi kuzikubali. Wakatangaza eti matokeo ya utafiti kuonyesha kuwa nafaka zinazozalishwa nchini haziwezi kumudu kuzalisha mafuta ya kukidhi mahitaji.

Ni kwa sababu hiyo, wameapa kulaumiwa kwa lolote litakalosemwa, lakini wahakikishe kuwa wale wamiliki wa viwanda vya mafuta ya kula, wanaingiza mafuta.

Juzi juzi tu tumelaumu Watanzania wenye asili ya Asia kushika uchumi wa nchi. Mimi nilipinga. Nilipinga kwa sababu wanaowapa utajiri huo ni weusi wenye akili zisizofanya kazi kuwakomboa weusi wenzao. Leo waliobariki mawese kutoka nje iingizwe bure nchini, ni wabunge.

Dk. Gama, hata alipotaka kujua nini kitawapata wafanyabiashara wakibainika kuwa wanachoingiza nchini ni mafuta yaliyokwishasafishwa, majibu yakakosekana. Mwenyekiti aliyekuwa akiongoza Bunge, akasema hiyo ni kazi ya watendaji. Hayawezi kuhojiwa kwenye sheria iliyokuwa ikipitishwa! Kwa msimamo huo sioni kitu gani kitawapa mshituko serikali kuwabana waagizaji hao, kama imeshindwa kuwaonea huruma wakulima wake.

 

>>ITAENDELEA

3919 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!